Jumapili, tarehe 8 Novemba, 2020
Leo ni Jumapili tarehe 22 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1442 Hijria sawa na tarehe 8 Novemba mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 1438 iliyopita, yaani tarehe 22 Rabiul-Awwal mwaka wa 4 Hijiria, vilianza vita kati ya Waislamu na Mayahudi wa kabila la Bani Nadhir baada ya watu wa kabila hilo kufanya njama za kutaka kumuua Mtume Muhammad (SAW). Bani Nadhir ni moja ya makundi matatu ya Mayahudi waliokuwa wakiishi katika vitongoji vya mji wa Madina, ambao kwa mujibu wa mkataba waliotiliana saini na Mtume (SAW), hawakutakiwa kuchukua hatua yoyote iliyo dhidi ya mtukufu huyo na Waislamu kwa ujumla. Baada ya Mayahudi kuvunja mkataba huo, Mtume Muhammad (SAW) aliwaamuru waondoke Madina. Hata hivyo Mayahudi hao ambao tayari walikuwa wamepewa ahadi za kuungwa mkono na wanafiki wa mji huo, hawakuwa tayari kutii amri hiyo. Ni kwa sababu hiyo, ndipo mtukufu Mtume kwa kushirikiana na Waislamu akazizingira ngome za watu hao kwa muda wa siku kadhaa na kuwalazimisha kuondoka katika maeneo yao.
Siku kama ya leo miaka 364 iliyopita, alizawa Edmond Halley, mtaalamu wa nyota wa nchini Uingereza. Halley alisoma katika kitengo cha Queen kilicho chini ya chuo kikuu cha Oxford, nchini humo na kuanza kujishughulisha na masuala ya utafiti wa nyota akiwa kijana mdogo, huku akifanya safari kuelekeaa kusini mwa dunia ya Bahari ya Atlantic. Edmond Halley alichukua muda mwingi katika kutalii nyota ambapo alipata kufahamu kwamba, kama ilivyo kwa sayari, nyota nazo zina mviringo na mzunguko wake maalumu. Mwaka 1704 alikuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Oxford, huku akiarifishwa kuwa mtaalamu wa masuala ya nyota mwaka 1720. Halley alifariki dunia mwaka 1742 wakati akijishughulisha na masuala ya nyota.
Katika siku kama ya leo miaka 346 iliyopita, alifariki dunia John Milton, malenga wa Kiingereza. Kazi za kwanza za ushairi za John Milton zilijulikana kwa majina ya Roho na Huzuni na Roho ya Furaha. Kazi nyingine ya uandishi ya John Milton ni ile aliyoipa jina la Paradise Lost. Malenga Milton alikuwa akitetea suala la kutenganishwa serikali na kanisa, kuweko uhuru wa kuabudu na wakati huo huo aliunga mkono uchujaji wa taarifa uliokuwa ukifanywa na serikali.
Siku kama ya leo miaka 125 iliyopita sawa na tarehe 8 Novemba mwaka 1895, miale ya X iligunduliwa na Wilhem Conrad Rontgen, mwanafizikia na mwanasayansi maarufu wa Ujerumani. Mtaalamu huyo mwaka 1901 alitunukiwa tuzo ya Nobel kwa kufanikiwa kugundua miale hiyo. Kwa kuwa hakutambua miale aliyoigundua, Rontgen aliamua kuipa jina la X. Miale hiyo hupenya kwa urahisi katika mwili wa mwanadamu na kwa ajili hiyo ni njia nzuri zaidi ya kuchukua taswira ya viungo au picha ya X-ray inayotumiwa kujua sehemu za ndani ya mwili zilizodhurika au kuvunjika.
Na siku kama ya leo miaka 120 iliyopita alizaliwa Bi Margaret Mitchell mwandishi wa Kimarekani huko Atlanta katika jimbo la Georgia nchini humo. Baba yake Bi Mitchell alikuwa wakili wa mahakama. Kwa muda fulani alisomea fani ya udaktari, lakini baadaye alilazimika kukatisha masomo hayo kutokana na majonzi aliyokuwa nayo kufuatia kifo cha baba yake. Margaret allianza kazi ya uandishi akiwa na miaka 22. Alizidi kupata umashuhuri baada ya kuchapisha riwaya yake aliyoiita kwa jina la "Gone with The Wind."
Na katika siku kama ya leo miaka 44 iliyopiita, Sheikh Nusratullah Ansari mwanamapambano wa na mwanamapinduzi wa Iran alikufa shahidi kutokana na mateso ya makachero wa Shirika la Usalama wa Taifa la utawala wa Shah lililojulikana kwa jina la SAVAK. Hujjatul Islam Nusratullah Ansari alizaliwa katika eneo la Buin Zahra. Sambamba na kupata masomo ya kidini alikuwa akiendesha harakati za mapambano ya kisiasa dhidi ya utawala wa kidhalimu wa Shah nchini Iran. Hatimaye mwaka 1354 Hijria Shamsia alitiwa mbaroni na makachero wa Shah na kuuawa shahidi katika siku kama ya leo baada ya miezi sita ya mateso.