Nov 12, 2020 22:04 UTC
  • Ijumaa tarehe 13 Novemba 2020

Leo ni Ijumaa tarehe 27 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1442 Hijria sawa na Novemba 13 mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 992 iliyopita aliaga dunia mshairi na mwandishi maarufu wa Kiarabu Abul Alaa al Maarri. Alizaliwa mwaka 363 Hijria katika Syria ya sasa na kupata elimu ya lugha na fasihi katika eneo la Ma'arra na miji mingine ya Sham. Baadaye alikwenda Baghdad, Iraq kwa elimu ya juu zaidi. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri la "Risalatul Ghufran" na "al Aamali."

Abul Alaa al Maarri

Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita mwafaka na tarehe 22 Aban mwaka 1344 Hijria Shamsia, alifariki dunia mwandishi na mhakiki mkubwa wa Kiirani, Said Nafisi akiwa na umri wa miaka 71. Baada ya kupata elimu ya upili, Nafisi alielekea Ufaransa kwa ajili ya elimu ya juu. Baada ya kumaliza masomo yake huko Ufaransa alirejea Iran na kufunza katika vyuo vikuu hapa nchini. Said Nafisi ameandika na kutarjumu vitabu zaidi ya 180 ikiwemo kamusi ya lugha ya Kifaransa na Kifarsi.

Said Nafisi

Siku kama ya leo Miaka 52 iliyopita, Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim, mkuu wa kituo cha kidini cha Najaf aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 92. Baada ya kuaga dunia Ayatullah Burujerdi ambaye alikuwa mar'ja' mashuhuri katika ulimwengu wa Kiislamu, Ayatulah Hakim alichukua nafasi yake na kufuatwa na Waislamu wengi na hasa wa Iraq, kuhusiana na masuala ya kifik'hi. Alipambana vikali na kila kundi au watu waliojaribu kuharibu jina la Uislamu. Fatua yake mashuhuri ya kupinga fikra ya ukomunisti dhidi ya mafundisho ya dini ilileta mabadiliko makubwa nchin Iraq. Fatua hiyo pia ilimpelekea kutoa amri ya kupigana jihadi dhidi ya utawala haramu wa Israel. Ujenzi wa maktaba, shule na vituo vya kidini na kiutamaduni pamoja na uandishi wa vitabu kama vile Mustamsak Urwat al-Wuthqah na Nahjul Faqaha ni miongoni mwa vitabu mashuhuri vilivyoandikwa na mwanazuoni huyo mashuhuri wa Kiislamu.

Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim

Siku kama ya leo miaka 50 iliyopita hayati Hafidh Assad alichukua hatamu za uongozi wa Syria baada ya mapinduzi ya kijeshi mwaka 1970 na baadaye akachaguliwa kuwa kiongozi wa chama cha Baath. Hafidh Assad alizaliwa mwaka 1930 na mwaka 1964 alichaguliwa kuwa kamanda wa kikosi cha anga cha jeshi la Syria. Miaka mitatu baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo. Hafidh Assad alifariki dunia mwezi Juni mwaka 2000 baada ya kuugua kwa muda mrefu. 

Hafidh Assad

Miaka 50 iliyopita katika siku kama ya leo, mwafaka na tarehe 13 Novemba 1970, tufani kubwa na kimbunga cha kutisha kiliikumba nchi ya Bangladesh. Janga hilo lilitokea wakati mapambano ya Wabangali kwa ajili ya kujitenga na Pakistan na kupata uhuru yalipokuwa kileleni. Tufani hiyo kubwa ilisababisha vifo vya watu laki mbili na kujeruhi wengine laki nane. Kimbunga na tufani hiyo pia iliwalazimisha mamia ya maelfu ya watu kukimbia makazi yao na kusababisha hasara kubwa katika mashamba, viwanda, makazi ya raia na miundombinu ya nchi hiyo. Bangladesh ni miongoni mwa nchi zinazokumbwa na majanga ya kimaumbile kama vimbunga, tufani na mafuriko ya mara kwa mara.

Na miaka 5 iliyopita tarehe 13 Novemba saa tatu na dakika 16 usiku kwa wakati wa Ulaya ya Kati milipuko kadhaa ya kigaidi ilitokea katika maeneo nambari 1, 10 na 11 ya jiji la Paris nchini Ufaransa na kuua watu 130 na kujeruhiwa wengine 368. Baadhi ya milipuko hiyo ilitokea karibu na uwanja wa michezo wa Stade de France ulioko kaskazini mwa jiji la Paris wakati wa mechi ya mpira wa miguu kati ya timu za taifa za Ufaransa na Ujerumani. Wakati huo huo watu wengine 87 waliuawa katika utekeji nyara uliofanyika katika ukumbi wa michezo ya kuigiza wa Bataclan mjini Paris. Mashambulizi hayo yalihesabiwa kuwa makubwa zaidi kutokea nchini Ufaransa baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Siku moja baadaye kundi la kigaidi la Daesh lilitangaza kuwa ndilo lililohusika na mashambulizi hayo.

Mashambulizi ya kigaidi ya Paris