Nov 13, 2020 23:01 UTC
  • Jumamosi, 14 Novemba, 2020

Leo ni Jumamosi tarehe 28 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1442 Hijria sawa na tarehe 14 Novemba 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 487 iliyopita, ardhi ya Ecuador inayopatikana huko Amerika ya Kusini iligunduliwa na wavumbuzi wa Kihispania na kuunganishwa na ardhi zilizokuwa zikidhibitiwa na Uhispania. Ecuador ilikoloniwa na Uhispania kwa karne tatu. Hata hivyo mwaka 1822 wananchi wapigania ukombozi wa nchi hiyo chini ya uongozi wa Simon Bolivar walifanikiwa kurejesha uhuru wa nchi hiyo na Ecuador ikajiunga na Shirikisho la Colombia Kubwa. ***

Bendera ya Ecuador

 

Miaka 304 iliyopita katika siku kama ya leo,  Gottfried Wilhelm Leibnitz mwanahisabati na mwanafalsafa wa Kijerumani aliaga dunia mjini Hanover Ujerumani akiwa na umri wa miaka 70. Wilhelm Leibnitz alianza kuzisoma kwa bidii na juhudi elimu za falsafa na hisabati akiwa na umri wa miaka 15 alifanikiwa kupata shahada za juu kabisa katika masomo hayo. Elimu na ufahamu mkubwa na mchango aliotoa katika elimu ya hisabati pamoja na vitabu alivyoandika kuhusiana na elimu hizo, ni mambo yaliyomfanya Gottfried Wilhelm Leibnitz awekwe katika faharasa ya wasomi maarufu wa falsafa na hisabati nchini Ujerumani. ***

Gottfried Wilhelm Leibnitz

 

Katika siku kama ya leo miaka 223 iliyopita inayosadifiana na tarehe 14 Novemba mwaka 1897, alizaliwa Charles Lyell mtaalamu wa masuala ya ardhi na mwanasayansi wa Scottland. Lyell alikuwa mtu wa kwanza kuweka misingi na kanuni sahihi za kielimu katika masuala ya geolojia. Baada ya kufanya utafiti mkubwa hatimaye aliandika kitabu cha mijadala mitatu kuhusiana na misingi ya elimu ya utambuzi wa ardhi alichokipa jina la Principles of Geology. ***

Charles Lyell

 

Siku kama ya leo miaka 131 iliyopita, Jawaharlal Nehru mmoja kati ya viongozi wakubwa wa harakati ya mapambano ya India dhidi ya mkoloni Mwingereza alizaliwa huko Allahabad kaskazini mwa India. Nehru alianza mapambano dhidi ya mkoloni Mwingereza baada ya kujiunga na harakati ya kitaifa ya ukombozi wa India. Jawaharlal Nehru alitiwa mbaroni mara kadhaa na kufungwa jela kutokana na mchango na nafasi yake kubwa katika mapambano hayo. Baada ya Mahatma Ghandi kujiunga na harakati ya kitaifa ya India, wanaharakati hao wakiongoza mapambano ya kupigania uhuru ya wananchi wa India walitoa pigo kubwa kwa mkoloni Mwingereza. Hatimaye India ilipata uhuru Agosti 15 mwaka 1947. ***

Jawaharlal Nehru

 

Miaka 131 iliyopita katika siku kama ya leo, Dakta Taha Hussein mwandishi na mwanafasihi mtajika wa Misri alizaliwa. Msomi huyo mashuhuri alipofuka macho akiwa mtoto. Hata hivyo kipaji chake cha hali ya juu kilimuwezesha kuendelea na masomo na hadi kufikia mwaka 1918 alikuwa amekamilisha masomo yake ya shahada ya uzamivu katika vyuo vikuu vya Misri na Ufaransa. Dakta Taha Hussein mbali na kuwa kipofu, aliweza pia kushika nyadhifa za juu ndani na nje ya Misri na kipindi fulani alikuwa Waziri wa Utamaduni wa Misri. ***

Dakta Taha Hussein

 

Na siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, Marekani ilichukua uamuzi wa kufunga na kuzuia akaunti za fedha zote za kigeni za Iran katika benki za Marekani na benki nyingine duniani. Hatua hiyo ilichukuliwa siku chache tu baada ya kutekwa ubalozi wa Marekani hapa nchini uliokuwa pango la ujasusi. Kufungwa kwa akaunti za benki za Iran kulichukua mkondo mpana zaidi wa mashinikizo ya kiuchumi ya serikali ya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Siku chache kabla ya hatua hiyo, Iran ilikuwa imechukua uamuzi wa kusitisha kupeleka mafuta nchini Marekani kufuatia hatua za chuki za dola hilo la kibeberu dhidi ya Iran. ***