Jumatatu tarehe 16 Novemba mwaka 2020
Leo ni Jumatatu tarehe 30 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 16 Novemba mwaka 2020.
Katika siku kama ya leo miaka 75 iliyopita inayosadifiana na tarehe 16 Novemba mwaka 1945, vikosi vya jeshi la Ufaransa viliishambulia Vietnam na kuanza mapambano ya muda mrefu ya wananchi kwa ajili ya kuikomboa nchi hiyo. Baada ya karne moja ya kukoloniwa Vietnam na Ufaransa, wakati wa Vita vya Pili vya Dunia Japan iliidhibiti nchi hiyo. Japan iliondoka Vietnam baada ya kushindwa katika vita hivyo, na Vietnam ikaanza kukaliwa kwa mabavu na Ufaransa.
Siku kama ya leo miaka 74 iliyopita, yaani tarehe 16 Novemba mwaka 1946, kwa mara ya kwanza ilitengenezwa mvua bandia. Mvumbuzi wa mvua hiyo aliyekuwa mtaalamu wa masuala ya hali ya hewa wa Marekani akishirikiana na mwanakemia mmoja wa nchi hiyo, walitumia gesi ya kaboni na hewa katika kutengeneza mvua hiyo. Mvua bandia hutumiwa katika maeneo yenye ukame au yenye uhaba wa mvua.
Tarehe 26 Aban miaka 52 iliyopita aliaga dunia Ustadh Ibrahim Pourdavud, mhakiki mkubwa na mtaalamu wa masuala ya Iran akiwa na umri wa miaka 83. Alielekea katika nchi za Ujerumani na India na kufundisha katika vyuo vikuu vya nchi hizo kwa ajili ya kukamilisha utafiti wake kuhusiana na masuala ya Iran. Mwaka 1315 Hijria Shamsia mhakiki huyo mkubwa aliitwa kufundisha katika Chuo Kikuu cha Tehran na mwaka 1346 alitunikiwa tuzo ya Sayansi ya Vatican kutokana na huduma zake kubwa za masuala ya kibinadamu. Msomi huyo ameandika vitabu kadhaa vikiwemo Utamaduni wa Iran ya Kale, Anahita na Hormuz-Nameh.
Na siku kama ya leo miaka 41 iliyopita ulianzishwa tena uhusiano wa Iran na Libya. Uhusiano huo ulikatwa kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Sababu ya kukatwa uhusiano huo ni msimamo wa kiongozi wa zamani wa Libya Kanali Muammar Gaddafi aliyeitambua serikali ya Shah nchini Iran kuwa ilikuwa tegemezi kwa ubeberu wa Marekani na kwamba ilitanguliza mbele maslahi ya nchi za Magharibi na utawala ghasibu wa Israel kuliko maslahi ya nchi za Kiarabu na Wapalestina.
