Jumanne tarehe 17 Novemba 2020
Leo ni Jumanne tarehe Mosi Rabiuthani 1442 Hijria sawa na tarehe 17 Novemba mwaka 2020.
Miaka 271 iliyopita katika siku kama ya leo, sawa na tarehe 17 Novemba 1750, alizaliwa Nicolas Appert mwanasayansi wa Ufaransa. Appert aligundua njia ya kuhifadhi chakula kwa kuondoa vijidudu au Pasteurization, ambayo ilileta mabadiliko makubwa katika kuvihifadhi vyakula ili visioze. Nicolas Appert aliaga dunia mwaka 1841 kutokana na kusakamwa na umasikini.
Siku kama ya leo miaka 151 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 17 Novemba mwaka 1869, mfereji wa Suez ambao unaunganisha Bahari ya Mediterranian na Bahari Nyekundu ulifunguliwa. Mfereji huo wenye urefu wa kilometa 167 na upana wa mita 120 hadi 200 ulichimbwa chini ya usimamizi wa mhandisi wa Ufaransa, Ferdinand de Lesseps. Mfereji wa Suezi pia unahesabiwa kuwa ni mpaka kati ya bara la Asia na bara la Afrika.
Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita wiki mbili tu baada ya wanafunzi wa vyuo vikuu hapa nchini kuteka ubalozi wa Marekani mjini Tehran ambao ulitambuliwa kuwa pango la ujasusi la nchi hiyo, mateka wanawake na weusi wenye asili ya Afrika waliokamatwa katika ubalozi huo waliachiwa huru kwa amri ya hayati Imam Ruhullah Khomeini (MA). Ubalozi huo ulikuwa kituo cha ujasusi na kupanga njama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwa sababu hiyo wafanyakazi wake walishikiliwa mateka kama majasusi wa Marekani hapa nchini. Hata hivyo Imam Khomeini kwa sababu za kibinadamu na vilevile kwa kutilia maanani kwamba, wanawake na Wamarekani weusi wanadhulumiwa na kubaguliwa nchini kwao, alitoa amri waachiwe huru. Sehemu moja ya barua ya hayati Imam Khomeini kwa wanafunzi wa vyuo vikuu waliokuwa wakiwashikilia mateka wamarekani hao inasema: 'Uislamu umetunga sheria makhsusi kwa ajili ya wanawake; na watu weusi kwa miaka mingi wamekuwa chini ya mashinikizo na dhulma za Marekani na pengine wamelazimishwa kuja Iran. Kwa msingi huo wapeni tahfifu iwapo haitathibitika kwamba wamefanya ujasusi." Mwisho wa kunukuu. Kwa utaratibu huo mateka 13 wa kike na wale wenye asili ya Afrika waliachiwa huru.
Katika siku kama ya leo miaka 38 iliyopita yaani tarehe 17 Novemba mwaka 1982, Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiislamu la Iraq liliasisiwa kutokana na vyama na makundi mbalimbali yaliyokuwa yakiupinga utawala wa dikteta Saddam Hussein. Lengo la kuasisiwa baraza hilo lilikuwa ni kuwaokoa wananchi wa Iraq na dhulma pamoja na ukandamizaji wa utawala wa Chama cha Baath. Kufuatia mashambulio ya kijeshi ya Marekani nchini Iraq na kuangushwa utawala dhalimu wa Saddam, Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiislamu la Iraq, lilihamishia harakati zake za kisiasa ndani ya ardhi ya Iraq na kuwa na nafasi muhimu katika uwanja huo.

Tarehe 27 Aban miaka 35 iliyopita aliuawa shahidi Meja Jenerali Mahdi Zainuddun aliyekua Kamanda wa Divisheni ya 17 ya Ali bin Abi Twalib katika vita vya miaka 8 vya kujitetea kutakatifu. Jenerali Zainuddin ambaye alikuwa miongoni mwa makamanda wa ngazi za juu wa Iran katika mapambano ya kukabiliana na wavamizi wa Kibaath na dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein, alizaliwa katika mji wa Khorramabad katika mkoa wa Lorestan hapa nchini mwaka 1338 Hijria Shamsia. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, shahidi Zaunuddin alianza shughuli zake katika taasisi ya Jihadi ya Ujenzi na kisha akawa mwanachama rasmi katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Hadi anauwa shahidi, Meja Jenerali Mahdi Zainuddin alikuwa miongoni mwa makanda wakuu wa jeshi hilo.
Na siku kama ya leo miaka miwili iliyopita alifariki dunia Bi Marzieh Hadidchi, mmoja wa wanamapambano wakubwa wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Bi Marzieh Hadidchi alizaliwa mwaka 1318 Hijiria Shamsia huko Hamadan. Alianza kujishughulisha na masuala ya kisiasa mwaka 1346 hujria Shamsia kwa kugawa vipeperushi na mwaka 1353 aliitiwa mbaroni na maafisa wa shirika la ujasusi la Shah maarufu kwa jina la SAVAK akiwa pamoja na binti yake, Ridhwanah na kufungwa jela sambamba na kuteswa vikali. Wakati Imam Khomein (MA) alipowasili nchini Ufaransa serikali ya nchi hiyo ilitaka kumuwekea polisi mwanamke kwa ajili ya kumlinda. Imam alikataa jambo hilo. Kwa sababu hiyo Bi Marzieh Hadidchi alisafiri kwenda Ufaransa, na kutokana na mafunzo maalumu aliyopewa, akawa mlinzi wa Imam Khomeini huko Neauphle-le-Château (Nofel Loshato). Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu Bi Marzieh Hadidchi, alikuwa miongoni mwa waasisi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) na Kamanda wa jeshi hilo eneo la Hamadan, magharibi mwa nchi.