Jumatatu tarehe 23 Novemba 2020
Leo ni Jumatatu tarehe 7 Mfunguo Saba Rabiuthani 1442 Hijria sawa na Novemba 23 mwaka 2020.
Miaka 114 iliyopita katika siku kama ya leo ambayo ni sawa na tarehe 3 Azar mwaka 1285 Hijria Shamsia, gazeti la 'Majlis' lililokuwa na kurasa 8 lilianza kuchapishwa nchini Iran. Mhariri Mkuu wa gazerti hilo alikuwa Adib al Mamalik Farahani ambaye alikuwa miongoni mwa waandishi mashuhuri wa zama hizo. Mbali na gazeti hilo kuandika habari za ndani na nje ya nchi, liliakisi pia mazungumzo yote ya Majlisi ya Ushauri yaani Bunge la Iran.
Siku kama ya leo miaka 83 iliyopita Jagadish Chandra Bose, msomi mtajika wa Bangladesh alifariki dunia. Jagadish alizaliwa Novemba 30 mwaka 1858 katika moja ya maeneo ambayo ni viungwa vya mji mkuu Dhaka. Miongoni mwa elimu alizokuwa amebobea Jagadish nii fizikia, sayansi ya mimea na akiolojia. Hata hivyo umashuhuri wa Jagadish Chandra Bose unatokana na kuvumbua kwake Radio na tanuri ya miale (Microwave).
Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha suala la kuundwa nchi huru ya Palestina. Suala la Palestina lilikuwa miongoni mwa mambo ya mwanzo kabisa kujadiliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Hata hivyo maazimio mengi ya Umoja wa Mataifa yamekuwa yakiathiriwa na nchi kubwa zinazowaunga mkono Wazayuni wa Israel na utawala huo ulitumia moja ya maazimio hayo hapo tarehe 14 Mei 1948 kuanzisha dola haramu la Israel katika ardhi ya Palestina.

Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, alifariki dunia André Malraux mwandishi na msanii maarufu wa Ufaransa. Malraux alizaliwa mwaka 1901 mjini Paris na katika ujana wake alikwenda nchini China na India zilizokuwa chini ya ukoloni wa Ufaransa na kujishughulisha na mapambano dhidi ya ukoloni wa nchi yake huko Mashariki mwa Asia. Wakati akirejea katika safari yake hiyo, aliandika kitabu maarufu kwa jina la ‘Hatma ya Mwanadamu.’ Katika vita vya ndani nchini Uhispania, Malraux alishirikiana na wapigania uhuru wa nchi hiyo. André alikuwa akipinga vita na umwagaji damu na alitetea pia uhuru wa mwanadamu. ‘Vilio vya Ukimya’, ‘Ushawishi wa Magharibi’, ‘Tumaini la Mwanadamu’ na ‘Washindi’ ni miongoni mwa vitabu vilivyoandikwa na msanii huyo wa Kifaransa.
Siku kama ya leo miaka 24 iliyopita, yaani tarehe 23 Novemba mwaka 1996, ndege ya abiria ya Ethiopia iliyokuwa imetekwa nyara ilianguka katika fukwe za Bahari ya Hindi huko nchini Comoro baada ya kuishiwa na mafuta. Ndege hiyo ya Shirika la Ndege la Ethiopia aina ya Boeing 767 ilikuwa na abiria 175. Abiria 125 walipoteza maisha yao katika ajali hiyo. Ndege hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka Addis Ababa kuelekea Nairobi.
Siku kama ya leo miaka 20 ilioyopita alifariki dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Ayatullah Sayyid Mahdi Rouhani. Alizaliwa mwaka 1303 Hijria Shamsia katika familia ya kidini katika mji mtakatifu wa Qum nchini Iran na baada ya masomo ya mwanzo alielekea Karbala nchini Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Alifanya utafiti mkubwa kuhusu dini na madhehebu mbalimbali na kuwa gwiji katika taaluma hiyo. Wakati wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Ayatullah Rouhani alikuwa bega kwa bega na wananchi wa Iran katika mapambano yao dhidi ya utawala wa kifalme wa Shah wakiongozwa na hayati Imam Khomeini. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi vikiwemo vile vya "Firqatus Salafiyyah", "Buhuth Ma'a Ahlisunnah Wassalafiyyah" na "Firaq wa Madhahibu Islamiyyah".