Nov 30, 2020 23:03 UTC
  • Jumanne, Disemba Mosi, 2020

Leo ni Jumanne tarehe 15 Mfunguo Saba Rabiu Thani 1442 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe Mosi Disemba 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 195 iliyopita, muungano wa kihistoria wa nchi za Ulaya uliojulikana kama Muungano Mtakatifu ulisambaratika baada ya kujiengua utawala wa Kikaisar (Tsarist) wa Russia katika muungano huo. Baada ya kuanguka kwa utawala wa Napoleon, muungano huo uliunda Congress ya Vienna, kati ya tawala za Russia, Austria na ufalme wa Pros na serikali hizo zikaafikiana kwamba nchi zilizo chini ya utawala wa muungano huo na katika uhusiano wa kimataifa zifuate misingi ya dini ya Kikristo. ***

 

Miaka 99 iliyopita katika siku kama ya leo, Mirza Kuchak Khan Jangali, mwanaharakati na mpigania ukombozi wa Kiirani aliuawa shahidi na vibaraka wa Reza Khan, dikteta wa wakati huo wa Iran kwa ushirikiano wa madola ya Umoja wa Kisovieti na Uingereza. Mirza Kuchak Khan Jangali alijifunza masomo ya dini akiwa katika rika la ujana na kufanikiwa kukwea daraja za juu za kielimu. Baadaye alijiunga na safu ya wapigania uhuru hadi alipokamatwa na vibaraka wa Reza Khan na kuuawa kwa kukatwa kichwa kilichopelekwa kwa mfalme huyo kibaraka. ***

Mirza Kuchak Khan Jangali,

 

Siku kama ya leo miaka 47  iliyopita David Ben-Gurion mmoja wa waasisi wa utawala wa Kizayuni wa Israel na Waziri Mkuu wa kwanza wa utawala huo ghasibu aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 87. Ben-Gurion alizaliwa tarehe 16 Oktoba 1886 katika mji wa Plonsk huko Uholanzi ambayo katika zama hizo ilikuwa sehemu ya ardhi ya ufalme wa Russia. Alielekea katika ardhi za Palestina mwaka 1906 akiwa na umri wa miaka 20 na kuasisisi harakati ya Kiyahudi. Mwaka 1907 aliasisi chama cha wafanyakazi wa Kizayuni ambacho taarifa yake ilikuwa inasema: "Malengo ya chama cha wafanyakazi wa Kizayuni ni kufanya juhudi za kujitegemea kisiasa kwa ajili ya Wayahudi katika ardhi hizi tukufu." Aidha katika Vita vya Kwanza vya Dunia David Ben-Gurion alikuwa na nafasi kubwa katika kuwahamisha taratibu Mayahudi kwenda ardhi za Palestina. Katika kipindi cha Vita vya Pili vya Dunia harakati hiyo ilishika kasi chini ya uungaji mkono wa madola makubwa hususan Uingereza, kiasi kwamba mwaka 1948 Miladia sawa na tarehe 5 Mei na baada ya kupitishwa azimio na Umoja wa Mataifa la kuigawa Palestina katika pande mbili za Kiyahudi na Palestina, kulitangazwa rasmi kuanzishwa utawala haramu wa Kizayuni na wa kibaguzi wa Israel. Masaa machache baadaye, Marekani na Urusi ya zamani zikatangaza kuutambua utawala huo khabithi. ***

David Ben-Gurion

 

Na katika siku kama ya leo ya tarehe Mosi Disemba nchi mbalimbali duniani huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Ukimwi. Kuweko Siku ya kimataifa ya Ukimwi kulifikiriwa kwa mara ya kwanza mwezi Agosti mwaka 1987 na James W. Bunn na Thomas Netter, maafisa wawili wa habari wa Kitengo cha Kimataifa cha Kupambana na Ukimwi cha Shirika la Afya Duniani (WHO) huko Geneva Uswisi. Maafisa hao wawili waliwasilisha wazo hilo kwa Dakta Jonathan Mann, Mkurugenzi wa Shirika la UNAIDS na baadaye akakubali pendekezo hilo, na kuliidhinisha. Na hatimaye akaafiki siku ya kwanza ya kimataifa ya Ukimwi iadhimishwe duniani kote tarehe Mosi Disemba mwaka 1988. Kuanzia wakati huo kila mwaka siku ya kimataifa ya Ukimwi huadhimishwa duniani kote tarehe Mosi Disemba.

Siku ya Ukimwi Duniani