Jumatano, Pili Disemba, 2020
Leo ni Jumatano tarehe 16 Mfunguo Saba Rabiu Thani 1442 Hijria sawa na tarehe Pili Disemba 2020 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, Peninsula ya Korea iligawanywa katika sehemu mbili za kaskazini na kusini. Baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia na kushindwa Japan ambayo ilikuwa imedhibiti sehemu kubwa ya maeneo ya mashariki mwa Asia, viongozi waitifaki walifanya vikao katika miji ya Yalta na Potsdam wakijadili juu ya namna ya kuongoza dunia baada ya kumalizika kwa vita hivyo. Hata hivyo katika vikao hivyo kulibainika mapema kwamba Marekani na Urusi ya Zamani, zilikuwa zikiwania fungu kubwa zaidi kwa ajili ya kupenyeza siasa zao na kulidhibiti eneo tajwa. Hivyo eneo hilo na kwa mujibu wa mapendekezo ya viongozi wa nchi zilizoibuka washindi katika vita, likagawanywa sehemu mbili katika siku kama ya leo. ***
Miaka 66 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Laos ilipata uhuru kamili. Uhuru wa nchi hiyo ulipasishwa katika mkutano uliofanyika Geneva mwaka 1945 kwa kuhudhuriwa na nchi za eneo na serikali kubwa duniani. Laos ilikuwa chini ya uongozi rasmi wa Ufaransa tangu mwaka 1893. Na ilipofika mwaka 1949, Ufaransa ililazimika kuipatia Laos uhuru wa kiwango fulani katika fremu ya Umoja wa Kifaransa, kufuatia mapambano ya ukombozi yaliyoanzishwa katika eneo la India na China.***
Miaka 64 iliyopita katika siku kama ya leo, Fidel Castro alianzisha harakati ya kuikomboa nchi yake ya Cuba. Castro akiwa na lengo la kupambana na dikteta Fulgencio Batista, alianzisha mapambano ya silaha akiwa pamoja na wenzake kwa kuishambulia kambi ya kijeshi ya Moncada. Hata hivyo vikosi vya dikteta Batista viliikandamiza vibaya harakati hiyo na kumtia mbaroni Fidel Castro na kumfunga jela. Baada ya muda Castro alipelekwa uhamishoni. Hata hivyo baadaye aliunda kundi jingine la wapiganaji na kurejea Cuba alikoanzisha mapambano mapya. Hatimaye wanamapinduzi hao wa Cuba walifanikiwa kuyadhibiti maeneo muhimu ya nchi hiyo hali iliyomfanya dikteta Fulgencio Batista akimbilie katika kituo cha kijeshi cha Marekani na baadaye kutoroka nchi hiyo. ***
Siku kama ya leo miaka 49 iliyopita, Umoja wa Falme za Kiarabu ulipata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza na kila inapowadia siku kama hii ya leo nchi hiyo huiadhimisha kama siku ya taifa. Ni vyema kutaja hapa kuwa, tawala za kifalme za kusini mwa Ghuba ya Uajemi zilikuwa chini ya utawala wa Uingereza tangu mwaka 1920 Miladia. Uingereza iliasisi vituo vingi vya kijeshi katika eneo hilo, hata hivyo baada ya Vita vya Pili vya Dunia, nchi hiyo ilidhoofika na ikaliweka katika ajenda yake suala la kuondoka katika Ghuba ya Uajemi. ***
Miaka 41 iliyopita, katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilipasishwa kwa wingi wa kura za wananchi. Katiba hiyo inasisitiza juu ya kuzingatiwa thamani za Kiislamu, uadilifu wa kijamii na kuheshimiwa haki za binadamu. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, katika mwaka 1368 Hijria Shamsiya, kipengee cha ziada kiliongezwa kwenye katiba hiyo, baada ya kupasishwa na Baraza la Wataalamu linalomteuwa Kiongozi Mkuu wa Iran na kuidhinishwa pia na wananchi. Kwa mujibu wa kipengee hicho cha nyongeza, katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hivi sasa ina vipengee 14 na vifungu 177. ***
Miaka 33 iliyopita katika siku kama ya leo, kombora la kwanza la balestiki lililotengenezwa katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilifanyiwa majaribio kwa mafanikio wakati wa vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Saddam Hussein dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika kipindi hicho ambapo Iran ilikuwa chini ya vikwazo vikali vya nchi za Magharibi huku ikipigana na adui kulinda ardhi yake, awamu ya kwanza ya majaribio ya kombora hilo ilifanyika kwa mafanikio na uzalishaji wake ukaanza wakati wa vita vya Saddam Hussein dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu. ***
Na tarehe Pili Disemba kila mwaka huadhimishwa kama Siku ya Kimataifa ya Kufutwa Utumwa kote duniani. Japokuwa utumwa umefutwa katika maeneo mengi ya dunia lakini suala hilo lingali linashuhudiwa duniani katika kalibu ya utumwa mambo leo. ***