Dec 03, 2020 20:46 UTC
  • Ijumaa, 4 Disemba, 2020

Leo ni Ijumaa tarehe 18 Mfunguo Saba Rabiu Thani 1442 Hijria sawa na tarehe 4 Disemba 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 840 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alizaliwa Abul-Qasim Ja'afar Ibn Hassan Hilli, maarufu kwa jina la 'Muhaqqiq Hilli', mmoja wa wanazuoni wakubwa na faqihi wa Kiislamu, katika mji mashuhuri wa Hillah, nchini Iraq. Muhaqqiq Hilli alikuwa msomi aliyekuwa na nafasi ya juu na mtaalamu wa sheria za Kiislamu ambaye pia alibobea katika fasihi na uandishi wa mashairi. Baada ya kukamilisha masomo ya awali na kupata daraja za juu za kiroho, Muhaqqiq Hilli alitambuliwa kuwa miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa zama zake. Kitabu muhimu zaidi cha msomi huyo wa Kiislamu ni Sharaiul Islam fii Masaailil-Halal wal-Haraam’. Mwanazuoni huyo pia ameandika vitabu vya “Nafi', 'Maarij' na Tanbih”. Muhaqqiq al Hilli alifariki dunia mwaka 676 Hijria akiwa na umri wa miaka 74. ***

Abul-Qasim Ja'afar Ibn Hassan Hilli 'Muhaqqiq Hilli'

 

Miaka 121 iliyopita, kwa mara ya kwanza chanjo ya homa ya matumbo au Typhoid ilitumiwa kwa mwanadamu ili kukabiliana na maradhi hayo ambayo husababisha kuhara damu. Awali chanjo hiyo ilivumbuliwa na mtafiti mmoja wa Kifaransa na baadaye ilikamilishwa na tabibu wa Kiingereza kwa jina la Almroth Edward Wright. ***

Chanjo ya typhoid

 

Siku kama ya leo miaka 87 iliyopita alifariki dunia mjini Najaf, Iraq na akiwa na umri wa miaka 68 Ayatullah Mirza 'Ali Shirazi' mmoja wa maulama wakubwa wa ulimwengu wa Kiislamu. Ayatullah Ali Shirazi alisoma elimu ya fiqhi na elimu nyingine za Kiislamu kwa maulama wakubwa kama vile Ayatullah Fishariki Isfahani na Ayatullah Mirza Muhaqqiq Shirazi, ambapo akiwa na umri wa miaka 22 alifikia daraja ya ijtihadi. Aidha mbali na Ayatullah Mirza 'Ali Shirazi' kutabahari katika elimu ya fiqhi na usulufiqhi, pia alibobea katika elimu ya theolojia, tiba, falsafa, historia na fasihi. Aidha kwa muda fulani alikuwa marjaa taqlidi wa Waislamu.***

Ayatullah Mirza 'Ali Shirazi'

 

Miaka 68 iliyopita katika siku kama ya leo, mkutano wa pande tatu yaani Marekani, Uingereza na Ufaransa ulifanyika katika kisiwa cha Bermuda kaskazini mwa Amerika Kusini. Mbali na nchi hizo tatu kujadili uhusiano baina yao, zilichukua maamuzi muhimu na kuratibu namna ya kukabiliana na siasa za Shirikisho la Umoja wa Sovieti huko Berlin. Katika zama hizo sehemu ya magharibi ya mji wa Berlin, Ujerumani ilikuwa chini ya udhibiti wa Marekani, Uingereza na Ufaransa na sehemu ya mashariki ilikuwa chini ya udhibiti wa Umoja wa Sovieti. Kupamba moto hitilafu za namna ya kuuendesha mji huo, ndiko kulikopelekea kujengwa ukuta maarufu wa Berlin mnamo mwaka 1961. ***

Ujenzi wa ukuta wa Berlin