Dec 06, 2020 21:42 UTC
  • Jumatatu, Desemba 07, 2020

Leo ni Jumatatu tarehe 21 Mfunguo Saba Rabiuthani 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 7 Desemba mwaka 2020 Miladia

Miaka 70 iliyopita, mnamo tarehe 21 Rabiuthani 1371 Hijria, Ayatullah Muhammad Nahavandi, alimu mkubwa wa zama hizo aliaga dunia. Ayatullah Muhammad Nahavandi mwana wa mwanazuoni na alimu mchamungu Ayatullah Mirza Abdurahim Nahavandi, alizaliwa katika mji mtukufu wa Najaf, nchini Iraq. Kama alivyokuwa baba yake, Ayatullah Muhammad Nahavandi alikuwa mmoja wa maulamaa wakubwa wa karne ya 14 hijria kutokana na alivyojaaliwa kukwea na kufikia daraja za juu za elimu na akhlaqi njema. Tafsiri kubwa ya Qur’ani aliyofasiri kwa lugha za Kiarabu na Kifarsi iitwayo Nafahaatu-Rahman na kitabu cha Dhiyaaul-Abs’aar Fi Mabaahithil-Akhyaar ni miongoni mwa athari muhimu zilizoachwa na mwanazuoni huyo.

Ayatullah Muhammad Nahavandi

Miaka 131 iliyopita, yaani tarehe 7 Desemba 1889, gari la kwanza la kisasa duniani lilitengenezwa. Gari hilo lililokuwa na uwezo wa kutembea kilomita 12 kwa saa lilitengenezwa na msomi wa Kijerumani aliyejulikana kwa jina la Karl Friedrich Benz. Gari hilo lilitumia nishati ya petroli au alkoholi. Mabasi tunayoyaona katika zama hizi ni hatua ya juu na ya ukamilifu zaidi ya muundo wa gari hilo lililoundwa hapo awali na Benz. Karl Friedrich Benz alifariki dunia mwaka 1929.

Karl Friedrich Benz

Miaka 79 iliyopita katika siku inayosadifiana na ya leo, wakati Vita Vikuu vya Pili vya Dunia vilipokuwa vimepamba moto barani Ulaya, ndege mia mbili za kivita za Japan zilishambulia kituo cha jeshi la Marekani katika bandari ya Pearl Harbor. Shambulizi hilo lilifanyika wakati Japan ilikuwa katika mazungumzo na Marekani kuhusu masuala ya mashariki mwa Asia. Sambamba na mashambulizi hayo ambayo yaliteketeza manowari 19 za Marekani, jeshi la Japan lilianzisha mashambulizi makubwa pia katika nchi za kusini mwa Asia na visiwa vya Bahari ya Pasifiki ikiwemo Indonesia ya leo pamoja na visiwa vya Java na Sumatra na kuyakalia maeneo hayo. Kufuatia shambulio la anga la Japan dhidi ya bandari ya Pearl Harbor, Marekani ikatangaza vita dhidi ya Japan na Vita Vikuu vya Pili vya Dunia vikapanuka na kuenea hadi mashariki mwa Asia.

Shambulio dhidi ya bandari ya Pearl Harbor

Na miaka 39 iliyopita katika siku kama hii ya leo, yaani tarehe 7 Desemba 1981, Abdul-Wahhab Kayyali mmoja wa viongozi wa Kongresi ya Harakati ya Ukombozi ya Waarabu na mmoja wa wanamapambano wa ukombozi wa Palestina aliuawa na magaidi wa Kizayuni mjini Beirut. Kwa sababu ya masuala ya Palestina, Kayyali alijishughulisha na siasa tangu akiwa masomoni. Kwa sababu hiyo, tasnifu yake ya Uzamivu (PhD) aliyoalifu akiwa katika Chuo Kikuu cha London, Uingereza ilihusu Palestina na mapambano ya Waarabu dhidi ya ukoloni na Uzayuni. Katika harakati zake za mapambano, Abdul-Wahhab Kayyali alichapisha jarida la kwanza la Palestina alilolipa jina la “Palestina Huru” na akaanzisha pia taasisi ya uchapaji. Miongoni mwa athari za mwanafikra huyo mpambanaji ni vitabu viitwavyo ‘Historia Mpya ya Palestina’, ‘Vuguvugu la Muqawama wa Palestina’ na ‘Tafiti Kuhusu Palestina’.

Abdul-Wahhab Kayyali