Jumatano, Desemba 09, 2020
Leo ni Jumatano tarehe 23 Mfunguo Saba Rabiuthani 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 9 Desemba mwaka 2020 Miladia
Siku kama ya leo miaka 197 iliyopita, yaani tarehe 23 Rabiuthani 1245 hijria, aliaga dunia Allamah Ahmad Naraqi, Faqihi, mwanachuoni wa hadithi na malenga wa Kiirani. Mwanazuoni huyo alizaliwa mwaka 1185 Hijria na kukulia katika mji wa Kashan katikati mwa Iran ambako alipata elimu kwa baba yake, Mullah Mahdi Naraqi. Miaka kadhaa baadaye alihamia katika mji mtakatifu wa Najaf, nchini Iraq na kupata elimu ya juu kwa maulamaa wakubwa wa mji huo. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi vikiwemo vya "Miirajus Saadah" na "Asrarur Hajj."
Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, yaani tarehe 9 Desemba 1987 mapambano ya kudumu na yasiyosita ya wananchi wa Palestina dhidi ya utawala ghasibu wa Kizayuni yalianza huko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Mapambano hayo yanayojulikana zaidi kwa jina la" Intifadha ya Kwanza" yalianzishwa kufuatia kushadidi mauaji ya kigaidi, kukandamizwa Wapalestina na kuendelea kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina na utawala haramu wa Kizayuni.
Miaka 278 iliyopita, yaani tarehe 9 Desemba 1742 alizaliwa katika mji wa Stockholm, Carl Wilhelm Scheele, mwanakemia mtajika wa Sweden na mwasisi wa sayansi ya kemia ya kisasa. Japokuwa alizaliwa katika familia ya kimasikini, Scheele aliweza kuendelea na masomo kutokana na bidii na mapenzi makubwa ya kusoma aliyokuwa nayo. Mwanasayansi huyo ambaye aliishi katika zama za kuchanua kwa elimu ya kemia, baada ya juhudi za miaka mitano za kujisomea na kutafiti mambo mnamo Oktoba 1772 alifanikiwa kugundua gesi ya klorini ambayo ni moja ya mada muhimu za kemia inayotumika sana katika utengezaji vitu. Mtafiti huyo wa Sweden aligundua pia manganizi na gliserini. Carl Wilhelm Scheele alifariki dunia 1786.
Tarehe kama ya leo mwaka 1961 ardhi ya Tanganyika ambayo hii leo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilijikomboa na kupata uhuru. Tanganyika ilianza kukoloniwa na Ujerumani mwaka 1880 hadi mwaka 1919 wakati ilipoanza kukoloniwa na Uingereza na kuendelea kuwa chini ya udhibiti wa mkoloni huyo hadi ilipojipatia uhuru wake wa kujitawala katika tarehe kama ya leo. Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika na baadaye akachaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa Tanganyika huru.
Na miaka 262 iliyopita katika siku kama hii ya leo, yaani tarehe 9 Desemba 1758, vita vya Madras vilivyodumu kwa miezi 13 ambavyo vilikuwa moja kati ya vita vikali zaidi vya kikoloni kati ya Uingereza na Ufaransa vilianza huko India. Vita hivyo vilianza baada ya Ufaransa kuishambulia vikali bandari ya Madras huko kusini mwa India, ambayo ilikuwa ikidhibitiwa na Waingereza.