Dec 09, 2020 21:59 UTC
  • Alhamisi, 10 Disemba, 2020

Leo ni Alhamisii tarehe 24 Mfunguo Saba Rabiu Thani 1442 Hijria sawa na tarehe 10 Disemba 2020 Miladia

Siku kama ya leo miaka 1054 iliyopita  aliaga dunia Abu Ali Muhammad bin Mudhafar mashuhuri kwa jina la Hatami au Baghdadi aliyekuwa mtaalamuu wa lugha, mwana fasihi na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu. Alisoma elimu za lugha za fasihi kwa walimu mahiri wa zama zake na baada ya kubobea katika uwanja huo alianza kufundisha huko mjini Baghdad. Abu Ali Muhammad bin Mudhafar ameacha athari nyingi pia za vitabu katika fani mbalimbali.   

Abu Muhammad bin Mudhafar 

Miaka 605 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo yaani mwaka 837 Hijiria, katika kipindi cha watawala wa Teimur alifariki dunia malenga wa Kiirani, Sayyid Qasim al Anwar. Alikuwa miongoni mwa wasomi wakubwa na mwenyeji wa mji wa Tabriz ulioko kaskazini magharibi mwa Iran. Baada ya kuishi na kufundisha katika mji wa Harat huko kaskazini magharibi kwa Afghanistan, Sayyid Anwar alianza kupata umashuhuri, kiasi kwamba walijumuika kwake wanafunzi na wafuasi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi hiyo. Hata hivyo kutokana na dhana mbaya ya watawala wa wakati huo dhidi ya malenga huyo, Sayyid Qasim al Anwar, alilazimika kuhama kutoka Harat kwenda Samarqand nchini Pakistan ya leo. Miongoni mwa athari za malenga huyo ni pamoja na diwani ya mashairi na vitabu vya "Anisatul Arifina" na " Anisul Aashiqina."  

Sehemu aliyozikwa Sayyid Qassim al Anwar 

Siku kama hii ya leo miaka 124 iliyopita sawa na tarehe 10 Disemba mwaka 1896 miladia  alifariki dunia mwanakemia maarufu wa Sweden, Alfred Bernhard Nobel. Nobel alizaliwa mwaka 1833 na alihamia nchini Russia akiwa kijana. Alfred Nobel alifanikiwa kuvumbua mada ya dynamite au baruti baada ya kufanya utafiti mkubwa kwa miaka kadhaa katika uwanja wa sayansi ya kemia. Hata hivyo mada hiyo badala ya kutumiwa kwa matumizi ya amani, ilitumiwa kama wenzo wa kivita. Ni kwa sababu hiyo, ndipo Nobel akatoa pendekezo la kutolewa tuzo kila mwaka kwa shakhsia aliyefanya juhudi kubwa katika uwanja wa kuimarisha amani na usalama duniani. Tuzo hiyo ambayo imepewa jina la mwasisi wake yaani Nobel mwenyewe, hutolewa katika nyanja tano za fizikia, kemia, tiba, fasihi na amani ya kimataifa kwa wasomi waliofanya jitihada kubwa za kuleta amani na mafanikio ya kielimu, uvumbuzi, na mambo mengine makubwa duniani. Hata hivyo uteuzi wa washindi wa tuzo ya Nobel hususan ile ya amani duniani umeathiriwa na ushawishi wa baadhi ya madola makubwa na kuiondoa tuzo hiyo katika mkondo wa asili wa mwasisi wake.

Alfred Bernhard Nobel 

Na mkiaka 72 iliyopita katika siku kama ya leo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu na kuidhinisha haki za kimsingi na kijamii za binadamu. Azimio hilo la haki za binadamu lilitayarishwa kwa maelekezo ya Umoja wa Mataifa kupitia jopo la wawakilishi wa nchi kadhaa duniani. Azimio hilo lina utangulizi mmoja na vipengee 30 huku kipengee nambari moja cha azimio hilo kikisisitiza kuwa binadamu wote ni sawa. Licha ya kupasishwa azimio hilo, leo hii vitendo na siasa za madola ya Magharibi hasa Marekani vinakinzana wazi na azimio hilo. Leo hii pia baadhi ya madola hayo ya Magharibi yamekuwa yakilitumia suala la haki za binaadamu kama wenzo wa kuyashinikiza mataifa mengine.

Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu