Ijumaa, 11 Disemba, 2020
Leo ni Ijumaa tarehe 25 Mfunguo Saba Rabiu Thani 1442 Hijria sawa na tarehe 11 Disemba 2020 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1154 iliyopita sawa na tarehe 25 Rabiu Thani mwaka 288 Hijria , alifariki dunia Thabit bin Qurrah Swabi, mtaalamu wa hesabati, nyota na tabibu katika kipindi cha utawala wa Bani Abbas. Alizaliwa mwaka 221 Hijria mjini Harran katika eneo la Mesopotamia nchini Iraq. Thabit bin Qurrah Swabi alikuwa akizungumza lugha za Kigiriki, Kiasyria na Kiarabu. Alisafiri kwenda mjini Baghdad, Iraq kwa lengo la kusoma na kwa usimamizi wa Muhammad bin Musa aliyekuwa mtaalamu mkubwa Mwislamu wa hesabati na nyota kipindi hicho, Thabit bin Qurrah Swabi akaingia katika uwanja wa elimu hizo. Alibuni nadharia mpya katika uwanja wa hesabati. Aidha katika utaalamu wa nyota yeye ni katika watu wa kwanza kurekebisha chombo cha Ptolemaic. Thabit bin Qurrah Swabi aliandika vitabu vingi katika uwanja wa tiba, hesabati na nyota, vilivyofasiriwa kutoka lugha ya Kigiriki kwenda Kiarabu. Miongoni mwa vitabu hivyo ni pamoja na kile kiitwacho "Adh Dhakhiratu fii Ilmi al Twib" na "Kitabul Mafrudhaat."
Miaka 1074 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa mjini (Corduba, Qurtuba) Uhispania Abu Omar Yusuf bin Abdallah mashuhuri kwa jina la Abdul Birr faqih, mtaalamu wa hadithi, fasihi na mwanahistoria. Alipata masomo ya msingi kutoka kwa baba yake na walimu wengine wakubwa wa kipindi hicho. Ibnu Abdul Birr aliupa umuhimu mkubwa utafiti, ambapo kwa kipindi cha muda mfupi alikuwa mmoja wa wasomi wakubwa wa mjini Andalusia. Kufuatia kukosekana amani na usalama katika mji wa Corduba, Ibn Abdul Birr alilazimika kuhamia mji mwingine wa Daynah ambao kipindi hicho ulikuwa moja ya vituo muhimu vya elimu vya Andalusia, na huko alifanikiwa kuandika vitabu. Miongoni mwa athari za msomi huyu mashuhuri ni kitabu cha "al Istiiab" ambacho kinahusu maisha ya masahaba wa Mtukufu Mtume Muhammad (saw).
Katika siku kama ya leo miaka 210 iliyopita Alfred Louis Charles de Musset-Pathay malenga na mwandishi mwashuhuri wa Ufaransa alizaliwa katika familia ya wasomi mjini Paris, Ufaransa. Musset aliandika diwani yake ya kwanza ya mashairi kwa jina la Simulizi za Uhispania na Italia akiwa na umri wa miaka 19 na hivyo kupata umashuhuri mkubwa kutokana na mbinu yake mpya ya uandishi. Akiwa na umri wa miaka 22 aliandika tamthilia yake ya kwanza iliyoibua utata kutokana na masuala ya kiroho na kimaadili. Fikra zake huru zilimfanya awe miongoni mwa waandishi watajika katika nusu ya kwanza ya karne ya 19. Alfred de Musset aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 47 hapo mwaka 1857.
Miaka 177 iliyopita katika tareke kama ya leo yaani tarehe 11 Disemba mwaka 1843 Miladia alizaliwa daktari na mtaalamu wa vividudu maradhi wa Kijerumani aliyevumbua ugonjwa wa kifua kikuu, Robert Koch. Baada ya kukamilisha masomo katika taaluma ya tiba, Robert Koch alijishughulisha na kutibu wagonjwa katika miji mbalimbali ya Ujerumani sambamba na kufanya uhakiki kuhusu maradhi tofauti. Tarehe 24 Machi mwaka 1882 alifanikiwa kuvumbua ugonjwa wa kifua kikuu (TB). Katika safari zake nyingi barani Afrika, tabibu huyo wa Kijerumani pia alibaini kuwa ugonjwa wa malale uliokuwa ukisababisha vifo vya Waafrika wengi ulikuwa ukisababishwa na mdudu anayeitwa mbung'o.
Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) uliasisiwa baada ya kupasishwa suala hilo kwa wingi wa kura na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa. Kwa utaratibu huo, taasisi hiyo ikaanza rasmi shughuli zake chini ya Baraza la Masuala ya Kijamii la Umoja wa Mataifa. Awali Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF), ulikuwa na jukumu la kuwahudumia watoto waliojeruhiwa katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Hata hivyo baadaye asasi hiyo muhimu ikapanua zaidi shughuli zake na kuanza kuandaa mahitaji ya kimsingi maishani kama chakula, elimu na malezi kwa watoto waliokosa haki hizo za kimsingi. Makao makuu ya UNICEF yapo mjini New York, Marekani.
Na Tarehe 11 Disemba mwaka 1958 Burkina Faso ilitangazwa kuwa Jamhuri. Tangu mwanzoni mwa karne ya 19 nchi hiyo ilikuwa chini ya utawala na ukoloni wa Ufaransa. Burkina Faso ambayo hapo kabla ilikuwa ikiitwa Upper Volta, mnamo mwaka 1958 ilijitangazia utawala wa ndani wa jamhuri. Hata hivyo iliendelea kuwa sehemu ya Ufaransa. Miaka miwili baadaye yaani tarehe 5 Agosti 1960, Burkina Faso ilijipatia uhuru kamili sambamba na kukubaliwa kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Mwaka 1984 jina la nchi hiyo lilibadilishwa rasmi kutoka Upper Volta na kuitwa Burkina Faso. Nchi ya Burkina Faso ina ukubwa wa karibu kilomita mraba 274,000 na inapatikana Magharibi mwa Afrika ikipakana na nchi za Mali, Ivory Coast, Ghana, Togo, Benin na Niger.