Jumatano Disemba 16 2020
Leo ni Jumatano tarehe Mosi Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1442 Hijria mwafaka na tarehe 16 Desemba 2020 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 231 iliyopita yaani tarehe Mosi Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1211, alifariki dunia mshairi mkubwa wa Kiislamu Sheikh Kadhim Tamimi Baghdadi, maarufu kwa jina la Uzri akiwa na umri wa miaka 80. Alikuwa msomi na mwanafasihi mkubwa na ameacha diwani ya mashairi. Miongoni mwa mashairi ya malenga huyu maarufu wa Kiislamu ni shairi maarufu la "Al Uzriya" ambalo linamsifu Mtukufu Mtume Muhammad (saw) na kizazi chake kitukufu na kubainisha misingi ya dini ya Uislamu. Shairi hilo lina zaidi ya beti 1000.

Miaka 133 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, Ayatullah Mirza Muhammad Hassan Husseini Shirazi alitoa fatuwa maarufu ya kuharamisha tumbaku ili kuzuia uporaji uliokuwa ukifanywa na wakoloni wa Kiingereza katika nchi za Kiislamu. Fatuwa hiyo ilitolewa baada ya Mfalme Nasiruddin Shah wa Iran kutia saini mkataba wa kuipa kampuni moja ya utawala wa kikoloni wa Uingereza mamlaka ya kuuza na kununua tumbaku ya Iran kwa kipindi cha miaka 50. Jina la Mirza Shirazi ni mashuhuri mno kutokana na fatuwa hiyo ya kuharamisha tumbaku. Fatua yake hiyo ya kuharamisha tumbaku na matumizi ya sigara, bidhaa ambayo ilikuwa imehodhiwa na Uingereza, ilitoa pigo kubwa kwa ukoloni wa Uingereza nchini Iran. Vilevile fatua hiyo ilitambuliwa kuwa mapambano ya moja kwa moja dhidi ya utawala wa Shah na ukoloni wa Uingreza nchini Iran na iliandaa uwanja wa mapambano ya baadaye ya wananchi wa Iran dhidi ya dhulma, ukandamizaji na ukoloni wa wageni.
Siku kama hii ya leo miaka 22 iliyopita Mahakama ya Rufaa ya Paris ilimhukumu kifungo na kumtoza faini mwanafalsafa na msomi mashuhuri wa nchi hiyo, Roger Garaudy, kwa kosa eti la kukana jinai dhidi ya binadamu katika kitabu chake cha 'The Founding Myths of Israeli Politics'. Katika kitabu hicho msomi huyo Mfaransa alithibitisha kisayansi na kwa hoja madhubuti kwamba Wazayuni walishirikiana na Manazi katika Vita vya Pili vya Dunia. Vilevile amethibitisha kwa hoja na ushahidi kwamba, kwa shabaha ya kutaka kupata uungaji mkono wa kuunda dola bandia la Israel katika ardhi ya Palestina, Wazayuni walikuza na kutia chumvi kupita kiasi jinai zilizofanywa na Adolph Hitler dhidi ya Mayahudi. Katika kitabu cha 'The Founding Myths of Israeli Politics' Profesa Garaudy anasema, idadi ya Mayahudi milioni 6 inayotajwa na Wazayuni kuwa iliuawa na Wajerumani wa zama za Hitler imetiwa chumvi kupita kiasi kwani jamii ya Wayahudi katika kipindi hicho haikuwa kubwa kiasi hicho. Msomi huyo alikamatwa na kuhukumiwa kifungo nchini Ufaransa kutokana na maoni yake, suala ambalo limethibitisha urongo wa madai ya kuwepo demokrasia na uhuru wa maoni nchini Ufaransa.
Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita mwili wa Mhandisi Muhammad Jawad Tundguyan, waziri wa mafuta wa wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulirejeshwa nchini Iran kutoka Iraq baada ya kupita miaka 11. Waziri Tundguyan na maafisa wengine kadhaa wa wizara hiyo walitekwa nyara na wanajeshi wavamizi wa Iraq wakati walipokuwa katika ziara ya kutembelea visima vya mafuta vya kusini mwa Iran. Waziri huyo na wenzake walitekwa nyara mwezi mmoja baada ya Iraq kuvamia ardhi ya Iran. Utawala wa Saddam wakati huo uliendelea kukanusha kutekwa nyara Mhandisi Tundguyan kwa muda fulani, lakini hatimaye ulikiri kumteka nyara waziri huyo wa zamani wa mafuta wa Iran. Uchunguzi wa kidaktari na ushahidi uliotolewa na watu waliokuwa karibu na Waziri Muhammad Jawad Tundguyan ulithibitisha kwamba waziri huyo wa zamani wa mafuta wa Iran alikufa shahidi kutokana na kuteswa vikali na askari jeshi wa utawala wa Baath wa Iraq.
Na siku kama ya leo miaka 29 iliyopita Kazakhstan ilijitangazia uhuru baada ya kudhihiri dalili za kusambaratika Urusi ya zamani. Wakazaki ambao wanaunda jamii kubwa zaidi nchini humo na ambao ni kutoka makabila ya Waturki na Wamongoli, katika karne ya 17 Miladia, waligawanyika katika sehemu tatu za tawala kubwa za kisultani. Mwanzoni mwa karne ya 18 taratibu waliwekwa chini ya udhibiti wa Warusi na wakati huo khususan katika karne ya 19 Miladia, Wakazaki hao wakiwa pamoja na watu wa maeneo mengine ya Asia ya kati walijiunga na dini ya Kiislamu.