Dec 18, 2020 23:26 UTC
  • Jumamosi, 19 Desemba, 2020

Leo ni Jumamosi tarehe 4 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1442 Hijria mwafaka na tarehe 19 Desemba 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 887 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria alizaliwa nchini Iraq Ibn Athir Jazari mwanahistoria na mwanafasihi mahiri wa Kiislamu. Ibn Athir alisoma mjini Mosul, Sham na Baghdad kwa maulama watajika kama Khatib Tusi. Alikuwa na mapenzi makubwa na kutwalii na kufanya uhakiki kuhusiana na historia na ni kutokana na sababu hiyo ndio maana athari zake nyingi zilizoko hii leo zinahusiana na historia. Kitabu mashuhuri zaidi cha Ibn Athir ni kile kinachojulikana kwa jina la "al-Kamil Fi Taarikh." Msomi na mwanahistoria huyo wa Kiislamu alifariki dunia mwaka 630 Hijria katika mji wa Mosul huko Iraq. ***

Ibn Athir Jazari

 

Katika siku kama ya leo miaka 233 iliyopita mwafaka na tarehe 19 Disemba 1787, nchi ya Kiafrika ya Sierra Leone iliunganishwa na Uingereza, baada ya kupita miaka 327 tangu ardhi ya nchi hiyo igunduliwe na wazungu. Sierra Leone iligunduliwa na mtalii wa Uhispania na kukoloniwa. Katika miaka ya kukoloniwa kwake na Uhispania, maelfu ya wanaume na wanawake wa Sierra Leone walichukuliwa watumwa na kwenda kuuzwa katika masoko ya Ulaya. Mwenendo huo uliendelea pia baada ya Waingereza kuishinda Uhispania na kuanza ukoloni wa Uingereza nchini humo. Mwaka 1961 Sierra Leone ilianza kujitawala na kuwa na utawala unaosimamiwa na jeshi na mwaka 1971 ikawa na utawala wa Jamhuri. ***

Bendera ya Sierra Leone

 

Miaka 114 iliyopita alizaliwa kiongozi wa Urusi ya zamani, katika familia maskini nchini Ukraine. Mwaka 1931, Brezhnev alijiunga na kuwa mwanachama wa chama hicho cha Kikomonisti. Brezhnev alitwaa uwaziri mkuu Russia na uongozi wa Chama cha Kikomonisti cha Urusi ya zamani mwaka 1964 wakati Nikita Khrushchev alipokuwa safarini nje ya nchi. Mashambulizi dhidi ya Czechoslovakia na kukaliwa kijeshi Afghanistan yalifanyika katika zama zake.***

Leonid Brezhnev

 

Siku kama ya leo miaka 100 iliyopita aliaga dunia alimu na mwanazuoni Mulla Fat'hullah Gharawi Isfahani aliyejulikana kwa jina la Sheikhu Shari'a Isfahani. Alizaliwa mwaka 1228 Hijria Shamsia huko Isfahan katikati mwa Iran na kupata elimu ya dini katika mji huo. Baadaye kidogo alielekea katika mji mtakatifu wa Mash'had na mwaka 1257 alikwenda Najaf nchini Iraq kwa ajili ya kutafuta elimu na kusoma kwa walimu wakubwa na mashuhuri wa zama hizo. Ameandika vitabu kadhaa katika masuala ya sheria na fiqhi ya Kiislamu. Sheikhu Shari'a pia alikuwa mstari wa mbele katika mapambano ya kiutamaduni, kisiasa na kijeshi dhidi ya wakoloni wa Kiingereza na aliongoza harakati za wananchi wa Iraq dhidi ya wakoloni hao.***

Mulla Fat'hullah Gharawi Isfahani

 

Na siku kama ya leo miaka 47  iliyopita, inayosadifiana na 19 Disemba 1972, kiongozi wa wakati huo wa Uganda Jenerali Idi Amin Dada aliwapatia wafanyakazi wa Kiingereza waliokuwa wakifanya kazi nchini humo makataa ya siku 12 wakubali kupunguziwa mishahara yao kwa asilimia 40 au waondoke nchini humo. Zoezi hilo liliwajumuisha karibu wafanyakazi 780 wa Kiingereza waliokuwa wakifanya kazi kwenye mashirika mbalimbali nchini Uganda. ***

Jenerali Idi Amin Dada