Ijumaa, Aprili 23, 2021
Leo ni Ijumaa tarehe 10 Ramadhani 1442 Hijria sawa na 23 Aprili mwaka 2021 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1445 iliyopita yaani tarehe 10 Ramadhani miaka mitatu kabla ya Hijra, alifariki dunia Bi Khadija binti Khuwailid mke wa Mtume Muhammad SAW katika mji wa Makka. Bi Khadija ambaye alikuwa mmoja wa wanawake mashuhuri na tajiri wa Makka aliolewa na Mtume Mtukufu miaka 15 kabla ya kubaathiwa mtukufu huyo. Bi Khadija alikuwa mtu wa kwanza kuamini ujumbe wa Mtume Muhammad SAW na alitumia uwezo na utajiri wake katika kuisaidia dini ya Kiislamu. Kuweko Bi Khadija SA pamoja na Mtume wa Uislamu kulikuwa na umuhimu mkubwa kiasi kwamba Mtume SAW alikitaja kifo cha mkewe huyo kipenzi kuwa ni msiba mkubwa. Mtume aliutaja mwaka aliofariki dunia Bi Khadija na msaidizi wake mwingine mkubwa yaani Abu Talib kuwa mwaka wa majonzi na huzuni. Hii ni kwa sababu Abu Talib ami yake Mtume SAW pia alifariki dunia mwaka huo huo.

Siku kama ya leo ya tarehe 3 mwezi ordibehesht katika kalenda ya mwaka wa Kiirani ni siku ya kumuenzi Sheikh Bahauddin Muhammad Amili maarufu kwa jina la Sheikh Bahai, mwanazoni mkubwa wa taaluma mbalimbali za Kiislamu. Sheikh Bahai ambaye alikuwa ametabahari katika elimu nyingi kama fiqhi, nujumu, hadithi, tafsiri ya Qur'ani na hesabati alifariki dunia katika mji wa Isfahan nchini Iran. Alizaliwa mwaka 953 Hijria eneo la Baalabak huko Lebanon katika familia ya Kiirani. Baba yake alikuwa miongoni mwa mashekhe wakubwa wa zama hizo. Sheikh Bahai ameandika vitabu zaidi ya mia moja ikiwa ni pamoja na Tashrihul Aflak, Kashkul na Hablul Matin.
Katika siku kama ya leo miaka 405 iliyopita, alizaliwa William Shakespeare, mshairi na mwandishi mashuhuri wa michezo ya kuigiza wa Uingereza. Shakespeare alianza kazi zake za usanii sambamba na kushiriki katika michezo ya kuigiza. Alipata umashuhuri mkubwa katika fani hiyo. Kazi zake za kisanii zilikuwa mchanganyiko wa sanaa iliyoakisi majonzi na vichekesho.
Miaka 163 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa mwanafizikia Max Plank wa Ujerumani ambaye pia alikuwa mtaalamu wa hisabati aliyebuni nadharia ya kwanta katika elimu ya fizikia. Mwaka 1918 Max Plank alitunukiwa tuzo ya fizikia ya Nobel kwa kugundua nadharia ya kwanta. Plank ambaye alikuwa mpinzani mkubwa wa dikteta wa zamani wa Ujerumani Adolph Hitler, alifanya utafiti mkubwa katika nyanja za mwendojoto (sayansi ya uhusiano wa joto na kazi za mitambo), fizikia nadharia, joto, mnururisho na nuru na kuandika vitabu kadhaa katika medani hiyo.
Tarehe 3 Ordibehest miaka 37 iliyopita utawala wa Kibaath wa Iraq ulianzisha vita na mashambulizi dhidi ya meli za kubeba mafuta za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika maji ya Ghuba ya Uajemi. Baada ya kupita karibu miaka minne tangu Saddam Hussein aivamie ardhi ya Iran, Iraq ikisaidiwa na madola makubwa, ilichukua hatua ya kuzidisha mashinikizo dhidi ya Iran kwa kutumia wenzo wa kuzuia uuzaji nje mafuta ya Iran na badala yake wazidishe uzalisha wa mafuta katika nchi za Kiarabu ili kufidia nakisi ya mafuta ya Iran katika masoko ya kimataifa. Kwa misingi huo walianza kushambulia meli za kubeba mafuta za Iran na bandari za kupakia bidhaa hiyo hapa nchini. Siku hiyo Iraq ikisaidiwa na Marekani na nchi nyingine za Magharibi, ilitumia ndege za kivita za Super Standard za Ufaransa kushambulia kisiwa cha Khark na meli zilizokuwa zimebeba mafuta za Iran.
Katika siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 23 Aprili 1992, alifariki dunia Satyajit Ray mwandishi na mtengeneza filamu mashuhuri wa India. Satyajit Ray alizaliwa mwaka 1921, na filamu zake za kijamii ziligusa zaidi hisia za jamii ya wananchi wa nchi hiyo, na kupelekea kupendwa zaidi na wananchi wa India.
Tarehe 23 Aprili miaka 26 iliyopita Shirika la Sayansi, Elimu na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) liliitangaza siku hii ya kuwa Siku ya Kimataifa ya Kitabu na Haki za Mwandishi. Lengo la kutangazwa siku hiyo ni kuonesha umuhimu wa kitabu na haki za waandishi wa vitabu, kuhamasisha watu kusoma vitabu, kuwapongeza watu wanaoandika vitabu kwa ajili ya kukuza na kustawisha utamaduni wa jamii ya mwanadamu na vilevile kuunga mkono na kusaidia ustawi wa sekta ya kusambaza vitabu. Utamaduni wa kusoma vitabu umeshamiri zaidi katika dunia ya sasa hususan miongoni mwa tabaka la vijana kutokana na kusambaa zaidi vitabu vya elektroniki kupitia mitandao ya intaneti.
