Apr 26, 2021 23:49 UTC
  • Jumanne tarehe 27 mwezi Aprili mwaka 2021

Leo ni Jumanne tarehe 14 Ramadhani 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 27 Aprili mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 1375 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 14 Ramadhani mwaka 67 Hijria, aliuawa shahidi Mukhtar bin Abu Ubaida al Thaqafi, kiongozi wa harakati ya kulipiza kisasi cha damu ya Imam Hussein bin Ali AS, mjukuu wa Mtume Mtukufu Muhammad SAW. Imam Hussein AS akiwa pamoja na wafuasi wake na watu wa familia yake, aliuawa shahidi na wafuasi wa Yazid bin Muawiya, akilinda dini tukufu ya Kiislamu. Mukhtar alianzisha harakati zake katika mji wa Kufa. Kabla yake, kulijitokeza kundi la 'Tawwabiin' ambalo lilianzisha mapambano dhidi ya utawala wa Bani Umayya, kwa lengo la kulipiza kisasi cha damu ya Imam Hussein AS. Mukhtar al Thaqafi alitawala Kufa kwa muda wa mwaka mmoja hivi, na hatimaye alishindwa na jeshi la Mus'ab bin Zubair na kuuawa shahidi katika siku kama hii ya leo.

Kaburi la Mukhtar bin Abu Ubaida al Thaqafi

Siku kama hii ya leo miaka 500 iliyopita, Ferdinand Magellan, baharia wa Kireno aliuawa na wenyeji wa Ufilipino kutokana na kuingilia mambo yao. Alizaliwa mwaka 1470 na kuanzia mwaka 1519 Miladia baharia huyo alianza safari yake kubwa ya baharini akiwa na meli tano. Ferdinand Magellan aligundua lango bahari huko kusini mwa bara la Amerika baada ya kuwasili katika pwani ya Amerika ya Latini. Lango bahari hilo limepewa jina la baharia huyo wa Kireno yaani Lango Bahari la Magellan.

Ferdinand Magellan

Miaka 61 iliyopita katika siku inayofanana na hii ya leo, nchi ya Togo inayopatikana huko katika pwani ya magharibi mwa Afrika ilipata uhuru. Wareno walikuwa watu wa kwanza kuikoloni Togo na nchi hiyo ilijulikana sana kwa jina la "Pwani ya Watumwa"  kwa kuwa nchi za Ulaya  zilikuwa zikiitumia nchi  hiyo kama kituo cha kusafirishia watumwa kuelekea Ulaya. Togo inapakana na nchi za Ghana na Benin na mji mkuu wake ni Lome.

Bendera ya Togo

Miaka 60 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Sierra Leone moja ya makoloni makongwe ya Uingereza magharibi mwa Afrika ilijipatia uhuru. Sierra Leone ilianza kukoloniwa na Ureno tangu karne ya 15 na nchi hiyo ilikuwa mojawapo ya vituo muhimu vya kuuzia watumwa waliokuwa wakipelekwa Ulaya. Uingereza ilianza kuikoloni Sierra Leone mwishoni mwa karne ya 18 hadi mwaka 1961 wakati nchi hiyo ilipopata uhuru. Baada ya uhuru, nchi hiyo ilikumbwa na mapinduzi na uasi mwingi. Kijiografia  Sierra Leon iko Magharibi mwa Afrika ikiwa na ukubwa wa kilomita mraba 71,000 na inapakana na Guinea na Liberia. 

Bendera ya Sierra Leon

Siku kama ya leo miaka 48 iliyopita alifariki dunia Kwame Nkrumah, mwanasiasa mashuhuri wa Kiafrika na mpigania uhuru wa Ghana. Mkrumah alizaliwa mwaka 1909 na baada ya kupata shahada ya uzamivu nchini Marekani alianza kujishughulisha na masuala ya kisiasa. Baadaye Kwame Nkrumah aliasisi chama cha Kitaifa cha Watu wa Ghana na kuanza mapambano dhidi ya wakoloni wa Kiingereza. Mwaka 1951 alishiriki katika uchaguzi wa Bunge na kuwa Waziri Mkuu. Baada ya Ghana kupata uhuru mwaka 1960 Kwame Nkrumah alikuwa Rais wa nchi hiyo lakini Februari 24 mwaka 1966 aliondolewa madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi na wafuasi wa nchi za Magharibi akiwa safarini nchini Uchina. Baadaye alielekea Guinea ambako aliishi hadi kufariki dunia. Kwame Nkrumah anatambuliwa kuwa miongoni mwa wanamapambano mashuhuri wa Afrika waliofanya jitihada kubwa katika kupata uhuru na kujitawala nchi za bara hilo.

Kwame Nkrumah

Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, Jenerali Abdul Qadir alifanya mapinduzi nchini Afghanistan na baada ya kumuua Daud Khan Rais wa wakati huo wa nchi hiyo, alimuweka madarakani Noor Muhammad Taraki kiongozi wa Chama cha Kidemokrasia cha Khalq. Baada ya muda Hafizullah Amin alifanya mapinduzi na kumuondoa madarakani Muhammad Taraki na yeye kushika hatamu za uongozi wa nchi hiyo. Hata hivyo mlolongo huo wa mapinduzi uliendelea kwani Hafidhullah Amin alipinduliwa na kisha kuuawa na Babrak Karmal. Katika kipindi cha uongozi wa Babrak, ndipo Afghanistan ilipovamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Shirikisho la Umoja wa Sovieti.

Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita Mzayuni mmoja aliyekuwa na misimamo ya kufurutu ada aliwashambulia na kuwamiminia risasi Waislamu waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala katika Msikiti wa Haram ya Nabii Ibrahim mjini al Khalil, Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kuua shahidi 29 miongoni mwao. Mauaji hayo yalitokea wakati Waislamu hao walipokuwa katika ibada ya funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Waislamu wengine wengi walijeruhiwa katika shambulizi hilo la kikatili. Mauaji hayo ambayo yalidhihirisha tena uhasama na chuki za Wazayuni wa Israel dhidi ya Waislamu, yalilaaniwa na Waislamu kote duniani. Ukatili huo ulizusha wimbi kubwa la machafuko katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina ambapo wananchi walizidisha mapambano dhidi ya maghasibu wa Tel Aviv. Israel ilimshika kwa muda na kumuachia huru mhalifu huyo katili kwa kisingizio kwamba alikuwa punguani!

Jinai za Wazayuni huko Palestina