Jumatano, Mei 5, 2021
Leo ni Jumatano tarehe 22 Ramadhani 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 5 Mei mwaka 2021 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1169 iliyopita, alifariki dunia Ibn Majah, mpokezi wa hadithi na mfasiri mashuhuri wa Qur’ani wa Kiislamu. Ibn Majah alizaliwa mwaka 209 Hijria katika mji wa Qazvin nchini Iran. Alielekea katika nchi mbalimbali za Kiislamu ili kujifunza elimu ya hadithi. Aliandika kitabu chake mashuhuri cha "Sunan Ibn Majah" baada ya kuhitimu masomo katika elimu ya hadithi, kitabu ambacho ni moja kati ya vitabu sita muhimu zaidi vya hadithi kwa Waislamu wa madhehebu ya Suni.

Siku kama ya leo miaka 203 iliyopita, alizaliwa Karl Heinrich Marx mwanafalsafa wa Kijerumani na mwasisi wa nadharia ya Umaksi. Karl Marx awali alianza kusomea taaluma ya sheria na baadaye historia na falsafa. Mwanafalsafa huyo wa Kijerumani kwa muda fulani alikuwa mkuu wa jarida moja na mwaka 1848 alishirikiana na mwanafalsafa mwenzake wa Kijerumani na kubainisha imani, maoni na mitazamo yake katika kitabu alichokipa jina la "Manifesto ya Ukomonisti." Miaka miwili baadaye Marx alibaidishwa kutokana na kujishughulisha na harakati za kisiasa na hadi mwishoni mwa maisha yake makazi yake yalikuwa nchini Uingereza.
Siku kama ya leo miaka 200 iliyopita, alifariki dunia Napoleon Bonaparte mfalme aliyekuwa na nguvu wa Ufaransa, akiwa uhamishoni. Napoleon alizaliwa mwaka 1769 na kuchukua madaraka makubwa ya uongozi baada ya mapinduzi ya Ufaransa mwaka 1789, ambapo aliifanya nchi hiyo ishinde vita na nchi nyingi za Ulaya. Baada ya kuwa mfalme wa Ufaransa, Napeleon alibadilika na kuwa mtawala aliyependa kujitanua na kuzivamia nchi nyingine katika maeneo mbalimbali duniani. Kwa ajili hiyo katika kipindi cha utawala wake alipigana vita kadhaa na nchi nyingine na kukalia kwa mabavu maeneo mengi ya bara Ulaya.
Siku kama ya leo miaka 156 iliyopita alifariki dunia, Haj Abdul-Hussein Tehrani, maarufu kwa jina la Sheikhul-Iraaqiyyin, mmoja wa maulama wakubwa wa Iran. Haj Abdul-Hussein Tehrani alitabahari katika elimu ya fiqhi, huku akiwa mcha-Mungu sana. Kadhalika alitambulika kwa kuwa na kumbukumbu ya hali ya juu katika msomo ya dini. Mbali na fiqhi, pia alikuwa alimu katika elimu ya hadithi na tafsiri ya Qur'an Tukufu. Alifanya juhudi kubwa katika kuasisi maktaba na kukusanya turathi za Kiislamu ambapo baada ya kufariki kwake dunia kuliasisiwa maktaba kubwa kwa ajili ya wanafunzi wa Kiislamu.
Miaka 77 iliyopita katika siku kama hii ya leo hayati Imam Ruhullah Khomeini akiwa na umri wa miaka 42, alitoa taarifa yake ya kwanza ya kisiasa akiwataka wananchi kusimama na kuanza harakati kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Katika taarifa hiyo Imam Khomeini alichunguza hali ya miaka ya nyuma, ya kipindi hicho na mustakbali wa wananchi wa Iran na Waislamu kwa ujumla na kusema: Kuanza harakati na mapambano kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ndiyo njia pekee ya kurekebisha hali ya dunia. Alisema suala hilo ndiyo falsafa ya kutumwa Manabii wote wa Mwenyezi Mungu. Imam pia alieleza sababu za hali mbaya ya Waislamu na wananchi wa Iran na kukumbusha majukumu mazito ya wanazuoni wa dini na athari mbaya za tabaka hilo kughafilika na masuala ya kisiasa. Katika taarifa hiyo Imam Khomeini alipiga kengele ya hatari na kuwaamsha Waislamu husuan wanafunzi wa vyuo vya kidini kuhusu umuhimu wa kusimama na kuanza mapambano ya kurekebisha Umma.
Miaka 40 iliyopita katika siku kama ya leo alifariki dunia Bobby Sands mwanamapambano maarufu wa Ireland baada ya kukaa katika jela ya Uingereza kwa wiki kadhaa na kugoma kula chakula kwa muda wa siku 66 katika kupigania uhuru wa Ireland ya Kaskazini. Serikali ya kikoloni ya Uingereza ilikabiliwa na wimbi kubwa la malalamiko kutoka ndani na nje ya nchi hiyo kufuatia kifo cha Bobby Sands na wanaharakati wenzake wa Ireland ambao waligoma kula chakula wakiwa katika jela za nchi hiyo.
Na tarehe 5 Mei imetangazwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirikisho la Kimataifa la Wakunga kuwa ni ya Siku ya Kimataifa ya Wakunga. Siku hiyo ilipendekezwa kwa mara ya kwanza kuwa Siku ya Kimataifa ya Wakunga mwaka 1980 na kutangazwa rasmi mwaka 1992. Lengo la kuainishwa siku hii ni kuwaenzi wakunga na kazi ya ukunga, kuzidisha uelewa na kubadilishana maarifa na taarifa zinazohusiana na afya ya akina mama na watoto wachanga na vilevile kuonyesha umuhimu wa kazi za wakunga.