Jumatano, Mei 19, 2021
Leo ni Jumatano tarehe 7 Mfunguo Mosi Shawwal 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 19 Mei 2021 Milaadia.
Siku kama hii ya leo miaka 1439 iliyopita kulipiganwa vita vya Uhud kando kando ya mlima wenye jina hilo kaskazini mwa mji wa Madina, kati ya Waislamu na Washirikina. Baada ya washirikina wa Kiquraishi kushindwa vibaya na Waislamu katika vita vya Badr walianzisha vita hivi vya Uhud kwa kuandaa jeshi la watu 3,000 waliokuwa na zana kamili kwa ajili ya vita hivyo, huku wapiganaji wa Kiislamu wakiwa 700 tu. Kabla ya kuanza kwa vita hivyo, Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w) aliwashauri masahaba zake juu ya namna atakavyopambana na Maquraishi na iliamuliwa kuwa vita hivyo vipiganwe nje ya mji wa Madina. Mwanzoni mwa vita hivyo, Waislamu walionekana kushinda, hata hivyo kufuatia kughafilika na baadhi yao kuasi amri ya Mtume (saw) aliyewataka kubakia mlimani, Waislamu hao walishuka mlimani kwa tamaa za kupata ngawira, hali iliyowafanya washirikina wawashambulie Waislamu na kudhoofika nguvu na uwezo wao. Waislamu 70 waliuawa shahidi katika vita hivyo akiwemo Hamza ami yake Mtume (s.a.w). Hata hivyo washirikina hawakuweza kupata ushindi wa moja kwa moja na hivyo wakalazimika kurejea Makka.
Siku kama ya leo miaka Miaka 500 iliyopita, majeshi ya utawala wa kifalme wa Othmania yaliuteka mji muhimu wa Belgrade, uliokuwa mji mkuu wa Yugoslavia ya zamani. Mwishoni mwa karne ya 14 Miladia Utawala wa Othmania ulianza kusonga mbele katika eneo la Balkan na kuweza kulitawala karibu eneo lote hilo. Miaka 20 baadaye yaani mwaka 1541 utawala huo ulifanikiwa pia kuyadhibiti maeneo ya Hungary.
Katika siku kama ya leo miaka 259 iliyopita alizaliwa Johan Gottlieb Fichte mwanafalsafa mashuhuri wa Kijerumani. Alizaliwa na kukulia katika familia maskini na iliyokuwa ikikabiliwa na ufakiri mkubwa. Mwanafalsafa huyo wa Kijerumani alikuwa mfuasi wa nadharia ya udhanifu au kwa kitaalamu â'Idealism''. Johan Gottlieb Fichte alifahamiana na Conte mwanafalsafa mwingine wa Kijerumani na kumkabidhi moja kati ya athari zake muhimu katika falsafa. Kiujumla Fichte alikuwa ameathirika na fikra pamoja na mitazamo ya Conte. Johan Gottlieb Fichte aliaga dunia mwaka 1814. Mwanafalsafa huyo ameandika vitabu kadhaa kama The Vocation of Man" na "Science of knowledge".
Siku kama ya leo miaka 96 iliyopita, alizaliwa Malcolm X, kiongozi wa harakati za kupigania uhuru Wamarekani wenye asili ya Afrika. Malcolm X alizaliwa katika familia masikini na akiwa na umri wa miaka minne, alishuhudia nyumba ya wazazi wake ikishambuliwa na kuteketezwa kwa moto na kundi la kibaguzi la Ku Klux Klan. Baadaye alijiunga na shule, hata hivyo hakuweza kukamilisha masomo yake kutokana na umasikini na aliacha shule akiwa na umri wa miaka 15; hivyo akalazimika kufanya kazi katika mgahawa mmoja ambapo alijikuta akijiunga na magenge ya utumiaji wa madawa ya kulevya na unyang’anyi. Kufuatia hali hiyo alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela akiwa na umri wa miaka 21. Akiwa jela alifahamiana na wafungwa wengi wenye asili ya Kiafrika waliotokana na familia za Kiislamu kama ambavyo pia alikuwa na mahusiano na Elijah Muhammad, kiongozi wa harakati ya siri ya Wamarekani weusi. Mahusiano na kiongozi huyo yaliendelea hata baada ya Malcolm X kutoka jela. Baada ya hapo alianza kusoma na kufanya utafiti mkubwa kuhusiana na dini ya Uislamu ambapo kwa msaada wa Waislamu alifanikiwa kujenga misikiti miwili katika mji wa Detroit, Philadelphia nchini Marekani. Malcom X alipigwa risasi na kuuawa tarehe 21 Februari mwaka 1965 katika mji wa New York baada ya kushadidei harakati zake za kupigania haki za Waislamu na Wamarekani weusi. Mauaji ya mwanaharakati huyo Mwislamu wa Marekani, kama yalivyo mauaji mengi ya kisiasa ya Marekani, bado yangali yanagubikwa na wingu kubwa. Hata hivyo ushahidi unaonyesha kuwa Malcom X aliuawa na maajenti wa shirika la usalama wa ndani ya Marekani FBI likishirikana na Shirika la Ujasusi la nchi hiyo CIA.
Siku kama ya leo miaka 86 iliyopita, Thomas Edward Lawrence mwanasiasa na afisa wa ujasusi wa Uingereza alifariki dunia katika ajali ya gari. Lawrence alizaliwa mwaka 1888. Katika kipindi cha miaka ya kati ya 1910 na 1914, mwanasiasa huyo wa Uingereza alifanya kazi katika nchi za Iraq, Syria na Palestina akiwa mjumbe wa kamati ya masuala ya akiolojia (elimu mambo ya kale). Aidha alikuwa mfanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza na mwaka 1916 aliteuliwa kuwa mkuu wa Idara ya Ujasusi ya Jeshi la Uingereza nchini Misri. Thomas Edward Lawrence alikuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa njama ya Uingereza na Ufaransa ya kuzigawa nchi za Kiarabu na utawala wa Othmania (Ottoman Empire) na alichangia pakubwa kuwaweka madarakani wafalme Faisal huko Syria, Abdallah nchini Jordan na Mfalme Abdulaziz huko Saudi Arabia. Kwa sababu hiyo alijulikana kwa jina la Lawrence wa Uarabuni ( Lawrence of Arabia).
Na siku kama ya leo miaka 85 iliyopita yaani tarehe 19 Mei mwaka 1936, chombo cha rada kilitengenezwa na Sir Robert Watson-Watt mtaalamu na mvumbuzi wa Kiingereza. Chombo hicho ambacho ni wenzo muhimu utumiwao na marubani kuonyesha vitu kwenye skrini au kugundulia na kutambulia mambo katika operesheni za kijeshi na zisizokuwa za kijeshi, kwa mara ya kwanza kiliwekwa katika viwanja vya ndege nchini Uingereza. Wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, rada ilihesabiwa kuwa wenzo muhimu wa kutoa tahadhari. Hii leo chombo cha rada kinatumiwa katika nyanja mbali hasa katika safari za ndege, opresheni za kijeshi na kadhalika.
Siku kama hii ya leo miaka 49 iliyopita inayosadifiana na tarehe 7 Shawwal 1393 Hijria, alifariki dunia Ayatullah Mirza Abul Hussein Sha'rani, mwandishi wa kitabu cha tafsiri ya Qurani tukufu kinachojulikana kwa jina la ‘Manhaju al Sadiqiin’, akiwa na umri wa miaka 73. Msomi huyo licha ya kubobea katika elimu za kidini, alikuwa mahiri katika kuzungumza lugha za kigeni kama Kifaransa, Kiingereza na Kiarabu. Licha ya kuonyesha uwezo wake mkubwa katika tafsiri ya Qurani fukufu ya Manhaju al Sadiqiin chenye juzuu 10, Ayatullah Mirza Abul Hussein Sha'rani aliacha athari ya kitabu cha Sharhu Kifayatil Usul.