Alkhamisi, tarehe 27 Mei, 2021
Leo ni Alkhamisi tarehe 15 Shawwal 1442 Hijria sawa na Mei 27 mwaka 2021
Katika siku kama ya lo miaka 1439 ilyopita alizaliwa Abu Tufail A'mir bin Wathilah Kinani ambaye alikuwa miongoni mwa washairi na mahatibu mashuhuri za zama za awali za Uislamu. Abu Tufail alikuwa miongoni mwa masahaba wa Mtume Muhammad (saw) na alisuhubiana kwa muda mrefu na Imam Ali bin Abi Twalib (as) na kushiriki katika vita vya Siffin, Jamal na Nahrawan pamoja na mtukufu huyo. Abu Tufail alifaidika sana na elimu na maarifa ya mtukufu huyo. Mashari mengi ya A'mir bin Wathilah yanamsifu Mtume Muhammad (saw).

Siku kama ya leo miaka 1190 iliyopita inayosadifiana na tarehe 15 Mfunguo Mosi Shawwal mwaka 252 Hijria, alifariki dunia Abdul-Adhim al Hassani. Mtukufu huyu ni miongoni mwa wajukuu wa Mtume Muhammad SAW kupitia shajara ya Imam Hassan Al-Mujtaba (AS). Abdul-Adhim al Hassani alikuwa mashuhuri sana kwa karama zake nyingi. Maimamu watukufu walithibitisha ukweli na uchamungu wake na walikuwa wakinukuu hadithi kutoka kwake. Baada ya kushadidi dhulma na ukandamizaji wa utawala wa Bani Abbas, Abdul-Adhim al Hassani alilazimika kuhajiri na kuhamia mjini Rey kusini mwa Tehran ya leo. Mtukufu huyo anajulikana pia kama shahidi ambaye aliuawa kwa kupewa sumu. Haram Tukufu ya Abdul-Adhim Hassani ipo katika mji wa Rey na wapezi wa Ahlul Bayt AS kutoka kona mbalimbali za dunia humiminika katika eneo hilo kwa ajili ya kwenda kufanya ziara.
Siku kama ya leo miaka 194 iliyopita aliaga dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Seikh Muhammad Taqi Razi katika mji wa Isfahan nchini Iran. Sheikh Taqi Razi maarufu kwa jila la Agha Najafi, alielekea katika mji mtakatifu wa Najaf kwa ajili ya elimu ya juu ya kidini baada ya kukamilisha elimu ya msingi. Alipata elimu kwa wanazuoni mashuhuri kama Mirza Muhammad Hassan Shirazi na Sheikh Mahdi Kashiful Ghitaa. Baada ya kurejea Isfahan, Sheikh Agha Najafi alikuwa marejeo ya Waislamu katika masuala ya kidini na kisheria. Alikuwa mstari wa mbele kupambana na wakoloni kupitia harakati iliyopewa jina la Harakati ya Tumbaku. Vitabu mashuhuri vya mwanazuoni huyo ni pamoja na "Anwarul Arifin", "Asrarul Ayat" na "Al-Ijtihad Wattaqlid".

Siku kama ya leo miaka 184 iliyopita ulisainiwa mkataba wa amani kati ya serikali ya Ufaransa na Amir Abdulqadir wa Algeria, kiongozi wa wapigania uhuru wa nchi hiyo. Amir Abdulqadir aliendesha mapambano dhidi ya wavamizi huko Algeria na kusimama kidete dhidi yao kwa miaka kadhaa kuanzia mwaka 1832, kufuatia uvamizi wa jeshi la Ufaransa huko Algeria. Ni kwa msingi huo ndipo Amir Abdulqadir akafahamika kama kiongozi mshika bendera ya mapambano ya wananchi wa Algeria.
Miaka 111 iliyopita siku kama leo, aliaga dunia Robert Koch, mgunduzi wa vijidudu maradhi aina ya bakteria na tabibu mashuhuri wa Kijerumani aliyegundua chanzo cha maradhi ya kifua kikuu au TB. Daktari Robert Koch alianza kufanya utafiti mkubwa juu ya sababu au vyanzo vya kutokea baadhi ya magonjwa kama vile kipindupindu, kimeta na kifua kifuu baada ya kuhitimu masomo katika taaluma ya tiba. Mwaka 1882 Robert Koch alifanikiwa kugundua vijidudu maradhi vinavyoitwa mycobacterium tuberculosis vinavyosababisha kifua kikuu. Ili kukamilisha uchunguzi wake, tabibu huyo Mjerumani alisafiri katika nchi za Afrika Kusini, Misri na India na kuchunguza magonjwa mengineyo maarufu katika maeneo hayo kama vile Malaria. Mwaka 1905 Robert Koch alitunukiwa Tunzo ya Nobel katika uwanja wa Tiba.

Miaka 95 iliyopita katika siku inayofanana na hii ya leo, mapambano ya ukombozi ya Waislamu katika milima ya Rif nchini Morocco dhidi ya wakoloni wa Kihispania na wa Kifaransa yaligonga mwamba. Kwa miaka mingi, Muhammad Abdul-Karim al-Khattwabi, maarufu kwa jina la Amir Muhammad Rifi, kiongozi wa harakati hiyo, alifanya mapambano mengi na wavamizi wa Uhispania na kupata ushindi. Ushindi wake dhidi ya majeshi vamizi ya Uhispania uliitia khofu Ufaransa. Mwanzoni mwa mwaka 1924 askari wa Ufaransa waliingia Morocco kwa ajili ya kuwasaidia wenzao wa Uhispania dhidi ya harakati hiyo ya Rifi. Katika kipindi hicho askari hao wa Ufaransa walifanya mauaji makubwa dhidi ya raia wa nchi hiyo. Baada ya askari vamizi wa Ufaransa na Uhispania kumtia nguvuni Muhammad Abdul-Karim al-Khattwabi walitekeleza jinai kubwa dhidi ya maelfu ya Waislamu wa harakati ya Rifi.
Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita mwafaka na Khordad 6 mwaka 1328 Hijiria Shamsia, alifariki dunia Allamah Muhammad Qazwini, mwanafasihi, mtafiti na mwanahistoria wa zama hizi wa Iran. Tangu utotoni Allamah Qazwini na kwa msaada wa baba yake, alijifunza masuala mengi kuhusu fasihi na teolojia ya Kiislamu. Mwanazuoni huyo ameandika vitabu vingi katika uwanja wa fasihi, falsafa na historia.