Jun 14, 2021 06:05 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Juni 16

Hujambo mpenzi mwanaspoti natumai huna neno popote pale ulipo. Haya ni baadhi ya matukio yaliyogonga vichwa vya habari viwanjani ndani ya siku saba zilizopita.

Soka; Iran yaisasambua Cambodia 10-0

Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku ya Ijumaa iliinyoa bila maji Cambodia kwa kuchabanga mabao 10-0, katika mchuano wa kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia mwaka ujao 2022 nchini Qatar. Vijana wa Iran waliwatia skulini mahasimu wao wa Cambodia katika mechi hiyo ya saba ya kuwania kutinga Kombe la Dunia mwakani iliyopigwa katika Uwanja wa Khalifa mjini Isa. Alireza Jahanbakhsh aliifungulia Iran mvua ya mabao kwa kucheka na nyavu akiwa karibu na eneo la kupiga penati kunako dakika ya 16. Shoja Khalilzadeh aliongeza la pili dakika 6 baadaye, kabla ya Mehdi Taremi kufanya mambo kuwa 3-0 katika dakika ya 26 ya mchezo. Bao hilo liliwavuruga mabeki wa Cambodia, ambapo Sor Rotana alijifunga mwenye katika dakika ya 32. Katika kipindi cha pili, Iran ilirejea uwanjani kwa kasi ya juu zaidi, na kuendeleza wimbi la mashambulizi. Waliofunga mabao ya Iran baada ya kutoka mapumzikoni ni Milad Mohammadi (58), Morteza Pouraliganji (62), Karim Ansarifard (77, penati baada ya Mehdi Ghaedi kuchezewa ndivyo sivyo), Kaveh Rezaei (80), huku Ghaedi na Rezaei wakiongoza bao moja moja kila mmoja katika kipindi cha lala salama na kulizamisha kabisa jahazi la Cambodia.

Timu ya soka ya Iran

Kabla ya hapo, Team Melli ya Iran kama wanavyojulikana hapa nchini waliwasasambua vijana wa Bahrain mabao 3-0 katika mchuano wake mwingine, na kuzidi kujihakikishia nafasi ya kukipiga katika fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar. Aidha wiki iliyopita, Iran ilishuka dimbani kuvaana na Hong Kong katika kipute kingine cha timu za Asia za kusaka tiketi ya Kombe la Dunia mwaka ujao 2022 nchini Qatar, na Kombe la Asia litakaloandaliwa na Shirikisho la Soka Barani Asia (AFC) nchini China mwaka 2023. Iran imekwea kileleni kwenye kundi lake C, ikiwa na alama 15. Cambodia ambayo inavuta mkia kundini, imeyaaga mashindano hayo ya kusaka tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia ikiwa na alama moja tu.

Timu ya Wanariadha wa Iran yaenda Japan, Olimpiki ya Tokyo

Timu ya taifa ya riadha ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliyopewa lakabu ya "Kamanda wa Nyoyo" kwa kumuenzi Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC). Kamanda Soleimani na Abu Mahdi al Muhandis, aliyekuwa Naibu wa Mkuu wa Hashd al Shaabi ya Iraq pamoja na wenzao 8 waliuawa shahidi kidhulma tarehe 3 Januari 2020 katika shambulio la kiwoga na la kuvizia la wanajeshi magaidi wa Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad, mji mkuu wa Iraq. Kamati ya Paralimpiki ya Kitaifa ya Iran imechukua uamuzi wa kuipa timu hiyo ya wanariadha wa Iran lakabu ya "Kamanda wa Nyoyo" ili kumuezi Kamanda Soleimani na mashahidi wenzake.

Kamanda wa Soleimani

 

Timu hiyo yenye wanariadha, makocha na wasimamizi zaidi ya 70 imeondoka nchini Jumatatu hii kuelekea Japan kwa ajili ya kushiriki Michezo ya Olimpiki na Olimpiki ya Walemavu ya Tokyo, ambayo ilipaswa kufanyika mwaka jana lakini ikaakhirishwa hadi mwaka huu, kutokana na janga la Corona. Hatua ya Iran ya kuipa timu hiyo jina la kumuezi Shahidi Soleimani si suala jipya, kwani imekuwa ikifanya hivyo huko nyuma, kwa lengo la kuwaenzi mashahidi, na kushajiisha utamaduni wa kujitolewa kwenye michezo. Timu ya wanariadha ya Iran iliondoka nchini kwenda Brazil kwa ajili ya Paralimpiki ya Rio mwaka 2016 ilipewa jina la Mina, kwa ajili ya kuwaenzi Mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu ambao waliokufa shahidi katika tukio la mkanyangano mjini Makka nchini Saudia mwaka 2015. Aidha mwaka 2012, timu ya Iran iliyoenda kushiriki Olimpiki ya London nchini Uingereza ilipewa jina la Rais Ali Delvari, mmoja wa shakhsia muhimu waliokuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ukoloni wa Uingereza kusini mwa Iran.

Uongozi TFF

Wakati joto la uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likizidi kupanda, Hawa Mniga amekuwa mwanamke wa kwanza kuchukua fomu ya kuwania urais wa shirikisho hilo. Hawa amechukua fomu hiyo ili kupambana rais wa sasa wa TFF, Wallace Karia ambaye alichukua fomu ya kuwania tena nafasi hiyo Juni 8. Mwanamama huyo ambaye ni mtumishi wa umma, alifika ofisi za TFF siku ya Ijumaa na kisha kuingia moja kwa moja ndani kuchukua fomu. Baada ya nusu saa alitoka lakini akakataa kuzungumza lolote kwa madai sio muda wa kampeni na kisha kuondoka eneo hilo. Hawa ni mdau mkubwa wa soka na amewahi kuwa katika kamati ya ajira ya TFF.

Wallace Karia anayewania muhula mwingine wa uongozi wa TFF

 

Mchakato wa uchaguzi huu wa TFF umekumbwa na mizingwe, tuhuma na wagombea kupakana matope. Mgogoro huu wa kuelekea uchaguzi huo umewaibua wanasiasa, ambao walikuwa na maoni haya. Hadi sasa watu wanane wamechukua fomu ya urais ambapo mbali na Hawa na Karia, wengine ni Deogratius Mutungi, Ally Mayay, Evans Mgeusa, Oscar Oscar, Tarimba Abbas na Zahir Mohammed Haji. Kuna baadhi ya watu waliojitosa kwenye kinyang'anyiro hicho, lakini wakatoswa, inakuaje? Uchaguzi huo mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania utafanyika Agosti 7 jijini Tanga.

Riadha: Kenya na Ethiopia unyo kwa unyo

Mwanariadha bingwa wa Kenya Faith Chepng’etich Kipyegon aliweka rekodi ya kitaifa ya mbio za mita 1,500 baada ya kumaliza nyuma ya Mholanzi Sifan Hassan mjini Rome, Italia, Alkhamisi ya Juni 10. Bingwa huyo wa Olimpiki, Jumuiya ya Madola na Dunia Chepng’etich alitimka mizunguko hiyo mitatu kwa dakika 3, sekunde 53.91. Alivunja rekodi yake ya kitaifa ya dakika 3, sekunde 56.41 aliyotimka mjini Eugene nchini Marekani mnamo Mei 28 mwaka 2016. Sifan mwenye asili ya Ethiopia na ambaye alikuwa ameshinda mbio za mita 10,000 na kuweka rekodi ya dunia ya dakika 29, sekunde 06.82 mjini Hengelo nchini Uholanzi mnamo Juni 6, alitwaa taji la Rome la mita 1,500 kwa dakika 3:53.63. Muda wake ni rekodi ya duru ya Diamond League ya Rome na pia bora katika mizunguko hiyo mitatu mwaka huu 2021. Muingereza Laura Miur alimaliza wa tatu kwa kutumia dakika 3, sekunde 55.59. Hapo Alhamisi, Conseslus Kipruto alishindwa kumaliza mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji ambazo Mmorocco Soufiane El Bakkali alitawala kwa dakika 8, sekunde 08.54. Muethiopia Bikila Takele (8:10.56) na Mohamed Tindouft kutoka Morocco (8:11.65) waliridhika katika nafasi ya pili na tatu, mtawalia. Duru ijayo ya Ligi ya Almasi (Diamond League) itafanyika Julai 1 mjini Oslo, Norway.

Huku hayo yakiarifiwa, mwanariadha mkongwe wa Kenya, Tegla Loroupe ametajwa kuwa kiongozi wa msafara wa timu ya wanariadha 29 watakaoliwakilisha taifa hilo la Afrika Mashariki katika Olimpiki ya Tokyo nchini Japan kuanzia Julai 23 hadi Agosti 8. Kocha Joseph Domongole kutoka Kenya amechaguliwa kuitia makali timu hiyo ya riadha ya Kenya. Tayari wanamichezo hao watakaoiwakilisha Kenya kwenye Olimpiki nchini Japan wameshapigwa chanjo ya pili ya Covid-19. Wakenya 90 wamefuzu kushiriki michezo hiyo ya Olimpiki Japan.

Michuano ya Uropa

Mechi za Mashindano ya 16 ya Soka ya Ulaya (EURO 2020) zimeng'oa nanga kwa kishindo na ushindani mkali. Mechi iliyochezwa kati ya Wales na Uswisi katika Kundi A ilimalizika kwa sare ya 1-1, katika Uwanja wa Olimpiki huko Baku, mji mkuu wa Azerbaijan. Wakati kipindi cha kwanza kilimalizika kwa sare ya 0-0, kiungo Embolo aliifungia Uswisi bao la kwanza kwa kichwa kupitia mpira wa kona katika dakika ya 49, na kuiweka timu yake kifua mbele. Wales ilisawazisha goli hilo katika dakika ya 74 kupitia mchezaji Morrel aliyepokea pasi kutoka kwa mchezaji Moore kwenye eneo la hatari. Sare hiyo ya 1-1 imezifanya timu zote mbili ziondoke uwanjani na alama moja kila moja. Nayo Uturuki ilizabwa mabao 3-0 ilipovaana na Italia kwenye mechi ya ufunguzi ya Mashindano hayo ya Soka ya Uropa ya 2020 (EURO 2020). Katika mechi hiyo ya kwanza ya Kundi A iliyochezwa huko Roma, mji mkuu wa Italia, kipindi cha kwanza kilimalizika kwa sare tasa. Italia ilimaliza mechi hiyo kwa ushindi wa mabao 3-0 yaliyofungwa katika kipindi cha pili. Wakati huohuo, fowadi Romelu Lukaku alifunga mabao mawili na kusaidia Ubelgiji kuipepeta Russia mabao 3-0 katika mchuano wa Kundi B uliohudhuriwa na zaidi ya mashabiki 26,000 jijini St Petersburg Jumamosi ya Juni 12. Nyota huyo wa zamani wa Chelsea, Everton na Manchester United, alisema magoli yake ni heshima kwa mwanasoka mwenzake kambini Inter Milan, Christian Eriksen ambaye Shirikisho la Soka la Denmark lilithibitisha kwamba anaendelea kupata nafuu hospitalini. Eriksen, 29, alianguka ghafla na kuzimia uwanjani katika dakika ya 41 kabla ya kupelekwa hospitalini kwa matibabu zaidi wakati wa mechi iliyokutanisha timu yake ya taifa ya Denmark na Finland katika uwanja wa Parken jijini Copenhagen. Mechi hiyo ilisitishwa kwa takriban saa mbili kabla ya kurejelewa baada ya Shirikisho la Soka la Denmark kuthibitisha kwamba Eriksen alikuwa amepata fahamu. Findland ilipata ushindi hafifu wa bao 1-0. Uholanzi iiizaba Ukraine mabao 3-2, wakati ambapo Uingereza ilikuwa ikiikung'uta Croastia bao 1 bila jibu.

Kombe la Euro 2020

Soka; Copa Amerika

Michuano ya Copa Amerika imeanza kutifua mavumbi huku mwenyeji Brazil ikiinyuka Venezuela mabao 3-0, na Columbia 1-0 Ecuador.

……………………TAMATI……………..