Jun 28, 2021 07:08 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Juni 28

Karibu tutupie jicho japo kwa mukhtasari baadhi ya matukio yaliyogonga vichwa vya habari kwenye ulimwengu wa michezo ndani ya siku saba zilizopita.

Muirani bingwa wa kunyanyua vyuma vizito

Muirani, Masoud Barzam ametwaa taji la Mtu Mwenye Nguvu Zaidi Duniani katika mashindano ya kimataifa ya utunishaji misuli na kunyanyua vitu vizito katika Umoja wa Falme za Kiarabu. Muirani huyo ameibuka kidedea katika mashindano hayo ya kimataifa yaliyofanyika baina ya Jumamosi Juni 26 na Jumapili Juni 27 huko Imarati. Mbali na kutunukiwa medali ya dhahabu kwa kutwaa taji hilo la juu zaidi la World Ultimate Strong Man, ametia kibindoni pia medali nyingine ya dhahabu katika kategoria ya kilo 105. Kadhalika Iran imetwaa medali tatu za dhahabu, mbili za fedha na mbili za shaba kwenye mashindano hayo ya kimataifa UAE.

Masoud Barzam

 

Katika hatua nyingine, wanamieleka wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamezoa medali kadhaa katika mashindano ya mieleka mtindo wa Freestyle yaliyofanyika huko Russia. Katika mashindano hayo ya dunia yanayofahamika kwa Kimombo kama International Aliev Freestyle Cup yaliyofanyika katika mji wa Kaspiysk eneo la Dagestan na kufunga pazia lake Jumapili ya Juni 27, Iran imezawadiwa medali moja ya dhahabu na tatu za shaba. Medali ya dhahabu ya Iran ilitwaliwa na Mohammad Javad Ebrahimi katika safu ya wanamieleka wenye kilo 92, huku Amid Hossein Maqsudi, Arashk Mohebbi, na Mojtaba Golij wakizoa medali ya fedha kila mmoja katika kategoria za kilo 70, 92 na 97 kwa usanjari huo.

Mieleka mtindo wa kujiachia

 

Klabu Bingwa Afrika

Mabingwa watetezi wa Ligi ya Klabu Bingwa Afrika, klabu ya Al Ahly wamefanikiwa kutinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuvuna ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Esperance ya Tunisia wikendi huko jijini Cairo nchini Misri. Mafarao wa Misri hawakupata wakati mgumu kupata ushindi huo kwa kuwa walikuwa wanaupigia nyumbani, na mara nyingi mcheza kwao hutuzwa. Ahly walicheza kwa kasi kubwa na hawakutaka kuleta masikhara, kwani wiki iliyopita walipata ushinda hafifu wa bao 1-0 wakiwa ugenini katika Uwanja wa Stade Olympique de Rades, walipochuana na Esperance Sportive de Tunis ya Tunisia katika mchezo wa nusu fainali. Mabao ya Al Ahly katika mchezo wa Jumamosi yalifungwa na Ali Maâloul kupitia mkwaju wa penalti kunako dakika ya 38, Mohamed Sherif akivurimisha la pili nyavuni katika dakika ya 56 ya mchezo, kabla ya Hussein El Shahat kulizamisha kabisa jahazi la wageni wao kwa bao la kiufundi la tatu dakika nne baadaye. Kwa matokeo hayo Al Ahly wanatinga fainali mzima mzima kwa jumla wa magoli 4-0 kufuatia ushindi wa bao 1-0 kwenye mechi ya mkondo wa kwanza Jumamosi iliyopita Tunisia. 

Al Ahly watavaana na Kaizer Chiefs katika fainali, ambao wikendi hii wakiupigia nyumbani kwao Afrika Kusini waliambulia sare tasa dhidi ya Wydad Casablanca. Kilichowanusuru ni ushindi wa bao 1-0 katika mchuano wa mkondo wa kwanza wiki iliyopita. Ahly ndiye bingwa mtetezi wa kombe hilo na pia ndio mabingwa mara nyingi katika historia ya michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika wakiwa wamebeba kombe hilo mara tisa.

Katika hatua nyingine, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetangaza kuwa nchi hiyo ya Afrika Mashariki imefanikiwa kupeleka timu nne kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho kwa msimu wa 2021 – 2022. Hayo yamesemwa na Cliford Mario Ndimbo, Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF katika taarifa kwa vyombo vya habari.

Safari Rally Kenya

Mfaransa Sebastien Ogier ndiye bingwa wa Mashindano ya Magari ya Safari Rally Duniani (WRC). Hii ni baada ya kuongoza timu ya Toyota kufagia nafasi mbili za kwanza akishinda duru ya Safari Rally siku ya mwisho iliyohudhuriwa na Rais Uhuru Kenyatta na Mawaziri Amina Mohamed (Michezo) na Najib Balala (Utalii), miongoni mwa viongozi wengine, mjini Naivasha, kaunti ya Nakuru, eneo la Bonde la Ufa. Mkenya Onkar Rai aliibuka mshindi wa Safari Rally wa kitengo cha daraja ya tatu (WRC3) akiendesha gari la Volkswagen Polo alipokamilisha katika nafasi ya saba mnamo Jumapili. Bingwa mara saba duniani Ogier akishirikiana na Mfaransa mwenzake Julien Ingrassia, hawakutarajiwa kabisa kutawala mbio hizo. Hii ni baada ya gari lao la Toyota Yaris kuharikibika mnamo Juni 25 wakati madereva wengi walitaabika katika mkondo wa Kedong. Hata hivyo, Ogier, ambaye alikuwa amenyakua mkondo wa kufungua mashindano wa Kasarani ya kilomita 4.84 jijini Nairobi hapo Juni 24, aliendelea kuimarika baada ya kurekebisha gari lake.

 

Alinyakua mkondo wa Oserian 2 (kilomita 18.87), Soysambu 1 (20.33km), Sleeping Warrior1 (31.04km) na Elementaita2 (14.67km) na kuingia siku ya mwisho ya mashindano hayo ya kilomita 320.19 akiwa nyuma ya kiongozi Thierry Neuville (Hyundai) na Takamoto Katsuta (Toyota). Ogier sasa anaongoza jedwali la WRC mwaka 2021 kwa alama 133 baada ya duru sita za kwanza kwenye ligi hiyo ya duru 12. Alizoa pointi 27 kwenye Safari Rally. Evans anasalia katika nafasi ya pili kwa alama 99 baada ya kujiongezea alama moja ya kumaliza nafasi ya 10 na pointi tatu za bonasi kwa kasi. Neuville yuko nafasi ya tatu kwa alama 77 baada ya kuambulia pakavu Jumapili. Rais Uhuru Kenyatta amesema Kenya itaendelea kuwa mwenyeji wa mashindano hayo hadi mwaka 2026. Hii ni baada ya serikali ya Nairobi kufikia makubaliano na Shirikisho la Magari Duniani International Automobile Federation (FIA) na Shirikisho la Ubingwa wa Magari ya Safari Rally World Rally Championship (WRC). Mashindano hayo yaliyokuwa na msisimko wa aina yake yameakisiwa kitaifa, kieneo na kimataifa, labda kwa kuwa yamerejea kwa kishindo baada ya kusimamishwa kwa karibu miongo miwili.

Kuelekea Robo Fainali Euro 2020

Katika raundi 16 ya Mashindano ya Soka la Uropa (EURO 2020), Italia ilitinga robo fainali baada ya kuifunga Austria mabao 2-1 katika muda wa ziada wa mechi ambayo muda wake wa kawaida uliisha kwa sare ya 0-0. Italia na Austria zilikabiliana katika raundi ya 16 kwenye Uwanja wa Wembley huko London, Uingereza. Italia iliongoza kwa bao 1-0 dakika ya 95 dhidi ya Austria kupitia mchezaji Federico Chiesa. Baadaye katika dakika ya 105, Matteo Pessina alifungia Italia bao la pili na kubadilisha matokeo kuwa 2-0. Mchezaji wa Austria Sasa Kalajdzic naye pia aliifungia timu yake bao la pekee katika dakika ya 114 na kubadili matokeo kuwa 2-1.

Italia itapambana na Ubelgiji katika robo fainali. Fainali ya mashindano haya ya kieneo itapigwa Jumapili ya Julai 11 katika Uwanja wa Wembley jijini London, kwa kuwakutanisha mshindi wa Nusu Fainali 1 na mshindi wa Nusu Fainali 2.

Huku hayo yakiarifiwa, mashambuliaji wa Ureno, Cristiano Ronaldo amevunja rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza aliyefunga magoli mengi kwenye michuano ya Ulaya pamoja na Kombe la Dunia kwa ujumla. Mchezaji huyo ambaye alifunga magoli mawili na kutoka sare ya 2-2 dhidi ya Ufaransa alivunja rekodi hiyo iliyokuwa ikishikiliwa na mchezaji nyota wa zamani wa Ujerumani Miroslav Klose, ambaye alifunga magoli 19, kwa ujumla kwenye michuano ya Ulaya na Kombe la Dunia. Cristiano Ronaldo ambaye alifunga magoli yote mawili anaandika historia hiyo ya kuwa mchezaji aliyefunga magoli mengi kwa kufikisha magoli 21 katika michuano yote miwili yaani (Euro na Kombe La Dunia). Katika hatua nyingine, mchezaji huyo amefikia rekodi ya nguli wa zamani wa soka wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Ali Daei, ya kuwa wachezaji waliofunga magoli mengi kwenye Timu za Taifa wakiwa wamelingana kwa kufikisha magoli 109.

C. Ronaldo (CR7)

 

Ali Daei ambaye ni mchezaji wa zamani wa Iran aliyefunga Magoli 109, kwenye michuano ya Kimataifa kati ya mwaka 1993 na 2006, amempongeza Ronaldo, akisema kuwa mchezaji huyo katu hatasahaulika na atakumbukwa sana kwenye madaftari ya kumbukumbu. Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Iran, Mohammad Javad Jahromi amesema karibu hivi, Jamhuri ya Kiislamu itazindua muhuri maalumu kwa ajili ya kumuenzi Ali Daei. Ronaldo alitazamiwa Jumapili hii kuipiku rekodi hiyo ya Daei katika mchuano wa kusisimua wa Euro 2020, lakini timu yake ya Ureno iliishia kuzabwa bao moja bila jibu na Ubelgiji. Bao la Ubelgiji lilifungwa na Thorgan Hazard kunako dakika ya 42. Jamhuri ya Czech imesogea mbele pia kwenye michuano ya EURO 2020 baada ya kuichabanga Uholanzi mabai 2-0, wakati ambapo Wales ilikuwa ikinyolewa bila maji na Denmark, kwa kugaragazwa mabao 4-0.

Mwanasoka mkongwe wa Iran, Ali Daei

 

………………………..TAMATI……………..