Mchango wa Maulamaa wa Kishia (27) +SAUTI
Ni matumaini yangu kuwa, hujambo mpenzi msikilizaji popote pale yanapokufikia matangazo haya ya Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kwa uwezo na tawfiki ya Allah tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ili tuweze kufungua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa na wanazuoni wa Kishia. Kipindi chetu kilichopita kilimzungumzia Zeinuddin bin Ali bin Ahmad Amili Juba’i ambaye anajulikana pia kwa lakabu ya Shahidi Thani. Tulieleza kwamba, Shahidi wa Pili, ni fakihi na mwanazuoni mkubwa wa Kishia na mtajika wa ulimwengu wa Kiislamu. Alizaliwa tarehe 13 Mfunguo Mosi Shawwal 911 Hijria katika familia ya kielimu huko Jabal Amil, Lebanon. Sehemu ya 27 ya kipindi chetu juma hili, kitamzungumzia Ahmad bin Muhammad Ardabili mashuhuri zaidi kwa jina la Muqaddas Ardabili au Muhaqqiq Ardabili. Kuweni pamoja nami hadi mwisaho wa kipindi hiki.
Ahmad bin Muhammad Ardabili maarufu kama Muqaddas Ardabili au Muhaqqiq Ardabili ni mmoja wa Maulamaa wakubwa na mashuhuri katika Ulimwengu wa Kishia katika karne ya 10 Hijria. Alizaliwa katika mji wenye hali ya hewa nzuri wa Ardabil Iran na kuleleka katika familia iliyokuwa na mapenzi makubwa na kizazi cha Bwana Mtume (saw), familia ambayo iliondokea kuwa mashuhuri kwa uchaji Mungu na utakasifu. Baaada ya kukamilisha masomo ya msingi, akiwa na lengo la kujiendeleza zaidi kielimu alihajiri na kuelekea katika mji wa Najaf huko Iraq. Katika zama hizo, mji wa Najaf ulikuwa moja ya vituo vikubwa na muhimu vya elimu za Kiislamu na Fikihi ya Kishia. Alisoma masomo ya fikihi kwa wanafunzi wa Shahidi Thani. Muqaddas Ardabili akiwa na lengo la kunufaika na anga ya kielimu ya Najaf alibakia katika mji huo hadi mwishoni mwa umri wake na kunufaika na baraka za kuwa jirani na Haram ya Imam Ali bin Abi Twalib (as). Baada ya Shahidi Thani, Muqaddas Ardabili ndiye aliyechukua wadhifa wa Marjaa na Kiongozi wa Mashia mjini Najaf.

Sheikh Ahmad bin Muhammad Ardabili alifahamika zaidi baina ya watu kwa lakabu ya Muqaddas Ardabili huku akifahamika baina ya watu maalumu na wanazuoni wa Fikihi kama Muhaqqiq na Mudaqqiq Ardabili. Sababu ya umashuhuri huo ni uchaji Mungu aliokuwa nao pamoja na kujipamba kwa tabia njema na maadili mema kama ambavyo aliacha athari, vitabu na uhakiki wenye thamani katika uga wa fikihi na itikadi athari ambazo leo zimebakia kuwa kumbukumbu muhimu. Muqaddas Ardabili alifahamika pia kwa utakasifu wa nafsi na kuipa mgongo dunia na hivyo kufanikiwa kufikia ukamilifu. Baina ya wasomi na wanazuoni wa kale na waliokuja baadaye hakuna aliyekuwa na shakhsia kubwa kama Muqaddas Ardabili. Vitabu vyake vina umakini wa hali ya juu kinadharia na kiuhakiki.
Muqaddas Ardabili alikuwa akiishi katika zama za utawala wa Safavi nchini Iran. Katika vipindi vilivyotangulia tulisema kuwa, watawala na wafalme wa utawala wa ukoo wa Safavi kutokana na sababu mbalimbali za kidini, kisiasa na vilevile maslahi ya utawala, walikuwa wakiwaheshimu Maulamaa wa Kishia na hata kuomba ushauri kutoka kwao katika masuala tofauti.
Katika zama hizo kwa ombi la watawala wa Safavi, baadhi ya Maulamaa watajika wa Kishia kama Muhaqqiq Karaki walihajiri na kuondoka Iraq, Lebanon na maeneo mengine na kuja Iran na kuwa chimbuko la baraka na huduma kubwa kwa Ulimwengu wa Kishia. Hatua ya Maulamaa na wasomi wakubwa kama Muhaqqiq Thani, Sheikh Bahai, Allamah Majlisi ya kuzielekeza siasa za utawala wa Safavi upande wa kueneza na kusambaza Ushia, iliweza kutoa huduma isiyo na kifani kwa Uislamu na Ushia, kiasi kwamba, kipindi hicho kinahesabiwa kuwa moja ya zama za kuchanua na kufikia kilele fikra za Kishia. Licha ya kuwa Shah Abbas, alimuita na kumtaka mara kadhaa Muqaddas Ardabili aliyekuwa Marjaa mkubwa wa Kishia wakati huo, arejee nchini Iran, lakini mwazuoni huyo alikataa mwaliko huo. Muqaddas Ardabili alikuwa akiona kuwa, uwepo wake katika mji wa Najaf wakati huo lilikuwa jambo la dharura zaidi.
Pamoja na kuwa, Muqaddas Ardabili alikataa takwa la Shah Abbas la kurejea Iran, lakini kwa ajili ya maslahi ya Ushia daima alikuwa akitoa tanabahisho na maelekezo kwa utawala huo. Ukumbusho huo ulikuwa ukipokelwewa kwa heshima na taadhima na Shah Abbas.

Wakati Muqaddas Ardabili anaingia katika uga wa harakati za kielimu na kitablighi, Chuo cha Kiislamu cha Najaf (Hawza) hakikuwa na ustawi na ile hali ya kung'ara kama ilivyokuwa kama zama za Sheikh Tusi, na kulikuwa na wanafunzi wachache tu waliokuwa wakisoma katika chuo hicho. Katika mazingira kama hayo, Muqaddas Ardabili alifanya hima na juhudi kubwa na kuelekeza idili yake kwa ajili ya kuhuisha chuo hicho ambapo akiwa na subira na ustahamilivu wa hali ya juu pamoja na irada thabiti, alifanya kila awezalo kukabiliana na mapungufu yaliyokuwako. Kutokana na sifa na haiba ya kimaanawi aliyokuwa nayo, alimu huyo aliweza kuipatia Hawza hiyo moyo na uhai mpya.
Kuhusiana na hili, Ayatullah Sayyid Hassan Sadr mmoja wa Marajii wakubwa wa Kishia katika karne ya 13 na 14 Hijria ameandika hivi: "Katika zama za Muqaddas Ardabili, kwa mara nyingine tena watafuta elimu walianza kukimbilia na kuelekea Najaf, chuo hicho kikaimarika na watu wakaelekea huko kutoka miji na mataifa mbalimbali na kuufanya mji huo kuwa kituo kikubwa zaidi cha kielimu."
Moja ya huduma kubwa iliyofanywa na Muhaqqiq Ardabili kwa ajili ya Ulimwengu wa Kishia ni kulea wanafunzi mahiri ambao baadaye waliondokea kuwa wasomi wenye mchango mkubwa na kila mmoja wao kuwa msomi mkubwa na mujtahidi. Aidha wanafunzi hao baadaye wakawa chimbuko la athari zenye thamani kwa ajili ya Ulimwengu wa Kiislamu.
Muhaqqiq Ardabili alivifanyia uhakiki na uchunguzi wa kina vitabu vilivyokuwa vikifundishwa katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Najaf na hakuwa akifundisha baadhi ya mambo ambayo kwa mtazamo wake aliyaona hayana faida kwa wanafunzi, ili kwa njia hiyo ipatikane fursa ya kujadili na kufanyia utafiti mambo ya kimsingi na muhimu katika vitabu hivyo.
Mmoja wa wanafunzi wake muhimu zaidi zaidi ni Sheikh Hassan, mtoto wa Shahidi Thani na mtunzi wa kitabu cha Maalim al-Usul, na Sayyid Muhammad, mjukuu wa Shahidi Thani ambaye ndiye mwandishi wa kitabvu cha Madarik al-Ahkam.
Ikhlasi katika kufundisha na kutoa mafundisho ni miongoni mwa sifa za dhahiri na za kipekee alizokuwa nazo Muqaddas Ardabili. Msomi huyo ambaye alikuwa kiongozi wa Chuo cha Kiislamu cha Najaf alikuwa na tawadhui na unyenyekevu wa hali ya juu kwa Maulamaa wengine hususan mbele ya wanafunzi wake na alikuwa akiwaheshimu na kuwathamini mno.
Wapenzi wasikilizaji kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki, sina budi kukomea hapa kwa leo. Tukutane tena Juma lijalo ambalo tutaendelea kumzungumzia Ahmad bin Muhammad Ardabili maarufu kama Muqaddas Ardabili au Muhaqqiq Ardabili. Hadi tutakapokuutana tena wakati mwingine, ninakuageni nikikutakieni usikilizaji mzuri wa sehemu iliyobakia ya matangazo yetu leo.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh