Sep 06, 2021 06:09 UTC
  • Spoti, Agosti 30

Hujambo mpenzi msikilizaji na haswa mfuatiliaji wa masuala ya spoti natumai huna neno. Karibu tutupie jicho baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika pembe mbalimbali za dunia....

Wanariadha wa Iran wang'ara Paralimpiki Japan

Timu ya wanamichezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imemaliza katika nafasi ya 13 kwenye Michezo ya Olimpiki ya Walemavu iliyofanyika katika mji mkuu wa Japan, Tokyo. Wanariadha hao wameweka historia kwa kuvuna medali kochokocho katika mashindano hayo ya paralimpiki ya dunia. Iran imeshinda jumla ya medali 24, zikiwemo 12 za dhahabu. Timu hiyo ya Jamhuri ya Kiislamu pia imetia kibindoni medali 11 za fedha, na moja ya shaba. Wanamichezo 4,400 wameshiriki Michezo ya Paralimpiki ya Tokyo huko Japan, yaliyoakhirishwa kwa mwaka mzima kutokana na janga la Corona. Iran imewakilishwa na wanamichezo 62 ambao walimaliza kibarua cha kusaka medali kwa udi na uvumba Jumamosi. Wamamichezo wa Iran waliotwaa medal za dhahabu ni pamoja na Rouhollah Rostami -kunyanyua uzani (powerlifting); majudoka Vahid Nouri na Mohammad Reza Kheirollahzade; Amir Khosravani – mchezo kuruka (long jump); na Mahdi Olad – kurusha kitufe (shot put). Wengine ni Hashemiyeh Motaghian – kurusha mkuki (javelin); Sareh Javanmardi katika mchezo wa kulenga shabaha kwa bunduki; Saeid Afrooz – kurusha mkuki, Zahra Nemati; ulengaji shabaha kwa uta na upote (archery); Hamed Amiri – mkuki; na Asghar Azizi Aghdam – taekwondo. Kadhalika timu ya voliboli ya kuketi sakafuni (sitting volleyball) ya Iran imelipa taifa hili dhahabu nyingine, mbali na kumiminiwa sifa kwa michezo mizuri. Katika ngoma ya fainali iliyopigwa Jumamosi, timu hiyo ya voliboli ya walemavu ya Iran iliigaragaza Russia seti 3-1 (25-21, 25-14, 19-25, 25-17).  

Michezo ya Olimpiki na Paralimpiki ya Japan ilipaswa kufanyika mwaka jana lakin ikaakhirishwa kutokana na janga la Corona

 

Kabla ya kutinga fainali, timu hiyo ilizitesa Ujerumani, Brazil na China katika mechi za Kundi B, kabla ya kuitandika Bosnia Hezergovina katika mchezo wa nusu fainali. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewapa pongezi wanamichezo hao wa Iran kwa kung'ara katika mashindano hayo ya kimataifa. Katika ujumbe wake wa pongezi, Ayatullah Ali Khamenei amewashukuru wanamichezo hao kwa kunyunyizia furaha na fakhari nyoyo za wananchi wenzao wa Iran. Kadhalika Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Sayyid Ebrahim Raisi ameinyooshea mkono wa tahania timu hiyo ya taifa ya walemavu ya Iran kwa kulipa fakhari na kulipaisha taifa hili kimataifa, kupitia michezo. China imemaliza ya kwanza katika mashindano hayo ya paralimpiki, kwa kuzoa medali 207, zikiwemo dhahabu 96. Nchi ya Afrika iliyojitutumua ni Tunisia, ambayo ipo katika nafasi ya 28, kwa kuzoa medali 11 zikiwemo 4 za dhahabu. Ikumbukwe kuwa, Iran ilimaliza katika nafasi ya 27 katika Mashindano ya Kimataifa ya Olimpiki ya Tokyo 2020 nchini Japan yaliyomalizika Julai 23, 2021. 

Jeshi la Iran lashinda Michezo ya Kimataifa ya Majeshi

Wanajeshi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wameibuka kidedea katika Mashindano ya Kimataifa ya Wanajeshi yaliyofanyika hapa nchini. Duru ya sita ya mashindano hayo ya kijeshi ya majeshi ya dunia yaliyofanyika huko Shahin katika mji wa Isfahan Iran, ilifunga pazia lake Septemba 3. Michezo hiyo ya kijeshi imehudhuriwa na timu nne za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Russia, Uzbekistan na Vietnam. Moja ya malengo ya duru ya sita ya mashindano hayo ya kijeshi ya majeshi ya dunia huko Isfahan ni kuimarisha amani, urafiki na kuzidisha uhusiano wa kiutamaduni kati ya Iran, Russia, Vietnam na Uzbekistan. 

Mbio za Kombe la Dunia 2022

Timu ya taifa soka ya Kenya Harambee Stars siku ya Jumapili ilishuka dimbani kuvaana na vijana wa Amavubi wa Rwanda katika mchuano wa kusisimua wa kusaka tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia nchini Qatar mwaka ujao 2022. Mchuano huo uliishia kwa sare ya kufungana bao 1-1. Katika mchezo huo uliopigwa katika Uwanja wa Taifa wa Kigali, Michael Olunga aliifanya Kenya iwe ya kwanza kucheka na nyavu, dakika 10 baada ya kupulizwa kipyenga cha kuanza ngoma. Hata hivyo wenyeji Rwanda walisawazisha mambo kupitia bao la kiufundi lililopachikwa wavuni na Abdul Rwatubyaye dakika 11 baadaye.

Qatar kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia mwakani

 

Kabla ya hapo, na kwa mara ya nne mfululizo, mechi kati ya timu za taifa za Kenya na Uganda ilikosa kupata mshindi baada ya Harambee Stars na Cranes kutoa sare 0-0 katika mchuano wa Kundi E wa kufuzu kushiriki Kombe la Dunia 2022, Alkhamisi. Katika mechi hiyo ambayo mshambuliaji matata Michael Olunga alikuwa akirejea kikosini baada ya kukosa ile mechi ya Togo jijini Lome kutokana na virusi vya corona, Wakenya walizidiwa ujanja kupenya ngome ya Waganda.

Soka; Cecafa Wanawake

Klabu ya Vihiga Queens ya Kenya imetinga mzima mzima nusu-fainali ya mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) ya kufuzu kushiriki Ligi ya Klabu Bingwa Afrika kwa upande wa akinadada; baada ya kuisasambua New Generation kutoka Zanzibar mabao 8-0 katika Uwanja wa Nyayo jijini Nairoibi siku ya Ijumaa. Jentrix Shikangwa alitetemesha nyavu za Wazenji mara tatu kwa mabao ya hatrick, Tereza Engesha mara mbili nao Mercy Anyango, Robai Kebedi na Maureen Achieng’ wakachangia bao moja kila mmoja katika mechi hiyo ya mwisho ya Kundi B. Akina dada hao wanaonolewa na makocha Charles Okere na Boniface Nyamunyamu walijikatia tiketi kwa kumaliza Kundi B katika nafasi ya pili kwa alama sita, tatu nyuma ya wanabenki wa CBE kutoka Ethiopia waliolipua Yei Joint Stars kutoka Sudan Kusini mabao 10-0. Vihiga watamenyana na washindi wa Kundi A Simba Queens ya Tanzania katika nusu-fainali mnamo Septemba 6 nao CBE watalimana na Lady Doves kutoka Uganda waliokamilisha Kundi A katika nafasi ya pili kwa tofauti ya ubora wa magoli baada ya wote kutoshana kwa pointi saba kila mmoja.

Nembo za mashirikisho ya soka ya nchi wanachama wa CECAFA

 

Lady Doves walilima PVP kutoka Burundi mabao 3-0 Ijumaa ya Septemba 3. Yei na Generation wamebanduliwa kutoka Kundi B nao PVP na FAD kutoka Djibouti wameaga mashindano kutoka Kundi A. Washindi wa Cecafa pekee watafuzu kushiriki michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika baadaye mwaka huu wa 2021 nchini Misri.

Riadha; Ligi ya Almasi

Mshikilizi wa rekodi ya Kenya ya mbio za mita 100, Ferdinand Omanyala Omurwa alijizolea dola 2,000 baada ya kumaliza duru ya Riadha za Diamond League ya Brussels katika nafasi ya nne nchini Ubelgiji hapo Ijumaa ya Septemba 3. Mwanafunzi huyo wa Chuo Kikuu cha Nairobi, ambaye aliweka rekodi ya kitaifa ya sekunde 9.86 nchini Austria mnamo Agosti 14, alitimka umbali huo kwa sekunde 10.02 akimaliza nyuma ya Waamerika Fred Kerley sekunde 9.94, Trayvon Bromell sekunde 9.97 na Michael Norman sekunde 9.98. Omanyala alimaliza mbele ya Rohan Browning kutoka Australia sekunde (10.14), mshikilizi wa rekodi ya Afrika ya sekunde 9.84 Akani Simbine kutoka Afrika Kusini (10.18), Mfaransa Mouhamadou Fall (10.19) naye Arthur Cisse akavuta mkia (10.34). Bingwa wa dunia mita 5,000 Hellen Obiri alikuwa Mkenya wa kwanza katika mbio za mita 5,000 akitamatisha wa tatu na kufuatiwa na Margaret Chelimo, Lilian Kasait na Eva Cherono. Ferguson Rotich ndiye Mkenya pekee aliyevuna ushindi mjini Brussels alipotawala mbio za mita 800 za wanaume kwa dakika 1:43.81. Cornelius Tuwei alimaliza mbio hizo za kuzunguka uwanja mara mbili katika nafasi ya tatu (1:45.29) kati ya washiriki 10. Brusseles ilikuwa duru ya 12. Jiji la Zurich nchini Uswizi litaandaa duru ya mwisho baina ya Septemba 8-9.

………………………..TAMATI………………