Oct 01, 2021 02:25 UTC
  • Ijumaa tarehe Mosi Oktoba 2021

Leo ni Ijumaa tarehe 24 Safar 1443 Hijria sawa na Oktoba Mosi mwaka 2021.

Katika siku kama ya leo miaka 1058 iliyopita Sahib bin Ubbad, mwanafasihi maarufu na msomi wa Kiislamu wa kizazi cha Dailami alifariki dunia. Sahib alikuwa mwandishi hodari na mtu mwenye hadhi na mashuhuri sana katika zama zake. Licha ya kwamba alikuwa waziri katika serikali ya kizazi cha Dailami, lakini alikuwa mtu mnyenyekevu na mwema kwa watu wa chini yake. Sahib bin Ubbad ameandika vitabu vingi, na maarufu zaidi ni kile cha "al Muhiit" chenye juzuu saba.

Mahali lilipo kaburi la Sahib bin Ubbad, Isfahan

Tarehe Mosi Oktoba ni siku ya Wazee Duniani. Siku hii ulitengwa kwa ajili ya kuwakirimu na kuwaenzi watu wa tabaka hilo. Ni vyema kukumbusha hapa kuwa hapa nchini Iran na kutokana na mabadiliko yaliyotokea baada ya Mapinduzi ya Kiislamu na utamaduni wa Kiislamu unaotawala hapa nchini wazee na watu wazima wanapewa nafasi ya juu ndani ya familia na katika jamii.

Miaka 72 iliyopita katika siku kama ya leo, kuasisiwa kwa Jamhuri ya Watu wa China kulitangazwa rasmi na Mao Tse Tung akachaguliwa kuwa rais wa jamhuri hiyo. Nchi ya China yenye ustaarabu mkongwe, ilikuwa chini ya udhibiti wa madola ya Ulaya kuanzia mwishoni mwa karne ya 16. Mara kadhaa Wachina walianzisha vita dhidi ya mkoloni hasa Muingereza ili kuikomboa nchi yao lakini hawakufanikiwa. Mwaka 1912 mapinduzi yaliyoongozwa na Sun Yat-Sen dhidi ya mfumo wa utawala wa Kifalme yalizaa matunda na kiongozi huyo akachaguliwa kuwa rais wa China.

Bendera ya China

Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, nchi ya Nigeria ilipata uhuru. Wareno waliwasili Nigeria katika karne ya 15 na mkoloni Mwingereza naye akawasili katika nchi hiyo katika karne ya 16. Katika karne ya 17 ardhi ya Nigeria iligeuzwa na kuwa moja kati ya vituo muhimu vya biashara ya utumwa. Mwishoni mwa karne ya 19 vikosi vya majeshi ya Uingereza, viliidhibiti kikamilifu ardhi ya Nigeria. Mwaka 1914 Uingereza uliziunganisha nchi mbili za Nigeria ya Kaskazini na Kusini zilizokuwa chini ya udhibiti wake na kuunda koloni moja la Nigeria. Miaka 40 baadaye nchi hiyo ikajitangazia kuwa na utawala wa ndani. Hatimaye baada ya kupitia misukosuko mingi, Nigeria ikajipatia uhuru katika siku kama ya leo.

Bendera ya Nigeria

Miaka 36 iliyopita sawa na siku kama ya leo ya tarehe Mosi Oktoba mwaka 1985 ndege za kijeshi za utawala haramu wa Israel ziliyashambulia makao ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) huko Tunisia. Watu wapatao 70 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa kufuatia mashambulio hayo. PLO ilikuwa imehamishia makao yake Tunisia kutoka Lebanon baada ya mashambulio ya kijeshi ya utawala haramu wa Israel nchini humo mwaka 1982. Hata hivyo uungaji mkono wa Marekani kwa utawala huo ulilifanya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kushindwa kuchukua hatua zozote za maana dhidi ya Tel Aviv.

Tags