Oct 09, 2021 18:51 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (28)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale yanapokufikieni matangazo haya ya Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

 

Kwa uwezo na tawfiki ya Allah tumekutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ili tuweze kufungua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa na wanazuoni wa Kishia, mchango wao katika Uislamu pamoja na kazi na athari zao. Kipindi chetu kilichopita kilianza kumzungumzia Ahmad bin Muhammad Ardabili mashuhuri zaidi kwa jina la Muqaddas Ardabili au Muhaqqiq Ardabili. Tulisema kuwa,  Muqaddas Ardabili ni mmoja wa Maulamaa wakubwa na mashuhuri katika Ulimwengu wa Kishia katika karne ya 10 Hijria. Alizaliwa katika mji wenye hali ya hewa nzuri wa Ardabil nchini Iran na kukulia katika familia iliyokuwa na mapenzi makubwa na kizazi cha Bwana Mtume (saw), familia ambayo iliondokea kuwa mashuhuri kwa uchaji Mungu na utakasifu wa nafsi. Sehemu ya 28 ya mfululizo huu juma hili itaendelea na maudhui hii. Karibuni.

 

Moja ya kazi na huduma kubwa na yenye thamani iliyofanywa na Muqaddas Ardabili ni kuhuisha Chuo Kikuu cha Kiislamu (Hawza) cha Najaf nchini Iraq na kulea wanafunzi mahiri na stadi. Alimu na msomi huyu alikuwa na nafasi na mchango mkubwa pia katika kueneza mafundisho ya Kiislamu kutokana na vitabu vingi alivyoalifu kuhusiana na maudhui mbalimbali hususan masuala ya kiitikadi, fikihi, Usulul-Fiqih na sira ya Ahlul-Baiti (as).

Miongoni mwa vitabu muhimu ni kile kinachojulikana kwa jina la Majmau al-Faidah Walburhan Fi Sharh Irshad al-Adh’han. Kitabu hiki ni moja ya vitabu mashuhuri na ni kitabu kilichokusanya maarifa ya hali ya juu na ya kina kabisa kuhusu Elimu ya Fikihi. Aidha kitabu hiki kinahesabiwa kuwa moja ya vyanzo muhimu na vyenye kiwango cha hali ya juu kuhusiana na Fikihi ya Madhehebu ya Jaafaria yaani Shia Ithnaashariyah.

 

Kitabu hiki daima kimekuwa kikipewa umuhimu na wasomi hasa wanazuoni waliofikia daraja ya Ijtihad. Licha ya kuwa, Muhaqqiq Ardabili aliandika kitabu hiki akitoa sharh na ufafanunzi wa kitabu cha Irshad cha Allamah Hilli, lakini kitabu hiki kina wigo mpana mno wa ufafanuzi, na alikiandika kwa umakini mkubwa na wa hali ya juu. Katika kitabu hiki Muhaqqiq Ardabili amechambua kielimu mno masuala mbalimbali yanayohusiana na Elimu ya Fikihi.

Moja ya kazi na huduma nyingine muhimu ya mwanazuoni huyu katika uga wa Fikihi ni kwamba, aliijengea elimu ya fikihi na Ijtihadi juu ya riwaya. Ukisoma  kitabu chake cha Majmau al-Faidah Walburhan Fi Sharh Irshad al-Adh’han cha Muhaqqiq Ardabili utaona kuwa, mwanazuoni huyu ameweka na kubainisha majimui kamili kabisa ya hadithi na riwaya kuhusiana na Furu’u din yaani Matawi ya Dini. Kabla ya mwanazuoni huyo, wanachuoni waliotangulia kabla yake walikuwa wakizingatia riwaya na hadithi katika masuala ya fikihi na wakitoa fatuwa kwa mujibu wa riwaya hizo, lakini, mbinu na mtindo maalumu wa alimu huyu ulikuwa wa aina yake.  

 

Muhaqqiq Ardabili alikuwa akiamini kuwa, fikihi ni elimu na maarifa kwa ajili ya maisha. Katika kutoa fatuwa na kubainisha hukumu, Muhaqqiq Ardabili alitoa fatuwa na kubainisha hukumu kwa mbinu ya uwiano na iliyozoeleka ambayo ilikwenda sambamba na mahitaji ya wakati huo pamoja na uhakika na uhalisia wa maisha ya watu.

Alimu huyo alikuwa akizingatia msingi wa kufanya mambo kuwa mepesi katika maamrisho ya dini na alikuwa akiamini kwamba, katika hukumu za kisheria kuanzia masuala ya kiibada mpaka katika miamala na mabadilishano pamoja na milango mingine ya fikihi haipasi kuwaweka watu katika mazingira magumu na ya mbinyo bila sababu yoyote. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 185 ya Surat al-Baqarah kwamba:

Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito. Aidha anasema katika Aya ya 78 ya Surat al-Hajj:  Yeye amekuteueni. Wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika Dini.

Mbali na Aya hizo, kuna riwaya na hadithi nyingi zinazoeleza na kubainisha kwamba, hukumu na sheria za dini ni nyepesi na ni zenye kutekelezeka. Hata hivyo ili kutoa tafsiri ya Aya hizi na kuainisha mpaka wa wepesi wenyewe uko wapi, kuna haja ya kuomba msaada na kuwarejea wasomi na watu waliobobea katika elimu ya tafsiri. Hapana shaka kuwa, Muhaqqiq Ardabili ni mmoja wa wasomi hao.

Moja ya sifa alizokuwa amejipamba nazo Muhaqqiq Ardabili ni kuchunga na kuzingatia suala la heshima kwa wengine hata wale waliokuwa ni wapinzani wake. Alimu huyu alikuwa akipinga mitazamo mingi ya wasomi na wanazuoni iliyokuwa imeenea katika zama zake kuhusiana na masuala mbalimbali ya kidini na kielimu na alikuwa akitoa fatuwa mpya ambazo zilikuwa zikikinzana na kupingana na wanazuoni wengine. Pamoja na hayo, hakuonyesha hata chembe ya dharau na kuwavunjia heshima wale aliopingana nao au kuwa na misimamo mikali dhidi yao.

 

Ahmad bin Muhammad Ardabili mashuhuri zaidi kwa jina la Muqaddas Ardabili au Muhaqqiq Ardabili

 

Muhaqqiq Ardabili alikuwa akiamiliana kimantiki pia na wafuasi wa madhehebu ya Kisuni na alikuwa akiwaheshimu mno wanazuoni na maulamaa wao. Itikadi yake pamoja na mitazamno yake katu havikumtoa katika njia ya insafu na uadilifu na hakuna wakati ambao alifungua kinywa chake na kusema maneno yasiyofaa. Katika zama zake kuna watu waliokuwa wakiamini kwamba, hata kuweka na kuwa na vitabu vya Masuni si jambo linalofaa. Hata hivyo, Muhaqqiq Ardabili alikuwa akiamini kuwa, katika vitabu vya Masuni kuna mambo sahihi na yasiyo sahihi ambayo yamekusanyika pamoja na hivyo haiwezekani yote yaliyomo ndani ya vitabu hivyo kuyataja kuwa ni mambo ya upotovu na hivyo kuyatupilia mbali.

Bali jambo la msingi ni kunufaika na mambo yaliyo sahihi na kuweka kando hadithi za kutengeneza na kubuni. Alikuwa akiamini kwamba, inawezekana kutenganisha jambo sahihi na la haki katika batili kwa kutumia hoja. Kutokana na kuwa na mtazamo huo, msomi huyo alisoma na kutwalii vitabu vingi vya Madhehebu ya Suni na baadhi ya wakati alifanya utafiti na uchunguzi sambamba na kukosoa mitazamo ya Maulama wakubwa wa Kisuni akitumia hoja madhubuti.

Aidha mwanazuoni huyu alikuwa akitilia mkazo mno suala la kuweko mahusiano ya kijamii na Waislamu wa Kisuni. Kwa hakika yote haya yanaonyesha na kudhihirisha ni jinsi gani Muhaqqiq Ardabili alikuwa na insafu, uadilifu, fikra huru na upeo wa hali ya juu hasa katika kipindi kile ambacho kulikuwa kumeenea mno fikra za mitazamo mikali na ya kuchupa mipaka katika jamii.

Licha ya alimu huyo kuwa na heshima na taadhima kubwa na hata huba na mapenzi makubwa kwa Maulamaa wa kabla yake na shakhsia wakubwa wa zama zake, lakini hilo halikumfanya aikubali na kuipokea mitazamo yao ya kielimu bila ya kuitafakari na kuifanyia utafiti.

Ushujaa wa Muhaqqiq Ardabili katika kuchambua na kuhakiki nadharia na mitazamo ya wasomi waliotangulia ulifungua mlango na njia mpya katika Elimu ya Fikihi na hilo kuleta maendeleo katika fikihi ya Kishia.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh