Spoti, Oktoba 11
Hujambo mpenzi msikilizaji na hususan mfuatiliaji wa masuala ya spoti natumai huna neno. Karibu tutupie jicho baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika pembe mbalimbali za dunia....
Mieleka: Wairani wazoa medali kibao Norway
Wanamieleka wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamezoa medali si haba katika mashindano ya dunia ya Mabingwa wa Mieleka huko Oslo, mji mkuu wa Norway. Siku ya Jumapili, Mohammadreza Geraei aliipa Iran medali ya nne ya dhahabu baada ya kuibua kidedea katika pambano la fainali, kwenye mieleka mtindo wa Greco Roman. Hii ni baada ya barobaro huyo Muirani ambaye pia alishinda dhahabu katika Michezo ya Olimpiki ya Tokyo 2020 iliyofanyika mwaka huu huko Japan, kumbwaga kwa alama 5-2 mshindani wake kutoka Russia, Nazir Abdullaev katika kateogoria ya wanamieleka wenye kilo 67. Wanamieleka wengine wa Iran waliotwaa medali za dhahabu katika mashindano hayo ya kimataifa yanayofahamika kama World Wrestling Championships kwa Kiingereza, ni Mohammadhadi Saravi 97kg, Aliakbar Yousefi 130kg na Meysam Dalkhani 63kg. Aidha Iran imetwaa medali mbili za fedha na kuibuka katika nafasi ya pili kwenye mashindano hayo. Washindi wa medali za fedha ni Mohammad-Ali Geraie 77kg na Pezhman Poshtam 82kg. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameipongeza timu hiyo kwa kufanya vyema.

Ayatullah Ali Khamenei amesema anatumai kuwa wanamichezo hao wa Ira wataendelea kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya siku za usoni. Naye Rais wa Iran amewanyooshea mkono wa tahania wanamichezo hao wa Kiirani kwa kuliweka jina la taifa hili katika ramani ya dunia kupitia michezo, kwa mara nyingine tena.

Katika ujumbe wake wa pongezi, Sayyid Ebrahim Raisi amesema: Mwanga wa kudumu na wa kihistoria wa wanamieleka wa nchi yetu wa Greco-Roman na kuibuka katika nafasi ya pili baada ya kuzoa medali nne za dhahabu na mbili za fedha, umelipa furaha na fakhari taifa azizi la Iran. Rais Raisi amewapongeza pia maafisa na makocha wa timu ya taifa ya mieleka ya Iran kwa jitihada zao, na kusema kuwa anataraji kuwa Iran itaendelea kung'ara kimataifa hata kwenye michezo mingine. Aidha Waziri wa Vijana na Michezo wa Iran, Hamid Sajjadi ameipongeza timu hiyo ya mieleka ya Greco-Roman ya Jamhuri ya Kiislamu kwa kufanya vyema kwenye mashindano hayo ya dunia huko Norway. Iran imeibuka ya pili kwa kuzoa jumla ya alama 146, ikitanguliwa na Russia iliyoibuka kidedea kwa kuchota pointi 152, huku Azerbaijan ikifunga orodha ya tatu bora kwa kuambulia alama 107.
Dondoo: Timu ya taifa ya soka ya Iran Jumanne hii inatazamiwa kuwa mwenyeji wa Korea Kusini katika mchuano wa kusaka tiketi ya Kombe la Dunia mwakani nchini Qatar. Timu hizo zitagaragazana katika Uwanja wa Azadi hapa jijini Tehran, ukiwa ni mchuano wa mkondo wa tatu wa Kundi A. Na difenda ngangari wa Iran, Rouzbeh Cheshmi amerejea katika klabu yake ya zamani ya Esteqlal. Mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 28, amesaini mkataba miaka miwili wa kuichezea klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Soka ya Iran, aliyoiacha msimu uliopita na kujiunga na klabu ya Ummu Salal ya Qatar.
Soka Wanawake; Tanzania mabingwa COSAFA
Timu ya taifa ya soka ya wanawake ya Tanzania 'Twiga Stars’ imetwaa ubingwa wa mashindano ya kandanda ya timu za kusini mwa Afrika yaliyoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Kusini mwa Afrika (Cosafa), baada ya kuifunga Malawi bao 1-0 kwenye mchezo wa fainali uliopigwa mjini Port Elizabeth huko Afrika Kusini.
Twiga imefanikiwa kuchukua ubingwa huo kwa mara ya kwanza tangu ianze kualikwa na mwaka pekee iliowahi kufanya vizuri ilikuwa 2011 ambapo ilimaliza katika nafasi ya tatu. Goli la Tanzania lilifungwa dakika ya 64 na Enekia. Tuzo ya mchezaji bora wa mchezo huo ilichukuliwa na nahodha wa Twiga Amina Bilal ambaye pia alichukua tuzo ya mchezaji bora wa mashindano.
Mbio za kuwania kutinga Kombe la Dunia 2022
Timu ya taifa ya kandanda ya Tanzania 'Taifa Stars' imefufua matumaini ya kusonga mbele kwenye hatua inayofuata ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia mwakani nchini Qatar baada ya kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Benin. Mechi hiyo ilianza kwa timu zote kushambuliana na dakika ya sita tu ya mchezo, Simon Msuva aliipatia bao la kuongoza Stars baada ya kuwatoka walinzi wa Benin na kuingia ndani ya boksi na mpira kisha kupiga shuti kali lililozama moja kwa moja kwenye nyavu za Benin.

Hadi kipindi cha pili kinamalizika Stars ilikuwa inaongoza kwa bao 1-0. Matokeo hayo yanaifanya Stars kufikisha alama saba baada ya kucheza mechi nne na kuongoza kundi J.
Huku Tanzania ikifufua matumaini ya kusogea mbele, nchi jirani ya Kenya ilikuwa inabanduliwa kwenye kampeni za kufuzu kushiriki Kombe la Dunia mwaka ujao 2022 nchini Qatar, baada ya kuzabwa bao 1-0 na Mali katika mechi ya nne ya Kundi E jijini Nairobi, siku ya Jumapili. Vijana wa kocha Mturuki Engin Firat watajilaumu wenyewe kukosa bao ama hata ushindi dhidi ya taifa hilo kutoka Afrika Magharibi baada ya kupoteza nafasi chungu nzima katika kipindi cha kwanza. Bao la Mali lilifungwa na Ibrahima Kone akikamilisha pasi kutoka kwa Charles Traore. Mali inasalia juu ya jedwali kwa alama 10, mbili mbele ya Uganda Cranes iliyoinyuka Amavubi Stars ya Rwanda bao 1-0 mjini Entebbe.
Kwengineko, Argentina ilishindwa kupenya ngome ya Paraguay waliowalazimishia sare tasa katika mechi ya Alkhamisi usiku ya kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia nchini Qatar. Huku hayo yakijiri, fowadi Raphinha Belloli wa Leeds United aliisaidia Brazil kutoka nyuma na kusajili ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Venezuela Alhamisi usiku katika mechi nyingine ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia. Na Northern Ireland walishuhudia Jamal Lewis akionyeshwa kadi nyekundu kwa kosa la kupoteza muda katika mechi iliyowapa Uswisi fursa ya kuwapiga mabao 2-0 na kuyeyusha kabisa matumaini yao ya kutinga fainali za Kombe la Dunia mwakani.
Ligi ya Mataifa ya Ulaya
Fainali ya Ligi ya Mataifa ya Uropa (Nations League) mwaka huu ilipigwa Jumapili hii ya Oktoba 10, katika Uwanja wa San Siro jijini Milan, huku mechi ya kutafuta mshindi wa tatu kati ya Ubelgiji na Italia ambao ni mabingwa wa Euro ikiandaliwa jijini Turin.
Ufaransa ilitoka nyuma na kupata ushindi mnono wa mabao 2-1 dhidi ya Uhispania katika mchuano wa kusisimua wa fainali. Na kwa kuwa kutangulia sio kufika, bao la Mikel Oyarzabal halikutosha kuipaisha Uhispania, na badala yake, Wafaransa walitoka nyuma na kufunga mawili kupitia washambuliaji nyota, Karim Benzema na Kylian Mbappe.

Kabla ya hapo, Italia iliizaba Ubelgiji 2-1 katika kwenye mchuano wa kutafuta mshindi wa tatu wa UEFA Nations League.
Saudia na New Castle
Wakurugenzi na wakuu wa timu mbalibali zinazoshiriki Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza wameeleza kusikitishwa kwao na hatua ya kuuruhusu utawala wa Aal-Saud ukiongozwa na mrithi wa ufalme wa nchi hiyo Muhammad bin Salman ununue asilimia 80 ya hisa za klabu ya soka ya New Castle ya Uingereza, kwa thamani ya dola milioni 300. Timu hizo za EPL zimesema ni jambo la kusikitisha kuiruhusu serikali ya Riyadh imiliki klabu hiyo ambayo ipo katika hatari ya kushushwa daraja ligini, licha ya rekodi yake nyeusi ya haki za binadamu. Weledi wa mambo ya spoti wanasisitiza kuwa, ni fedheha kubwa kwa usimamizi wa EPL kuidhinisha muamala huo. Haya yanajiri huku mpango wa umiliki wa klabu ya Newcastle United kutwaliwa na Hazina ya Uwezekaji wa Umma (PIF) nchini Saudi Arabia ukikamilika. Usimamizi wa EPL umeidhinisha utaratibu huo baada ya kupokea vyeti vya kisheria vinavyohakikisha kwamba Serikali ya Saudi haitadhibiti kwa namna yoyote ile uendeshaji wa shughuli mbalimbali za kikosi hicho. Kwa mujibu wa mapatano hayo, PIF itapokeza Newcastle United ufadhili wa asilimia 80 ya fedha za kujiendeshea akthari ya shughuli zake. Ifahamike kuwa, bin Salman ndiye mwenyekiti wa PIF.

Kubadilishwa kwa umiliki wa Newcastle United kunatamatisha ghafla kipindi cha miaka 14 cha kuhudumu kwa Mike Ashley kama mmiliki wa Newcastle United. Ashley ambaye ni Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya Sports Direct, alinunua kikosi cha Newcastle United mnamo Mei 2007. Idadi kubwa ya mashabiki wa Newcastle United walikongamana nje ya uwanja wa St James’ Park mnamo Ijumaa ya Oktoba 8, kusherehekea tukio hilo la kubadilishwa kwa umiliki wa klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL). Thamani ya mali ya PIF inakadiriwa kufikia pauni 250 bilioni, kiasi cha fedha ambacho sasa kinafanya Newcastle kuwa miongoni mwa klabu tajiri zaidi duniani kwa sasa. Mara ya mwisho kwa Newcastle kutwaa taji la haiba kubwa katika ulingo wa soka ni 1955 walipotia kapuni ufalme wa Kombe la FA.
………………….TAMATI….…………..