Oct 25, 2021 08:56 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Oktoba 25

Hujambo mpenzi msikilizaji na hususan mfuatiliaji wa masuala ya spoti natumai hujambo hapo ulipo. Karibu tutupie jicho baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika pembe mbalimbali za dunia....

Mpira wa magongo; Iran yang'ara

Timu ya taifa ya wanawake ya mpira wa magongo unaochezwa kwenye theluji ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka katika nafasi ya pili kwenye mashindano ya kimataifa ya mchezo huo yaliyoifanyika mjini Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu. Akina dada hao wa Kiiarani walikubali kichapo cha magoli 3-1 walipovaana na Russia katika mchuano wa fainali.

Timu hiyo ya wanawake ya Iran imeibuka mshindi wa pili licha ya kuwa hii ni mara yao ya kwanza kushiriki mashindano ya kimataifa ya kiwango hicho. Mashindano hayo ya kimataifa ya mpira wa magongo kwa upande wa wanawake yalianza Oktoba 18 na kumalizika Oktoba 20.

Taekwondo; mashindano ya dunia ya Fajr

Timu ya taifa ya wanaume ya taekwondo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka kidedea kwenye Mashindano ya Kimataifa ya Taekwondo ya Fajr yaliyofanyika hapa mjini Tehran. Duru ya 31 ya mashindano hayo yalianza Ijumaa na kufunga pazia lake Jumamosi.

Mwanataekwondo wa Iran akimtandika mpinzani

Wanataekwondo 171 kutoka nchi za Iran, Armenia, Afghanistan, Pakistan, Uturuki, Russia, Iraq, Lebanon na India wameshiriki kwenye mashindano hayo katika kategoria mbalimbali. Iran wametawazwa mabingwa wa mashindano hayo kwa kuzoa alama 1004, mbali na medali nane za dhahabu. Uturuki imeibuka ya pili baada ya kutia kibindoni medali tatu za fedha, huku Pakistan ikifunga orodha ya tatu bora kwa kujinyakulia medali medali moja ya fedha.

Rais Raisi awatuza wanariadha waliong'ara Olimpiki Tokyo

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ebrahim Raisi ameinyooshea mkono wa tahania timu ya taifa ya riadha ikiwemo ile ya walemavu ya Iran kwa kung'ara katika Michezo ya Olimpiki na Paralimpiki ya Tokyo huko Japan. Akiongea katika hafla ya kuwatuza wanariadha hao wa Iran hapa jijini Tehran siku ya Jumapili, Sayyid Raisi amewashukuru wanamichezo hao kwa kumimina furaha na fakhari katika nyoyo za wananchi wenzao wa Iran. Hii hapa sehemu ya shamrashamra za utoaji wa tuzo hizo kwa mabingwa wa riadha wa Iran waliofanya vyema huko Tokyo, Japan.

Rais Raisi na timu ya wanariadha wa Iran walioshinda Paralimpiki na Paralimpiki ya Tokyo 2020

Waziri wa Vijana na Michezo wa Iran, Hamid Sajjadi na wanamichezo wakongwe wa Jamhuri ya Kiislamu ni miongoni mwa wageni waalikwa walioshiriki kwenye hafla hiyo. Timu ya wanamichezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilimaliza katika nafasi ya 13 kwenye Michezo ya Olimpiki ya Walemavu iliyofanyika katika mji mkuu wa Japan, Tokyo. Wanariadha hao wameweka historia kwa kuvuna medali kochokocho katika mashindano hayo ya paralimpiki ya dunia. Iran ilishinda jumla ya medali 24, zikiwemo 12 za dhahabu, 11 za fedha, na moja ya shaba. Kabla ya hapo, Iran ilimaliza katika nafasi ya 27 katika Mashindano ya Kimataifa ya Olimpiki ya Tokyo 2020 nchini Japan yaliyomalizika Julai 23, 2021. 

Kabla ya kuwatuza wanariadha wa Iran waliong'ara Tokyo, Rais Raisi alihudhuria kitimtimu cha fainali ya mieleka ya Pahlavani katika ukumbi wa ndani wa Uwanja wa Azadi hapa Tehran. Mieleka mtindo wa Pahlavani ya Iran inatambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kama moja ya michezo ya kale zaidi duniani.

Soka; Ligi ya Mabingwa Afrika

Klabu ya Simba ya Tanzania imebanduliwa katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu huu baada ya kukubali kuzabwa mabao 3-1 na Jwaneng Galaxy ya Botswana, licha ya kuupigia nyumbani katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jiji Dar es Salaam. Katika kipindi cha kwanza cha mechi hiyo, Simba ilionekana kulishambulia mara kwa mara lango la Jwaneng lakini kipa wao Ezekiel Morake alipangua mikwaju ya Simba. Wekundu wa Msimbazi waliishia kufunga bao moja pekee lililopachikwa wavuni na Rally Bwalya kunako dakika ya 40. Msimu uliopita, Simba ilitinga hatua hiyo na kwenda hadi robo fainali na kutolewa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini. Huku hayo yakiarifiwa, klabu ya Biashara ya Tanzania ingali inasubiri tamko la Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) ili kujua hatma ya mechi yake ya Shirikisho dhidi ya Al Ahly Tripoli ya Libya. Mechi hiyo ilipangwa kucheza wikendi nchini humo. Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia ameliambia gazeti la Mwananchi kwamba bado wanasubiri taarifa ya CAF juu ya ombi la kusogezwa mbele mchezo huo hadi Jumanne.

Kwengineko, miamba ya soka nchini Kenya, klabu ya Gor Mahia imetinga kiwepesi mkondo wa mwisho wa mechi za Kombe la Shirikisho la CAF. Hii ni baada ya klabu ya Al Ahly Merowe ya Sudan kujizuia kushiriki mchuano wa mkondo wa pili uliotazamiwa kupigwa Jumapili katika Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi. Baada ya kuvuna ushindi mnono wa mabao 3-1 wiki iliiyopita nchini Misri, Kogalo walikuwa na uhakika wa kupeta nyumbani kwenye mchuano wa Jumapili.

Nayo klabu ya Tusker imeyaaga mashindano hayo baada ya kuchabangwa na Zamalek ya Misri mabao 4-0 siku ya Ijumaa. Tusker walikuwa mawindoni kufuta kichapo cha goli moja walichopokea kutoka kwa mibabe hiyo ya Misri, waliporudiana katika mechi ya Klabu Bingwa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) katika Uwanja wa Burg El Arab mjini Alexandria mnamo Ijumaa Oktoba 22. Vijana wa kocha Robert Matano walihitaji ushindi wa mabao 2-0 ili kusalia kwenye mashindano hayo. Hata hivyo, walijikuta wanakung'utwa vibaya sana na Waarabu ugenini. Ndo yale ya mgeni njoo mwenyeji apone?

Riadha Afrika Mashariki

Mwanariadha nyota wa Tanzania, Alphonce Simbu ameendeleza makali yake katika mbio baada ya kuibuka mshindi wa kwanza wa mbio za Rock City Marathon zilizofanyika jijini Mwanza, zikishirikisha wanariadha kutoka Tanzania, Kenya na Uganda. Simbu ambaye Agosti mwaka huu aliiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Olimpiki yaliyofanyika nchini Japan na kushika nafasi ya saba baada ya kukimbia kilometa 50 kwa kutumia saa mbili dakika 11 na sekunde 35; aliendeleza makali hayo baada ya kushinda mbio za kilometa 21 kwa wanaume baada ya kutumia saa moja dakika sita na sekunde 19, huku mwanariadha wa Kenya Bernad Msau akishika nafasi ya pili kwa kutumia saa moja dakika saba na sekunde sita. Wakati huohuo, Mtanzania mwingine, Shingade Giniki aliibuka mshindi wa tatu baada ya kukimbia mbio hizo kwa saa moja dakika saba na sekunde 35. Kwa upande wa wanawake kilometa 21, Mkenya Isgan Cheruto aliibuka mbabe baada ya kutumia saa moja dakika 17 na sekunde 31 huku nafasi ya pili hadi ya 10 zikibebwa na Watanzania.

Kipchoge wa Kenya atuzwa tena!

Katika hatua nyingine, bingwa mara mbili wa mbio za marathon katika Olimpiki, Eliud Kipchoge wa Kenya ameshinda tuzo ya mwanariadha bora wa kiume duniani. Kipchoge ametawazwa kuwa mshindi wa Tuzo za Wanariadha Bora katika Michezo ya Olimpiki ya Tokyo 2020 iliyofanyika mwaka huu nchini Japan. Hafla ya utoaji wa tuzo hizo iliyoandaliwa na Baraza la Kamati za Kitaifa za Olimpiki (ANOC), ilifanyika Jumapili nchini Ugiriki. Kipchoge alikabidhiwa tuzo hiyo na Rais wa baraza hilo kanda ya Afrika, Mustapha Berraf.

Kipchoge wa Kenya

Kipchoge amekuwa mwanariadha wa tatu wa kiume kuhifadhi taji la olimpiki kwa upande wa wanaume, akila kwenye meza moja sasa na Abebe Bikila wa Ethiopia aliyeshinda (1960 na 1964) na Mjerumani Waldemar Cierpinski (1976 na 1980). Wakati huo huo, jina la mwanariadha huyo bora duniani mwaka 2018 na 2019 limetiwa katika orodha ya wawaniaji wa tuzo ya mwanariadha bora dunia mwaka 2021. Shirikisho la Riadha Duniani (WA) siku ya Alkhamisi lilitangaza majina ya wanariadha 10 wataoawania tuzo hiyo ya kifahari itakayopeanwa mwezi Desemba mwaka huu 2021. Kipchoge atachuana na miamba ya riadha duniani kama vile bingwa wa Olimpiki mbio za mita 5,000 Joshua Cheptegei (Uganda), na mshindi wa Olimpiki na Diamond League wa kurusha tufe Ryan Crouser (Marekani).

Ligi ya EPL

"Najiamini, sing'atuki ng'o!" Si kauli yangu mpenzi msikilizaji, bali ni matamshi ya mkufunzi wa klabu ya Manchester United Ole Gunnar Solskjaer ambaye anakabiliwa na mashinikizo ya kutakiwa aachie ngazi, baada ya timu yake kuandamwa na wimbi la vichapo. Kichapo cha hivi punde ni kile cha Jumapili, ambapo Mashetani Wekundu walilishwa mabao 5-0 licha ya kuupigia nyumbani Old Trafford.

Mo Salah na wenzio wa Liverpool wakishangilia bao

Man U walipokea kichapo hicho kutoka Liverpool, katika mchuano ambao mshambuliaji nyota wa Reds, Mohamed Salah alifunga mabao matatu ya hatrick. Kidogo wapate bao la kufutia machozi kutoka kwa Criatiano Ronaldo, lakini mitambo ya VAR ikagundua kuwa aliotea. Huku hayo yakijiri, Mason Mount alipachika wavuni mabao matatu na kuifanya Chelsea kupepeta Norwich City mabao 7-0 uwanjani Stamford Bridge. Katika mchuano mwigine wikendi, Phil Foden alipachika wavuni mabao mawili katika mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ulioshuhudia Manchester City wakichabanga Brighton mabao 4-1 ugani Amex Jumamosi usiku. Ushindi huo wa Man-City ambao ni mabingwa watetezi wa EPL uliwapaisha hadi nafasi ya pili jedwalini kwa alama 20, mbili nyuma ya viongozi Chelsea. Wakati huohuo, mabao matatu ya hatrick kutoka kwa mshambuliaji Joshua King yalisaidia Watford kupepeta Everton 5-2 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumamosi uwanjani Goodison Park. Masaibu ya Tottenham Hotspur chini ya kocha Nuno Espirito msimu huu yaliendelezwa na West Ham United waliowacharaza 1-0 kwenye mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika Uwanja wa London.

………………………TAMATI……..……….