Oct 26, 2021 02:29 UTC
  • Jumanne tarehe 26 Oktoba mwaka 2021

Leo ni Jumanne tarehe 19 Rabiul Awwal 1443 Hijria sawa na Oktoba 26 mwaka 2021.

Miaka 74 iliyopita katika siku kama hii ya leo eneo la kiistratejia la Jammu na Kashimir liliunganishwa na India baada ya nchi hiyo kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza na Pakistan kujitenga na India. Ilipangwa kuwa, eneo la Jammu na Kashmir lenye wakazi wengi Waislamu litajiunga na Pakistan lakini mtawala wa eneo hilo akichochewa na India na Uingereza, aliamua kuliunganisha na India na kupuuza matakwa ya wananchi. Baada ya kutangazwa habari hiyo Pakistan ililishambulia eneo hilo na kutwaa sehemu ya Jammu na Kashmir. Tangu wakati huo hadi sasa India na Pakistan zimepigana vita mara mbili juu ya umiliki wa eneo la Jammu na Kashmir na hitilafu za pande hizo mbili zingali zinaendelea.

Siku kama ya leo tarehe nne Aban miaka 57 iliyopita Imam Ruhullah Khomeini baada ya kuachiwa huru kutoka katika jela ya utawala wa Shah alitoa hotuba kali akishambulia vikali kitendo cha kupasishwa sheria ya kuwapa kinga raia wa Marekani waliopatikana na hatia ya kufanya uhalifu nchini Iran. Katika hotuba hiyo Imam Khomeini alizishambulia vikali Marekani na utawala ghasibu wa Israel. Hotuba hiyo iliwaamsha wananchi na kuukasirisha utawala wa kiimla wa Shah kiasi kwamba, uliamua kumuwekea vizuizi vingi kiongozi huyo wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita mji wa Khorramshahr wa Iran ulikaliwa kwa mabavu na jeshi la dikteta wa zamani Iraq Saddam Hussein. Mji wa Khorramshahr uko katika mkoa wa Khozestan kusini magharibi mwa Iran. Mji huo ulikuwa chini ya uvamizi wa majeshi ya Iraq kwa muda wa karibu mwaka mmoja na miezi minane. Mji huo ulikombolewa tarehe 3 Khordad ambayo inajulikana katika utamaduni wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa jina la "Siku ya Istiqama na Ushindi.

Khorramshahr

Siku kama ya leo miaka 26 iliyopita maajenti wa shirika la ujasusi la Israel Mossad walifanya mauaji ya kigaidi dhidi ya Katibu Mkuu wa zamani wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina, Dakta Fathi Shiqaqi, akiwa huko Malta. Shiqaqi alizaliwa mwaka 1951 katika kambi ya wakimbizi wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza. Alihitimu masomo ya udaktari na kufanya kazi katika hospitali moja ya Baitul Muqaddas. Alianzisha harakati za mapambano dhidi ya utawala ghasibu wa Israel akiwa bado kijana. Mwaka 1979 Dakta Shiqaqi alikamatwa na kusweka jela nchini Misri kwa sababu ya kuandika kitabu kuhusu harakati za Imam Ruhullah Khomeini na ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Dakta Shuqaqi aliitangaza Siku ya Kimataifa ya Quds iliyoainishwa na Imam Khomeini, kuwa ni siku ya kuhuisha Uislamu na mapambano ya jihadi dhidi ya Wazayuni huko Palestina.

Dakta Fathi Shiqaqi