Dec 05, 2021 22:53 UTC
  • Jumatatu, Disemba 6, 2021

Leo ni Jumatatu tarehe Mosi Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1443 Hijria sawa na Disemba 6 mwaka 2021 Milaadia.

Katika siku kama ya leo miaka 243 iliyopita yaani tarehe 6 Disemba mwaka 1778, alizaliwa Joseph Louis Gay-Lussac mwanafizikia na mwanakemia wa Ufaransa. Gay-Lussac alifanya tafiti nyingi na kugundua vitu mbalimbali katika kipindi cha maisha yake. Miongoni mwa mambo yaliyogunduliwa na mwanakemia huyo ni gesi ya sumu ya halogen, kipimio cha ulevi, hydromita au chombo cha kupimia uzito wa maji na viowevu na kuitambua Chloride na Iodine kama elementi mpya. Miongoni mwa kazi zake muhimu za kisayansi alizofanya mwanakemia huyo ni kuweka kanuni ya kupanuka kwa gesi. Kanuni hiyo iliyopewa jina lake pamoja na la mshirika wake ilijulikana kama Law of Charles and Lussac. Gay-Lussac alifariki dunia mwaka 1850.

Joseph Louis Gay-Lussac

Miaka 232 iliyopita siku kama ya leo yaani mwaka 1211 Hijiria, alifariki dunia mshairi mkubwa wa Kiislamu, Sheikh Kadhim Tamimi Baghdadi, maarufu kwa jina la Uzri akiwa na umri wa miaka 80. Alikuwa msomi na mwanafasihi mkubwa na ameacha diwani ya mashairi. Miongoni mwa mashairi ya malenga huyu maarufu wa Kiislamu ni shairi maarufu la "Al Uzriya" ambalo linamsifu Mtukufu Mtume Muhammad (saw) na kizazi chake kitukufu na kubainisha misingi ya dini ya Uislamu. Shairi hilo lina zaidi ya beti 1000.

Siku kama ya leo miaka 134 iliyopita Ayatullah Mirza Muhammad Hassan Shirazi alitoa fatuwa maarufu ya kuharamisha tumbaku na sigara ili kuzuia uporaji uliokuwa ukifanywa na wakoloni wa Kiingereza katika nchi za Kiislamu. Fatua hiyo ilitolewa baada ya mfalme Nasiruddin Shah wa Iran kutia saini mkataba wa kuipa kampuni moja ya utawala wa kikoloni wa Uingereza mamlaka ya kuuza na kununua tumbaku ya Iran kwa kipindi cha miaka 50. Jina la Mirza Shirazi ni mashuhuri mno kutokana na fatua hiyo ya kuharamisha tumbaku. Fatua yake hiyo ya kuharamisha tumbaku na matumizi ya sigara, bidhaa ambayo ilikuwa imehodhiwa na Uingereza, ilitoa pigo kubwa kwa ukoloni wa Uingereza nchini Iran. Vilevile fatua hiyo ilitambuliwa kuwa mapambano ya moja kwa moja dhidi ya utawala wa Shah na ukoloni wa Uingreza nchini Iran na iliandaa uwanja wa mapambano ya baadaye ya wananchi wa Iran dhidi ya dhulma, ukandamizaji na ukoloni wa wageni.

Ayatullah Mirza Muhammad Hassan Shirazi

Miaka 104 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Finland iliyokuwa chini ya utawala wa Russia ilijipatia uhuru. Kuwa jirani Finland na Russia kuliwatia wasiwasi mno viongozi wa Finland, kiasi kwamba, katika karne ya 12 waliiomba Sweden iwahami dhidi ya Moscow. Badala yake Wasweden waliikalia kwa mabavu Finland. Mwaka 1721 Russia iliivamia Finland na kudhibiti sehemu ya ardhi ya nchi hiyo. Hatimaye mwaka 1917 vikosi vamizi vya Russia vililazimika kuondoka nchini Finland na nchi hiyo ikajitangazia uhuru.

Miaka 41 iliyopita katika siku kama hii ya leo alikufa shahidi rubani Ahmad Keshvari. Brigedia Ahmad Keshvari aliingia katika Jeshi la Anga la Iran mwaka 1351 Hijria Shamsia na kuhitimu mafunzo ya kuendesha helikopta. Baada ya ushindi wa Mapindizi ya Kiislamu nchini mwaka 1979 alitoa mchango mkubwa katika kupambana na makundi yaliyokuwa dhidi ya Mapinduzi katika maeneo ya magharibi mwa Iran na baadaye kidogo aliteuliwa kuwa kamanda wa Jeshi la Anga katika eneo la Ilam. Baada ya jeshi la Saddam Hussein kuvamia ardhi ya Iran, Brigedia Keshvari alikuwa mstari wa mbele kupambana na jeshi la adui na kulisababishia hasara kubwa ya nafsi na mali. Ahmad Keshvari aliuawa shahidi baada ya kukamilisha operesheni iliyokuwa na mafanikio akiwa njiani kurejea nchini.

Ayatullah Mirza Muhammad Hassan Shirazi

Tarehe 6 Disemba miaka 29 iliyopita, Wahindu wenye misimamo mikali waliubomoa Msikiti wa Babri katika mji wa Faizabad kwenye jimbo la Uttar Pradesh nchini India. Msikiti huo ulijengwa mwaka 1528 na Zahiruddin Muhammad Babur juu ya kilima na tangu wakati huo ulijulikana kwa jina la Msikiti wa Babri. Baada ya kupita karne tatu tangu ujengwe yaani mwaka 1855, mtawala mmoja Muingereza alipotosha ukweli kwa makusudi na kuandika kuwa msikiti huo umejengwa kwenye magofu ya jumba la ibada ya masanamu la Wahindu. Suala hilo lilikuwa chanzo cha fitina na ugomvi mkubwa kati ya Waislamu na Wahindu. Mwaka 1992 Wahindu wenye misimamo ya kufurutu mipaka walivamia Msikiti wa Babri na kuubomoa kikamilifu, suala ambalo lilizusha vita baina ya Waislamu na Wahindu.

Msikiti wa Babri

Miaka 25 iliyopita katika siku kama ya leo, mtayarishaji filamu mashuhuri wa Iran, Ali Hatami aliaga dunia. Baada ya kuhitimu masomo katika Chuo cha Sanaa hapa nchini, Hatami alijiunga na televisheni ya taifa na kujishughulisha na masuala ya filamu. Filamu zake nyingi ziliakisi mapenzi yake makubwa kwa utamaduni wa Iran. Miongoni mwa filamu hizo ni Sattarkhan, Sutedelan, Kamalul Mulk na Maadar yaani Mama.

Ali Hatami