Jumanne tarehe 7 Disemba 2021
Leo ni Jumanne tarehe Pili Jamadi Awwal 1443 Hijria sawa na Disemba 7 mwaka 2021.
Miaka 1052 iliyopita siku kama hii ya leo, alifariki dunia malenga wa Kiirani Abu Is'haq Kesa-i Marvazi. Alizaliwa mwaka 341 Hijria katika mji wa Marv, moja kati ya miji ya Iran ya zamani, ambao hivi sasa unapatikana katika ardhi za Turkmenestan. Malenga huyu aliishi katika zama za mwisho za utawala wa Kisaman na mwanzoni mwa zama za utawala wa Maghaznavi. Marvazi alitunga beti kadhaa za mashairi kukisifu kizazi cha Mtukufu Mtume Muhammad (saw) hasahasa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Malenga huyu mkubwa wa Kiirani ameacha tungo kadhaa za mashairi.
Tarehe 7 Disemba miaka 132 iliyopita gari la kwanza la kisasa duniani lilitengenezwa. Gari hilo lililokuwa na uwezo wa kutembea kilomita 12 kwa saa lilitengenezwa na msomi wa Kijerumani aliyejulikana kwa jina la Karl Friedrich Benz. Gari hilo lilitumia nishati ya petroli au alkoholi. Karl Benz alifariki dunia mwaka 1929.
Miaka 80 iliyopita katika siku inayosadifiana na ya leo, wakati Vita vya Pili vya Dunia vilipokuwa vimeshadidi barani Ulaya, ndege mia mbili za kivita za Japan zilishambulia kituo cha jeshi la Marekani katika bandari ya Pearl Harbor. Shambulizi hilo lilifanyika wakati Japan ilikuwa katika mazungumzo na Marekani kuhusu masuala ya mashariki mwa Asia. Sambamba na mashambulizi hayo ambayo yaliharibu meli 19 za kivita za Marekani, jeshi la Japan pia lilifanya mashambulizi makubwa katika nchi za kusini mwa Asia. Baada ya mashambulizi hayo Marekani ikatangaza vita dhidi ya Japan na Vita vya Pili vya Dunia vikapanuka zaidi hadi mashariki mwa Asia.
Siku kama ya leo miaka 68 iliyopita, inayosadifiana na 16 Azar 1332 Hijria Shamsia, upinzani wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tehran dhidi ya safari ya Richard Nixon, Makamu wa Rais wa Marekani katika kipindi hicho hapa nchini, ulipelekea wanachuo watatu kuuawa na askari vibaraka wa utawala dhalimu wa Shah. Safari hiyo ilifanyika miezi mitatu na nusu tu baada ya mapinduzi ya Marekani dhidi ya serikali ya Dakta Muswaddeq. Siku ya pili baada ya mauaji hayo, Richard Nixon alitunukiwa shahada ya heshima ya uzamivu wa sheria katika Chuo Kikuu cha Tehran. Kwa mnasaba huo, tarehe 16 Azar kila mwaka huadhimishwa nchini Iran kama "Siku ya Mwanachuo" hapa nchini.
Na katika siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, Abdul Wahhab Kayyali mmoja wa wanamapambano wa Palestina aliuawa na magaidi wa Kizayuni mjini Beirut. Aliingia katika masuala ya kisiasa akiwa mwanafunzi na risala yake ya shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha London pia ilihusu masuala ya Palestina na mapambano ya Waarabu dhidi ya ukoloni na Uzayuni.