Jumatano, Disemba 8, 2021
Leo ni Jumatano tarehe 3 Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1443 Hijria sawa na tarehe 8 Disemba 2021 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 153 iliyopita, ulianguka utawala wa Washugani au kwa jina jingine watawala wa kijeshi huko Japan. Kuanguka kwa utawala huo kulipelekea kuanza kwa marekebisho ya kijamii, kisiasa na kiutamaduni nchini humo. Washugani walikuwa moja kati ya makumi ya silsila zenye nguvu huko Japan, walioanzisha utawala wao wa kidikteta tangu karne ya 12 Miladia.
Katika siku kama ya leo miaka 151 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Mirza Abu Abdillah, Sheikhul-Islami Zanjani, msomi mkubwa na mshairi wa Kiislamu. Msomi huyo mkubwa, alizaliwa mwaka 1224 Hijiria huko Zanjani, moja ya miji ya Iran na kuelekea Isfahani kwa ajili ya masomo akiwa kijana mdogo. Akiwa Isfahan, Ayatullah Mirza Abu Abdillah alipata kusoma katika hauza ya kielimu ambayo ilikuwa na itibari kubwa kielimu wakati huo. Baada ya kuhitimu masomo yake alirejea eneo alikozaliwa na kujishughulisha na kulea na kuto elimu kwa wanafanzu wake. msomi huyo ameandika vitabu kadhaa vikiwemo vya 'Hujjatul-Abraar' na 'Hidaayatul-Muttaqin'.

Katika siku kama ya leo miaka 118 aliaga dunia Herbert Spencer mwanafikra na mwanafilosofia wa Kiingereza. Spencer alizaliwa mwaka 1820 Miladia na kujifunza elimu mbalimbali kutoka kwa baba yake. Aidha alijiongezea ujuzi wa kielimu kutokana na juhudi zake za kupenda kutalii mambo. Herbert Spencer aliamini kuwa, mtu anaweza kujipatia elimu kwa kushuhudia na kupata uzoefu.
Miaka 107 iliyopita katika siku kama ya leo, yalijiri mapigano ya baharini ya Falklands pambizoni mwa visiwa vya Falklands katika bahari ya Atlantic kati ya Uingereza na Ujerumani. Vikosi vya wanamaji vya Ujerumani vilipigwa vibaya na vile vya Uingereza na kupelekea visiwa hivyo kwa mara nyingine tena kuwa chini ya himaya ya Waingereza.

Siku kama ya leo miaka 106 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Sayyid Ismail Sadr, alimu na mujtahidi wa ngazi ya juu mjini Kadhimiya, Iraq. Alisoma masomo ya awali ya dini ya Kiislamu kwa kaka yake na kisha akaelekea mjini Najaf, Iraq kwa ajili ya kujiendeleza zaidi katika uwanja huo. Akiwa mjini Najaf alijifunza elimu ya sheria za Kiislamu (fiqhi), elimu ya akhlaq na elimu nyingine tofauti za kidini. Baada ya kufariki dunia mwalimu wake mkubwa Ayatullah Mirza Shirazi, Ayatullah Sayyid Ismail Sadr alichukua jukumu la ufundishaji mjini Karbala nchini humo.
Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita, Chian Kai-shek kiongozi wa wapigania uhuru wa China alikimbilia Taiwan akiwa na wafuasi wake wengi baada ya kushindwa na wapiganaji wa chama cha Kikomonisti chini ya uongozi wa Mao Tse Tung na kuunda serikali ya kitaifa ya Uchina. Uungaji mkono wa Marekani kwa kiongozi huyo wakati huo ulipelekea Taiwan kujitenga na Uchina na kiti cha nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama kikapatiwa Taiwan.
Na katika siku kama ya leo miaka 22 iliyopita sawa na tarehe 17 Azar 1378 Hijria Shamsia aliaga dunia Husseini Makki mwanasiasa, mwanahistoria na mwandishi wa zama hizi wa Iran. Hussein Makki alizaliwa mwaka 1290 Hijria Shamsia. Baada ya kukamilisha masomo ya utangulizi alielekea katika mji wa Tehran na kuanza kufanya kazi serikalini. Baada ya mwaka 1320 Hijria Shamsia kupatina anga ya wazi ya kisiasa alianza rasmi harakati zake katika magazeti. Maandishi ya Husseini Makki ya kihistoria, kiutafiti na kifasihi yalikuwa sehemu muhimu ya makala katika magezeti mashuhuri ya Tehran zama hizo. Kujiunga kwake na Chama cha Iran na Chama cha Demokrasi cha Iran ndio uliokuwa mwanzo wa safari yake ya kuelekea katika harakati za kisiasa ambapo aliwahi kushika wadhifa wa Bunge katika duru tatu mtawalia.