Dec 13, 2021 01:04 UTC
  • Jumatatu tarehe 13 Disemba 2021

Leo ni Jumatatu tarehe 8 Jamadil Awwal 1443 Hijria sawa na Disemba 13 mwaka 2021.

Miaka 127 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo, alifariki dunia mmoja wa maraaji' wakubwa wa Kiislamu Ayatullah Mirza Habibullah Rashti. Katika uhai wake alielekea mjini Najaf Iraq kwa ajili ya masomo ya dini na kuhudhuria masomo ya Sheikh Murtadha Ansari. Ayatullah Mirza Habibullai Rashti taratibu akawa mmoja wa maraaji' wakubwa katika mji mtakatifu wa Najaf. Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na kitabu kiitwacho "Badaiul Afkar.

Ayatullah Mirza Habibullahi Rashti

Siku kama ya leo miaka 120 iliyopita aliaga dunia Sheikh Muhammad Abduh ambaye alikuwa miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa Kiislamu katika mji wa Alexandria nchini Misri. Alipata elimu katika Chuo Kikuu cha al Azhar na kisha akahudhuria darsa za Jamaluddin Asadabadi, mwanazuoni aliyepigania uhuru wa nchi za Kiislamu. Baada ya kupelekwa uhamishoni Sayyid Jamaluddin, Sheikh Muhammad Abduh alichukua nafasi yake ya kufundisha na kutoa elimu kwa wanazuoni na wanafikra za Kiislamu. Hata hivyo Sheikh Abduh alibaidishiwa nchini Syria baada ya satuwa ya wakoloni wa Kiingereza kuenea nchini Misri. Baada ya kufunza kwa kipindi cha miaka sita nchini Syria alihamia Paris na kusaidiana na Sayyid Jamaluddin Asadabadi katika kuchapisha gazeti la al Uruwatul Wuthqaa.

Sheikh Muhammad Abduh

Katika siku kama ya leo miaka 96 iliyopita, Majlisi ya Waasisi nchini Iran ambayo iliundwa kwa ajili ya kuhamisha mfumo wa kisultani kutoka silsila ya Qajar hadi utawala wa kifalme wa Pahlavi, ilitekeleza kazi yake kwa kufanya mabadiliko ya kimsingi katika Katiba ya Iran. Kwa msingi huo utawala wa miaka 153 wa wafalme wa Kiqajari nchini Iran ulifikia kikomo na badala yake ukaanza utawala wa miaka 53 wa Pahlavi hapa nchini. 

Majlisi ya Waasisi

Katika siku kama ya leo miaka 58 iliyopita, Sheikh Mahmud Shaltut Mkuu wa Chuo Kikuu cha Al Azhar na Mufti Mkuu wa Misri aliaga dunia. Mwanazuoni huyu mkubwa alizaliwa mwaka 1892 nchini Misri. Akiwa na umri wa miaka 14 alianza masomo ya shule ya upili katika chuo cha kidini cha Alexandria kilichokuwa tawi la Al Azhar. Alipata chetu cha chuo kikuu mwaka 1918 na kuanza kufunza katika chuo hicho na alihamia Chuo Kikuu cha al Azhar mwaka 1927. Alizidi kupanda cheo kieleimu na kuteuliwa kuwa mwanachama wa Baraza la Fatwa chuoni hapo. Mwaka 1958 aliteuliwa kuwa mkuu wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Al Azhar ambapo alitoa huduma kubwa. Kati ya hatua muhimu za Sheikh Shaltut katika kipindi cha uongozi wake ni jitihada za kuimarisha umoja na mshikamano baina ya madhehebu za Kiislamu. Baada ya kuandikiana barua kadhaa na Ayatulahil Udhma Borujerdi, marjaa mkubwa wa Kishia, Sheikh Shaltut alitambua rasmi Madhehebu ya Shia Ithnaashari kuwa ni moja ya madhehebu kubwa za Kiislamu na akatenga kiti maalumu cha kufundisha madhehebu hiyo katika Chuo Kikuu cha al Azhar. Vilevile alitoa fatwa mashuhuri akisema kuwa inajuzu kwa Mwislamu atakaye, kufuata Madhehebu ya Shia Jaafariya. Sheikh Shaltut aliaga dunia mwaka 1963 akiwa na umri wa miaka 72.

Sheikh Mahmud Shaltut

Katika siku kama ya leo miaka 18 iliyopita, Saddam Hussein, dikteta wa zamani wa Iraq alitiwa mbaroni akiwa katika maficho yake karibu na Tikrit huko kaskazini mwa Baghdad. Saddam alijificha katika eneo hilo baada ya Iraq kuvamiwa na majeshi ya Marekani na Uingereza mwezi Machi 2003. Kutiwa nguvuni dikteta huyo wa Iraq aliyemwaga damu za raia wengi wa nchi hiyo kuliwafurahisha sana Wairaki na nchi kama vile Iran na Kuwait ambazo zimepatwa na maafa makubwa kutokana na udhalimu za Saddam Hussein dhidi ya nchi hizo. Katika upande mwingine, pamoja na kuwa walimwengu walikuwa wakisubiri kwa hamu kusikia jinai zilizotendwa na dikteta huyo wa zamani wa Iraq wakati wa utawala wake, Marekani ilimweka dikteta huyo chini ya uangalizi wake baada ya kumtia nguvuni lengo likiwa ni kuzuia kufichuliwa ushirikiano wa karibu uliokuwapo kati ya dikteta huyo na serikali za Magharibi khususan ikulu ya Rais wa Marekani, White House.

Saddam Hussein akiwa mahakamani