Jumapili, tarehe 17 Aprili, 2022
Leo ni Jumapili tarehe 15 Ramadhani 1443 Hijria sawa na Aprili 17 mwaka 2022.
Siku kama ya leo miaka 1440 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alizaliwa Imam Hassan al-Mujtaba (as), mmoja wa Ahlul-Bait wa Mtukufu Mtume (saw). Imam Hassan (as) alikulia chini ya malezi na usimamizi wa Mtume, Bibi Fatma Zahra, binti wa Mtume, na Imam Ali bin Abi Twalib (as). Baada ya kuuawa shahidi baba yake yaani Imam Ali hapo mwaka wa 40 Hijria, mtukufu huyo alifanya kazi kubwa ya kusimamia na kuwaongoza Waislamu. Mwanzoni Waislamu wengi walimbai na kumpa mkono wa utiifu Imam Hassan, lakini mfumo wa utawala wa Bani Umayyah uliokuwa ukiongozwa na Muawiya mwana wa Abu Sufiyan ambao wakati huo ulikuwa na nguvu kubwa, ulianzisha uadui na chuki dhidi ya Imam huyo. Hatimaye Imam Hassan (as) alijiandaa kukabiliana na utawala dhalimu wa Bani Umayyah, lakini viongozi wengi wa jeshi lake walidanganyika na ahadi za uongo za maadui na kumuacha peke yake, hali iliyomlazimu mtukufu huyo kufanya suluhu na mtawala huyo wa Bani Umayyah kwa lengo la kuhifadhi dini tukufu ya Kiislamu.
Siku kama ya leo miaka 107 iliyopita, sawa na tarehe 17 Aprili 1915, kwa mara ya kwanza kabisa duniani ilitumiwa gesi ya kubana pumzi ya wanadamu vitani. Hatua hiyo ya kinyama ilichukuliwa katika Vita vya Kwanza vya Dunia. Ujerumani ilitumia gesi hiyo ya kubana pumzi dhidi ya askari wa Uingereza na Ufaransa na kuua askari wengi wa vikosi vya Waitifaki. Wajerumani walipata ushindi katika vita hivyo vilivyokuwa mashuhuri kwa jina la Vita vya Gesi.
Siku kama ya leo miaka 96 iliyopita, raia wa Scotland kwa jina la John Logie Baird, alifanikiwa kuvumbua televisheni ambayo hii leo imekuwa na umuhimu mkubwa katika upashaji habari duniani. Baird alikuwa mmoja wa wavumbuzi wakubwa wa enzi zake. Baada ya hapo mtu wa kwanza kutengeneza televisheni iliyoimarika zaidi alikuwa Giovanni Caselli, raia wa Italia ambaye mnamo mwaka 1862 alifanikiwa kutengeza chombo ambacho kwa kutumia mfumo wa telegrafi, kiliweza kutoa ramani na picha. Televisheni ya kwanza ambayo ilionyesha vizuri picha, ilianza kutumika tarehe 17 mwezi Aprili mwaka 1926 kwa ajili ya klabu ya kifalme nchini Uingereza.
Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita inayosadifiana na tarehe 17 Aprili 1946, Syria ilijipatia uhuru wake kutoka kwa askari wa kigeni waliokuwa wakiitawala nchi hiyo. Syria na baadhi ya ardhi zinazoizunguka awali ilikuwa ikijulikana kwa jina la Sham, na kabla ya kudhihiri dini tukufu ya Kiislamu ilikuwa chini ya udhibiti wa Iran, Ugiriki, Misri na Rome. Ardhi hiyo ilikuwa makao ya utawala wa Ugiriki na baada ya kukaliwa kwa mabavu na Misri, baadaye ilichukuliwa na utawala wa Othmaniya. Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia na baada ya kuporomoka utawala wa Othmaniya, Syria ilikoloniwa na Ufaransa. Kufikia Juni 1941, wakati wa vita vya pili vya dunia, askari wa Uingereza na Ufaransa waliikalia kwa mabavu nchi hiyo, hadi kufikia mwaka 1946 wakati ilipojipatia uhuru wake.
Siku kama ya leo miaka 18 iliyopita, mwafaka na tarehe 17 Aprili 2004, vifaru vya utawala wa Kizayuni wa Israel vilishambulia gari lililokuwa limembeba Dakta Abdulaziz Rantisi, mwanaharakati wa Palestina na kiongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas, na kumuuwa shahidi. Dakta Rantisi alichaguliwa kuiongoza harakati ya Hamas baada ya kuuawa shahidi Sheikh Ahmad Yassin mwasisi na kiongozi wa harakati hiyo. Rantisi alizaliwa mwaka 1964 katika mji wa Yafa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na alihitimu elimu ya tiba kama daktari katika chuo kikuu cha Alexandria nchini Misri.