May 02, 2022 22:17 UTC
  • Jumanne tarehe 3 Mei mwaka 2022

Leo ni Jumanne tarehe Mosi mfunguo Mosi Shawwal 1443 Hijria sawa na Mei 3 mwaka 2022.

Leo ni tarehe Mosi Shawwal inayosadifiana na Idi tukufu ya al-Fitr. Idul Fitri ni miongoni mwa sikukuu kubwa katika dini tukufu ya Kiislamu. Baada ya kukamilisha ibada ya funga, kuomba na kujipinda kwa ibada katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, Waislamu hufanya sherehe katika siku hii kubwa wakimshukuru Mola Manani kwa kuwawezesha kukamilisha ibada huyo. Iddi al Fitr ni kuuaga mwezi mtukufu wa Ramadhani ambao ni mwezi wa ibada na kujisafisha. Katika siku kama hii ya leo ni haramu kufunga saumu yoyote na Waislamu baada ya juhudi za mwezi mzima za kupambana na nafsi na kuchuma matunda ya ucha-Mungu hukusanyika pamoja na kusali Sala ya Iddul Fitr. Kuhusiana na utukufu wa siku hii Mtukufu Mtume (saw) anasema: "Mtu yeyote atakayemuasi Mwenyezi Mungu katika siku ya Idi, basi ni kama mtu aliyemuasi Mwenyezi Mungu siku ya miadi, yaani Siku ya Kiama." Kwa mnasaba wa siku hii adhimu, Redio Tehran inatoa mkono wa pongezi, heri na fanaka kwa Waislamu wote duniani.

Siku kama ya leo miaka 1190 iliyopita yaani tarehe Mosi Shawwal mwaka 253, Hijria alifariki dunia mpokezi mashuhuri wa Hadithi wa Ahlusunna, Imam Muhammad Ismail Bukhari. Abu Abdullah Muhammad Ismail aliyekuwa mashuhuri kwa jina la Imam Bukhari ni miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa Hadithi wanaoaminiwa na Ahlusunna. Alisafiri sana kwa ajili ya kutafuta Hadithi za Mtume (saw). Kitabu mashuhuri zaidi cha mwanazuoni huyo ni kile cha ‘Jamius Swahih’ maarufu kama Sahihi Bukhari. Vitabu vingine mashuhuri vya mwanazuoni huyo ni ‘Al-Adabul Mufrad’, ‘Al-Jaamiul-Kabiir’ na ‘Tarikhul-Kabir an Taraajam Rijaal-Sanad.’

Bukhari

Siku kama ya leo miaka 874 iliyopita, sawa na tarehe Mosi Shawwal mwaka 569 Hijiria alifariki dunia Said Bin Mubarak maarufu kwa jina la Ibn Dahhan, mfasiri, mwanafasihi na malenga wa Kiislamu. Ibn Dahhan alizaliwa mjini Baghdad na baada ya kumaliza masomo yake ya awali, alianza kusoma lugha sambamba na kupokea hadithi kutoka kwa wanazuoni wakubwa wa zama zake. Mtaalamu huyo mkubwa wa lugha alitilia maanani taaluma ya fasihi hususan katika kusoma mashairi na hivyo kuwa mfano wa kuigwa na wanafunzi wake katika usomaji mashairi. Aidha alilipa umuhimu mkubwa suala la kuhuisha baadhi ya vitabu vilivyosahaulika kiasi kwamba mwishoni alipoteza uwezo wake wa kuona katika kazi hiyo.

Miaka 837 iliyopita katika siku kama hii ya leo ya tarehe Mosi Shawwal alifariki dunia Abu Abdallah Muhammad bin Omar Razi mashuhuri kwa jina la Fakhrurazi msomi na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu. Alizaliwa katika mji wa Rey jirani na Tehran na alifanikiwa kwa haraka kujifunza elimu mbalimbali za Kiislamu kama Fiqihi, Tafsiri, Falsafa na Mantiki kutokana na kipaji kikubwa alichokuwa nacho. Mwanazuoni huyo ameandika vitabu vingi. Miongoni mwa vitabu vya Fakhrurazi ni Sherh Nahaj al-Balagha, Nihayat al-Uquul wa Siraj al-Quluub.

Abu Abdallah Muhammad bin Omar Razi

Leo ni Siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo vya Habari. Maadhimisho haya yanalenga kulinda na kutetea uhuru wa vyombo vya habari na kuwaenzi wadau wa sekta hiyo ambao wakati mwingine wanahatarisha maisha yao wakitekeleza wajibu na majukumu yao.

Siku hiyo iliainishwa kutokana na pendekezo lililotolewa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO). Hii leo uhuru wa vyombo vya habari unabinywa na kukandamizwa na baadhi ya tawala za kidikteta na kimabavu zisizopenda kuona ukweli ukiwafikia watu. Katika upande mwingine uhuru wa vyombo vya habari unatumiwa vibaya na baadhi ya nchi hususan za Magharibi kutangaza kila kitu, makala, picha na filamu chafu na zinazokiuka maadili ya kibinadamu. Mwenendo huo umekwenda mbali zaidi kiasi cha kutumiwa uhuru wa vyombo vya habari kwa ajili ya kuvunjia heshima matukufu ya kidini ya mabilioni ya watu kote duniani.

Siku kama ya leo miaka 593 iliyopita, Jeanne d'Arc alianzisha harakati ya kihistoria ya kuzikomboa baadhi ya ardhi za Ufaransa zilizokuwa zikikaliwa kwa mabavu na Uingereza. Jeanne d'Arc alikuwa kamanda wa jeshi ambaye alipewa jukumu na Mfalme wa Ufaransa la kuongoza mapambano dhidi ya majeshi ya Uingereza yaliyolikalia kwa mabavu eneo la kaskazini mwa Ufaransa. Hatimaye Kamanda huyo alikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kimaonyesho nchini Uingereza kwa tuhuma za kuritadi na kuacha dini na mwaka 1431, aliuawa kwa kuchomwa moto akiwa hai. 

Jeanne d'Arc

Siku kama ya leo miaka 553 iliyopita alizaliwa Niccolò di Bernardo dei Machiavelli, mwanahistoria na mwanasiasa wa Italia katika mji wa Florence. Sambamba na shughuli zake za kisiasa, Machiavelli aliandika pia historia ya Florence. Katika mtazamo wa kisiasa, Machiavelli alikuwa akiamini kwamba yawezekana kutumia wenzo wowote ule kwa ajili ya kupata madaraka na kwa ajili ya kuyalinda, na kwamba hakuna udharura wowote wa kuheshimu misingi ya maadili katika masuala kama hayo. Miongoni mwa kazi za mwanahistoria na mwanasiasa huyo wa Italia ni "The Art of War" na "The Prince."

Niccolò di Bernardo dei Machiavelli

Katika siku kama ya leo miaka 528 iliyopita, sawa na tarehe 3 Mei 1494 Miladia, Christopher Columbus, baharia wa Uhispania aligundua nchi ya Jamaica, huko Amerika ya Kati katika safari yake ya pili ya uvumbuzi ndani ya bara la Amerika. Licha ya tabia ya upendo na maridhiano ya wakazi asilia wa Jamaica na nchi nyingine zilizogunduliwa, lakini Christopher Columbus na watu wengine waliotumwa na Uhispania, waliwafanyia ukatili wenyeji hao wakazi. Kwa utaratibu huo Jamaica ambayo kutokana na nafasi yake muhimu ya kijografia na kwa kuwa na dhahabu nyingi zilizokuwa zikikodolewa macho na Uhispania, ilikoloniwa kuanzia mwaka 1509 Miladia hadi muda unaokaribia karne mbili. Baada ya Uhispiania nchi hiyo pia ilikoloniwa na Uingereza ambapo katika kipindi hicho akthari ya wakazi wake asilia walifukuzwa au kuuawa. Hatimaye nchi hiyo iliweza kujipatia uhuru wake mwaka 1962 Miladia.

Jamaica

Siku kama ya leo miaka 507 iliyopita yaani tarehe 3 Mei 1515 manowari za Ureno zilianza kushambulia kisiwa cha Hormuz cha Iran na hivyo kuanzisha wimbi la uingiliaji na ukoloni wa nchi za Magharibi katika eneo la Mashariki ya Kati. Kisiwa hicho kiko katika eneo la kiistratijia la lango la Hormuz lililoko katika Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman, kusini mwa Iran. Kutokana na kuwa Iran ilikuwa dhaifu katika upande wa jeshi la majini, wakoloni wa Kireno walivikalia kwa mabavu visiwa kadhaa vya Iran vilivyoko katika Ghuba ya Uajemi, ikiwemo Bahrain ambayo wakati huo ilikuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Hatua kwa hatua, Iran iliimarisha jeshi lake la majini, na mwaka 1652, iliweza kuvikomboa visiwa vyote vilivyokuwa vikikaliwa kwa mabavu na Wareno.

Siku kama ya leo miaka 215 iliyopita ulitiwa saini Mkataba wa Finckenstein kati ya Iran na Ufaransa wakati mfalme Napoleon wa Ufaransa alipokuwa katika vita na nchi nyingine za Ulaya. Kwa mujibu wa mkataba huo uliokuwa na vipengee 16, ilipangwa kuwa Iran ingepata silaha za aina mbalimbali kutoka Ufaransa kwa ajili ya kukabiliana na mashambulizi ya Warusi. Ufaransa pia iliahidi kutuma wataalamu wa mizinga na wahandisi wa masuala ya kijeshi nchini Iran kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa jeshi la nchi hiyo. Kwa upande wake, Iran iliahidi kukata uhusiano wake na Uingereza na kuisaidia Ufaransa katika kupeleka majeshi yake huko India.

Mkataba wa Finckenstein