Sibtain katika Qur'ani na Hadithi 11
Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Karibuni kusikiliza kipindi kingine katika mfulululizo wa vipindi hivi vya Sibtain katika Qur'an na Hadithi ambapo kwa leo tunaendelea kuzungumzia udharura wa kuwapenda Aali za Mtume wetu Mtukufu Muhammad (saw).
Kama tulivyowahi kuashiria katika kipindi kilichopita suala hili limesisitizwa kupitia Aya, Hadithi na mashairi mengi ya wasomi wa Kiislamu. Baadhi ya mashairi hayo ni yale yaliyotungwa na kusomwa na Washairi mashuhuri akiwemo Sheikh as-Sha'rani, mashairi ambayo yamenukuliwa pia na as-Shablanji as-Shafii' katika kitabu chake cha Nur al-Abswar. Bilas haka washairi hawa wamenufaika na maana ya Aya na Hadithi zinazozungumzia udharura wa kuwapenda Watu wa Nyumba ya Mtume (saw). Miongoni mwa Hadithi zilizopokelewa kuhusiana na suala hilo ni ile iliyopokelewa kutoka kwa Ibn Abbas kwamba Mtume (saw) alisema: 'Hakuna umma utakaofika mbele ya Mwenyezi Mungu Siku ya Kiama ukiwa mtukufu zaidi kuliko umma wangu, wala ahlu bait wowote watakaokuwa watukufu kuliko Ahlu Bait wangu, hivyo mwogopeni Mwenyezi Mungu kuwahusu.'
Hakuna shaka yoyote wapenzi wasikilizaji kwamba kila mtu aliye na roho safi na iliyo salama hupenda fadhila na utukufu, na upendo katika Mungu, kwa ajili ya Mungu na kwa watu wa Mungu ni moja ya sifa za watu wenye imani. Hivi ndivyo zinavyosema Hadithi zilizopokelewa kupitia madhehebu zote mbili za Kisuni na Kishia kutoka kwa Mtume Mtukufu (saw). Al-Muttaqi al-Hindi amendika katika kitabu chake cha Kanz al-Ummal kwamba Mtume (saw) alisema: 'Haamini mmoja wenu ila anipende zaidi kuliko nafsi yake, apende Ahli zangu kuliko ahli zake, watu wangu kuliko watu wake na kizazi changu kuliko kizazi chake.' Sheikh Swadouq vile vile ameandika katika kitabu chake cha Ilal as-Sharai' kwamba Mtume (saw) alisema: 'Mja hawi ni mwenye kuamini ila baada ya kunipenda mimi kuliko nafsi yake, kizazi changu kuliko kizazi chake, Ahlu Bait wangu kuliko ahlu bait wake na dhati yangu kuliko dhati yake.' Naye Shaikh Tabarsi ananukuu katika kitabu cha Mishkaat al-Anwar Hadithi ifuatayo kutoka kwa Mtume Mtukufu (saw): 'Mtu anayeruzukiwa na Mwenyezi Mungu kuwapenda Maimamu kutoka katika Ahlu Bait wangu, huwa amepata heri ya dunia na Akhera, hivyo asishuku kuwa yuko kwenye Pepo. Kuna sifa (heri/mambo mema) 20 katika kuwapenda Ahlu Bait wangu: Ishirini ni za humu duniani na ishirini nyingine ni za huko Akhera." Kisha Mtume akazibainisha zote hizo, hivyo heri kwa wale walio na sifa hizo.
*************
Huenda mtu akauliza, wasikilizaji wapenzi kwamba je, ni kwa nini Ahlul Bait hawa wa Mtume walizingatiwa na Mwenyezi Mungu kwa kiwango kikubwa kiasi cha kufanywa mapenzi juu yao kuwa malipo ya Mtume Mtukufu (saw) kutokana na juhudi kubwa alizofanya katika kuwafikishia wanadamu ujumbe wake wa mbinguni? Je, ni kwa nini Mtume alifanya mapenzi juu ya watukufu hao kuwa suala lenye umuhimu mkubwa na lililomshughulisha sana kiakili na kiroho katika ufikishaji wa ujumbe wake wa mbinguni kiasi cha kumfanya aseme: 'Mapenzi kwangu na kwa Ahlu Bait wangu ni yenye manufaa katika sehemu saba zilizo na hofu kubwa: Wakati wa kuaga dunia, kaburini, kufufuliwa, kuwasilishwa kitabu cha matendo, kuhesabiwa, wakati wa kupimwa matendo na kwenye Siraat (njia nyembamba).' Je, kuna siri gani kwenye jambo hilo?
Ndugu wasikilizaji, kuna majibu mengi sana ambayo yametolewa kuhusiana na suala hili. Moja ya majibu hayo ni kuwamba kuwapenda watukufu hawa wa Nyumba ya Mtume Mtukufu ni alama ya wazi ya kumpenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake (saw). La sivyo, ni vipi mtu atampenda Mwenyezi Mungu na kisha awachukie mawalii na wapendwa wake katika viumbe au ampende Mtume na kisha kuwachukia wapendwa wake? Je, atadai vipi kuamini utume wa Mtume (saw) ilihali anapinga watu walioshauriwa na Mtume mwenyewe wafuatwe kama viongozi wa umma wa Kiislamu baada ya yeye kuaga na kuondoka duniani?!
Mwanazuoni wa Kihanafi, Sheikh Sulaiman al-Qanduzi amenukuu katika kitabu chake cha Yanabiul Mawadda akinukuu kitabu cha Manaqib Ali cha Ibn al-Maghazili as-Shafi' Hadithi inayosema kwamba Mtume Mtukufu (saw) alimuhutubu Imam Ali (as) kwa kumwambia: "Ewe Ali! Mtu atakayekuua wewe atakuwa ameniua mimi, atakayekuchukia atakuwa amenichukia mimi na atakayekutusi atakuwa amenitusi mimi, kwa sababu wewe kwangu ni kama nafsi yangu. Moyo wako unatokana na moyo wangu na dongo lako linatokana na dongo langu. Mwenyezi Mungu Mtukufu aliniumba mimi na wewe kutokana na nuru yake na kuniteua (takasa/fadhilisha) mimi na kukuteua (takasa/fadhilisha) wewe na kisha kunichagua mimi kuwa Nabii na wewe kuwa Imamu. Hivyo atakayekanusha Uimamu wako atakuwa amekanusha Unabii wangu."
Ahlul Bait (as) wamefikia daraja ya juu zaidi kimaanawi mbele ya Mwenyezi Mungu kadiri kwamba ameshurutisha kukubaliwa amali za waja wake na kuwapenda Ahlul Bait hao pamoja na kuwafuata katika miongozo yao ya kidini. Suala hilo lina maana kwamba watukufu hawa (as) wanapasa kufuatwa na kutiiwa katika kila wanalolisema kama ambavyo Mtume Mtukufu (saw) ananukuliwa akisema: 'Hakika Mwenyezi Mungu aliwaumba Manabii kutokana na miti tofauti, na niliumbwa mimi na Ali kutokana na mti mmoja. Mimi ndio shina la mti huo, Ali ni tawi lake, Fatwimah mbegu yake, Hassan na Hussein matunda yake na Mashia wetu ni majani ya mti huo. Hivyo, yeyote atakayeshikamana na moja ya matawi hayo ataokoka na atakayeyaacha na kuyapuuza ataangamia. Hata kama mja atamwabudu Mwenyezi Mungu kati ya maeneo mawili ya Swafa na Marwa kwa muda wa miaka elfu moja na kisha akaongeza miaka mingine elfu moja hadi akawa mithili ya ngozi iliyokauka na kuwa kuukuu (chakaa), hali ya kuwa hatambui mapenzi yetu, Mwenyezi Mungu atavuta pua lake na kumtumbukiza motoni.' Kisha Mtume (saw) alisoma kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema: 'Sema: Kwa haya sikuombeni malipo yoyote kwenu ila mapenzi katika ndugu.'
************
Baada ya haya, wapenzi wasikilizaji mnaowapenda Ahlu Bait wa Mtume (saw), tumepata kufahamu malipo ya ulinganiaji wa ujumbe wa Uislamu, tumejua ni nani ndugu na wapendwa wa Mtume Mtukufu (saw) waliokusudiwa katika Aya ya Mawadda. Tumapata kufahamu vilevile nafasi yao adhimu (as) ambapo Mwenyezi Mungu amejaalia mapenzi juu yao kuwa malipo ya kazi na juhudi kubwa alizofanya Mtume (saw) katika kutufikishia ujumbe wa Uislamu, na hii ndio moja ya dalili na makusudio ya Aya ya Mawadda au Mapenzi.
Jambo jingine tunalolipata kwenye Aya hii ni kwamba mapenzi juu ya watu hao wa Nyumba ya Mtume (saw) ni jambo la dharura na wajibu wa kidini kwa sababu malipo yake ni ya wajibu. Hili, kama tulivyotangulia kusema katika vipindi vilivyopita, linatokana na fadhila na wema mkubwa aliotufanyia Mtume (saw) kutokana na machungu na mateso makubwa aliyoyapitia katika kutufikishia ujumbe wa dini tukufu ya Uislamu, na hivyo kutuokoa kutokana na giza la upotovu.
Dalili nyingine wapenzi wasikilizaji, inayotokana na Aya hii ni wajibu wa kutii na kutowapinga watukufu hawa wa Nyumba ya Mtume (saw), seuze kuwadhulumu, kuwapiga vita, kuwavunjia heshima na kuwaua kinyama. Ni wazi kuwa kuwapinga kunakinzana wazi na kuwapenda na hili ndilo jambo linalothibitishwa wazi na Allama Hilli katika kitabu chake cha Kashful Haq wa Nahju Swidq na vilevile katika kitabu chake kingine cha Minhajul Karama. Ama Ibn al-Batriq ameandika ifuatavyo katika kitabu chake cha Khaswais al-Wahy al-Mubeen: "Kuwapenda ni jambo ambalo limekwishathibiti kwa sababu hilo linatokana na amri ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, kama malipo ya ulinganiaji. Nayo ni sawa na wajibu wa mapenzi kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw). Hali ikiwa ni hivyo, ni wajibu kwa watukufu hao kutiiwa kama ilivyo wajibu kutiiwa Mtume (saw) na pia ni wajibu kufuata miongozo yao. Hawakuwajibikiwa hilo ila kutokana na ukweli kwamba wao ni sawa na nafsi ya Mtume (saw) kutokana na kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema: Watakaokuhoji katika haya baada ya kukufikia elimu hii waambie: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wanawake zetu na wanawake zenu, na sisi wenyewe na nyinyi wenyewe…… Na nafsi yake ni Ali, wanawake wake ni Fatwimah, na watoto wake ni Hassan na Hussein (as)."
Na kwa hayo wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya ksiwahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Ni matumaini yetu kuwa tumenufaika sote kwa pamoja na yale tuliyoyasikia katika kipindi cha leo. Basi hadi wakati mwingine panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.