Jun 22, 2022 07:50 UTC
  • Sibtain katika Qur'ani na Hadithi 12

Hamjambo wapenzi wasikilizi. Tuna furaha kujumuika nanyi tena katika sehemu hii ya 12 ya kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambacho kinakujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu inayokutangazieni kutoka mjini Tehran.

Bado tunaendelea kujadili fadhila za Imam Hassan na Hussein (as) zinazofafanuliwa na Aya za kitabu kitakatifu cha Mwenyezi Mungu ambayo ni Qur'ani Tukufu na Hadithi za Kiislamu ambazo zinakubaliwa na madhebu zote za Kiislamu. Ni wazi kuwa masuala yote tuliyoyajadili katika vipindi vilivyopita kuhusiana na Ahlul Bait wa Mtume (as) ni kwa msingi wa Hadithi zinazokubalika na pande zote mbili za madhehebu ya Shia na Suni. Baada ya hayo sasa tunajadili Aya nyingine mbili zinazofanana kuhusiana na fadhila za watukufu hawa ambazo zinapatikana katika Sura mbili tofauti za Qur'ani, ya kwanza ikiwa ni kauli ya Mwenyezi Mungu katika Aya za 43 na 44 za Surat an-Nahl zinazosema: Nasi hatukuwatuma kabla yako ila wanaume tuliowapa Wahyi (Ufunuo). Basi waulizeni wenye ukumbusho kama nyinyi hamjui. Kwa Ishara wazi na Vitabu. Nasi tumekuteremshia wewe Ukumbusho ili uwabainishie watu yaliyo teremshwa kwao, wapate kufikiri. Na Aya ya pili ni kauli yake Mwenyezi Mungu katika Aya ya 7 ya Sirat an-Anbiyaa inayosema: Na hatukuwatuma kabla yako ila wanaume tuliowapa Wahyi (Ufunuo). Basi waulizeni wenye kumbukumbu (elimu) ikiwa nyinyi hamjui.

Aya mbili hizi zinazofanana katika Sura mbili tofauti za Qur'ani Tukufu zinatufanya tusite kidogo na kutafakari juu ya mambo mawili muhimu. Jambo la kwanza ni kuwa ni kanuni na utaratibu wa watu wenye busara na hekima katika maisha yao yote, kuiga na kufuata miongozo ya mtu ambaye ni mjuzi, mwenye elimu na aliye na maarifa zaidi miongoni mwao ili pate kuwaongoza katika masuala muhimu yanayowahusu maishani. Kanuni hii ni kanuni ya mtu asiyejua jambo fulani kumrejea yule aliye na elimu na ujuzi wa jambo hilo, na Aya tulizotangulia kusoma zinasisitiza juu ya jambo hilo muhimu katika maisha ya mwanadamu. Baada ya kulifahamu suala hili wapenzi wasikilizaji, sasa swali hili linajitokeza hapa kwamba je, ni nani hawa wenye ukumbusho na elimu ambao wamezungumziwa na Aya mbili hizi tukufu? Kabla ya hilo, nini hasa maana ya elimu hapa? Tutayajibu maswali haya muhimu hivi pende.

***********

Ukumbusho katika kitabu kitakatifu cha Mwenyezi Mungu, yaani Qur'ani Takatifu, una maana kadhaa ikiwemo Qur'ani yenyewe. Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 9 ya Surat al-Hijr: Hakika Sisi ndio tulioteremsha Ukumbusho huu, na hakika Sisi ndio tutakaoulinda. Maana nyingine ya ukumbusho ni Mtume Mtukufu (saw) kama anavyosema Mwenyezi Mungu katika aya za 10 na 11 za Surat Talaaq: Hakika Mwenyezi Mungu amekuteremshieni Ukumbusho, Mtume anaye kusomeeni Aya za Mwenyezi Mungu zinazobainisha.

Wafasiri wa Qur'ani wanasema kwamba Mwenyezi Mungu alimwita Mtume wake hapa kuwa ni ukumbusho kutokana na kulingania kwake ukumbusho mwingine ambao ni Qur'ani Tukufu. Kwa kutegemea moja ya maana hizi kwamba ukumbusho ni ima Qur'ani au Mtume Mtukufu (saw), basi watu wa ukumbusho watakuwa ni akina nani? Je, watu hao si ni Watu wa Nyumba ya Mtume ambao nyumbani kwao ndiko kulikoteremshwa Wahyi na ujumbe wa Mwenyezi Mungu, nao ni Ali, Fatwimah, Hassan na Hussein na baada yao Maimamu wengine 9 watoharifu wanaotokana na kizazi cha Imam Hussein (as)?!

Nam wapenzi wasikiliza, watukufu hawa walizaliwa na kukulia katika nyumba ambayo ndani yake uliteremka Wahyi wa Mwenyezi Mungu na hivyo kuwa katika nafasi nzuri ya kuwa wao ndio waliofahamu zaidi mambo yaliyokuwa yakiendelea katika nyumba hiyo tukufu. Hivyo wao ndio walio katika nafasi nzuri zaidi ya kuulizwa na kufuatwa kuhusiana na masuala ya kidini na kimaanawi kuliko watu wengine wote.

Kwa kutegemea maana nyingine kuwa ukumbusho ni Mtume Muhammad al-Mustafa (saw), ni wazi kuwa watu hao wanajulikana wazi kama ilivyotubainikia kutokana na ufafanuzi wa Aya za Tat'hir na Qurba au Mawadda, nao ni Ali Amir al-Mu'mineen, Fatwimah, Mbora wa Wanawake Ulimwengu na Hassan na Hussein, Mabwana wa Vijana wa Peponi (as). Baada yao ni Maimamu wengine tisa watoharifu na waongozaji kwenye haki na wongofu kama walivyohesabiwa, kutajwa na kuarifishwa na babu yao mwenyewe Mtume Mtukufu (saw), kwa majina, lakabu na sifa zao maalumu kwamba wao ndio watakaokuwa makhalifa na wasii wake mtume na kwamba wa mwisho wao ni Mahdi Muahidiwa na Anayesubiriwa (af).

Huu ndio ukweli uliofikiwa na watafiti na wanazuoni wote wenye insafu, waadilifu na wanaotafuta ukweli kutoka madhehebu zote mbili za Kiislamu, yaani Shia na Suni. Ama ikiwa kuna baadhi ya watu wanaotaka kupata maarifa zaidi kuhusiana na suala hili, huenda marejeo bora zaidi yakawa ni Hadithi na Riwaya za kuaminika ambazo zimefanyiwa utafiti na kutegemewa na wajuzi wa Hadithi pamoja na wafasiri wa Qur'ani waliofafanua maana ya Aya hizi tunazozijadili. Tutalitazama jambo hilo hivi pundi, hivyo endeleeni kuwa nasi.

**********

Tabari amenukuu katika tafsiri yake ya Jamiul Bayaan na Qurtubi katika tafsiri yake pia, al-Hakim al-Askalani katika Shawahid Tanzil, Ibn Kathir katika Tafsiri al-Qur'ani al-Adhim, Tha'labi katika tafsiri yake ya al-Kashf wal Bayaan, al-Aluusi katika tafsiri yake ya Ruuh al-Maani na wengineo ambapo wanazuoni wote hawa wa Kisuni wanasema kwamba Imam Ali (as) alisema kuhusiana na Aya hii tukufu: 'Sisi ndio watu wa ukumbusho'. Amesema katika Hadithi nyingine: 'Wallahi sisi ndio watu wa ukumbusho.'

Wanazuoni hao hao wa Kisuni pia wamenukuu madhumuni na makusudio hayo hayo ya Aya hiyo ya Qur'ani kutoka kwa Imam Muhammad Baqir (as). Mwanazuoni wa Kihanafi as-Sheikh Sulaiman al-Qanduzi anasema katika kitabu chake cha Yanabiul Mawadda kwamba Imam Ja'ffar as-Swadiq (as) alisema: 'Ukumbusho una maana mbili: Qur'ani na Muhammad (saw), na sisi ndio makusudio ya maana zote mbili.'

Ama Riwaya za wanazuoni wa Kishia, wapenzi wasikilizaji, ni nyingi mno kuhusiana na suala hili. Sheikh al-Kulaini (MA) amenukuu nyingi ya Riwaya hizo katika kitabu chake cha al-Kafi. Moja ya Riwaya hizo ni ile inayomnukuu Mtume (saw) akisema: 'Ukumbusho ni mimi na Maimamu wa Ukumbusho. Nyingine ni ile ambayo inamnukuu Imam Swadiq (as) akisema: 'Ukumbusho ni Muhammad na sisi watu wa nyumba yake, viongozi.' Mtukufu huyu pia amenukuliwa akisema katika ufafanuzi wa kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema: Na hakika haya ni ukumbusho kwako na kwa kaumu yako. Na mtakujaulizwa, kwamba: 'Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) ndiye ukumbusho na Aali zake (as) ndio wasailiwa nao ni watu wa ukumbusho.'

Kuna watu waliomwambia Imam Baqir (as): 'Kuna watu miongoni mwetu wanaodai kuwa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu inayosema: Basi waulizeni wenye ukumbusho kama nyinyi hamjui, ni Mayahudi na Wakristo, naye (as) akajibu kwa kusema: Hivyo wanakuiteni kwenye dini yao! Kisha alinyanyua mkono wake na kuuweka kwenye kifua chake kitukufu na kusema: 'Sisi ndio watu wa ukumbusho na sisi ndio wasailiwa.'

Na hizo, wapenzi waumini, ni baadhi ya sifa za Imam Hassan na Hussein (as) ambao wasomi na historia imethibitisha wazi kwamba ni miongoni mwa watu wa ukumbusho, kwa sabau hawakuulizwa swali lolote katika nyanja yoyote ile nao wakawa wameshindwa kulijibu bali walibu kwa usahihi na ufasaha mkubwa maswali yote waliyoulizwa katika maisha yao yote. Hakuna hata swali moja waliloulizwa kuhusiana na jambo lolote nao wakawa wanasitasita au kushindwa kulijibu kwa njia iliyotatikana. Majibu yote waliyotoa kuhusiana na maswali na mijadala mbalimbali waliyoshiriki yalithibitisha wazi na bila kuacha shaka yoyote kwamba kweli wao ndio waliokuwa watu wa Qur'ani na Watu wa Nyumba ya Mtume, warithi, mawasii, makhalifa wake (saw) na ukumbusho ambao haupaswi kuulizwa watu wengine wasiofaa wala kustahiki kuulizwa maswali ya waja wa Mwenyezi Mungu.

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji, ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi kwa juma hili, ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuriya Kiislamu ikikutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapojaaliwa kukutana nanyi tena katika kipindi kijacho panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.