Sibtain katika Qur'ani na Hadithi 14
Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Ni matumaini yetu kwamba hamjamno na mko tayari kabisa kujiunga nasi kusikiliza sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambacho tunataraji kitatunufaisha sote kwa pamoja.
Baadhi ya wakati Qur'ani Tukufu hunasibisha matukio kwa Mwenyezi Mungu moja kwa moja ambaye ndiye msababishahi mkuu wa kila sababu na muumba wa kila sababu, na mara nyingine kunasibisha matukio hayo kwa sababu na visababishi vya kimaumbile ambavyo pia vimeumbwa na Mwenyezi Mungu na kufanywa kuwa sababu na njia ya wanadamu kuweza kumjua na kumfikia kimaanawi Mwenyezi Mungu. Hivyo, katika hali ambayo anatuamuru katika kitabu chake kitakatifu tushikamane naye moja kwa moja kwa mujibu wa kauli yake inayosema: Na shikamaneni na Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye Mlinzi wenu, Kiongozi bora kabisa, na Msaidizi bora kabisa, katika Aya ya 78 ya Surat al-Haj, wakati huohuo anasema katika Aya ya 103 ya Surat Aal Imran: Na shikamaneni na Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane.
Mifano ya aina hii, wapenzi wasikilizaji, ni mingi mno katika kitabu hiki kitakatifu, kwa sababu kimsingi na katika hatua ya mwanzo msaada unapasa kuwa ni wa Mwenyezi Mungu kabla ya jambo jingine au mtu mwingie yeyote. Kuna mifano mingi sana ambayo imetolewa na Manabii na Mitume wa Mwenyezi Mungu ikiwemo hii ya kauli ya Nabii Ya'qub (as) aliposema katika Aya ya 18 ya Surat Yusuf: Lakini subira ni njema; na Mwenyezi Mungu ndiye wa kuombwa msaada kwa haya mnayoyaeleza. Na kauli ya Mwenyezi Mungu alipokuwa akimzungumzia Mtume wake Muhammad al-Mustafa (saw) katika Aya ya 112 ya Surat al-Anbiyaa kwa kusema: Akasema: Mola wangu! Hukumu kwa haki. Na Mola wetu ni Mwingi wa Rehema, anayeombwa msaada juu ya mnayoyasifia. Na katika Sura tukufu ya al-Hamd, Mwenyezi Mungu anatufundisha Tauhidi ya matendo kwa kwa kusema: Wewe tu tunakuabudu, na Wewe tu tunakuomba msaada. Tunasoma Aya ya 45 ya Surat al-Baqara katika kitabu hicho hicho kitakatifu kauli yake Mwenyezi Mungu inayosema: Na tafuteni msaada kwa kusubiri na kwa kuswali; na kwa hakika jambo hilo ni gumu isipokuwa kwa wanyenyekevu.
Na hivi, ndugu wasikilizaji, ndivyo Waislamu wanavyosoma kila siku kitabu hiki kitakatifu cha Mwenyezi Mungu bila kuona mgongano wowote katika kauli zake hizi. Jambo hili bila shaka linatokana na ukweli kwamba msaada wa asili na wa kwanza ni wa Mwenyezi Mungu na kwamba misaada mingine yote inatokana na Yeye Muumba na kwamba misaada hiyo ni ya hatua ya pili inayokuwa na athari kutokana na idhini yake Mwenyezi Mungu. Misaada hiyo ya hatua ya pili ni njia ya ibada na maadili tu inayomuwezesha mwandamu kupata ridhaa ya Muumba wake. Kushimana na mambo mengine pia ni hivyo hivyo. Kwa maana kwamba asili katika mshikamano ni ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, yaani anayepaswa kushikamana naye kiasili ni Mwenyezi Mungu kambla ya jambo lolote jingine. Mambo mengine ambayo yameruhusiwa kushikamana nayo ni ya hatua ya pili na baada ya Mwenyezi Mungu kuyaridhia na kuwaruhusu wanadamu na waja wake kushikamana nayo. Mambo hayo yamebainishwa na kufafanuliwa kwa urefu na Mtume Mtukufu (saw) kupitia Hadithi nyingi mashuhuri zaidi kati yazo ikiwa ni ile ya Thaqalain, ambacho ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu (Qur'ani Tukufu) ambayo ni Kamba iliyoteremshwa ardhini kutoka mbinguni, na ambayo inaambatana na Aali watoharifu wa Mtume Mtukufu (saw). Wao ni sehemu ya Vizito viwili hivyo na ambao ndio wanaotarjumu na kukifasiri kwa njia sahihi Kizito hicho cha kwanza (Qur'ani Tukufu). Ni safina ya wokovu ambayo anayeipanda huwa ameokoka na anayeiacha hughiriki na kuangamia! Hii ni kwa sababu wao ndio kishiko madhubuti na kilicho imara.
*********
Ndugu wasikilizaji na watukufu, Aya ya Mwenyezi Mungu inayosema: Na shikamaneni na Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane, ni muhimu sana kwa sababu inabainisha vyema inakoanzia njia inayopaswa kufuatwa na waja na inakoelekea njia hiyo nyoofu inayomfikisha mwandamu kwenye ufanisi na mafanikio ya milele. Aya hii inabainisha vyema njia hiyo inayopaswa kufuatwa na Umma, na kuutaka ushikamane vilivyo na Kamba pamoja na sheria za Mwenyezi Mungu zinazowafikisha Kwake. Je, ni ipi Kamba hii inayozungumziwa na kukusudiwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu? Hii ni kutokana na ukweli kwamba Kamba hii ambayo Mwenye Mungu ametuamuru tushikamane nayo kikamilifu kwanza inamuokoa mwandamu na pili ni kuwa inamfikishia katika radhi za Mwenyezi Mungu. Je Kamba hii muhimu ya Mwenyezi Mungu ni ipi?
Ibn Hajar al-Haitami al-MakKi as-Shafii' anaandika katika kitabu chake cha Swawaiqul Muhriqa kwamba, mfasiri wa Qur'ani ath-Tha'labi ameandika katika kitabu chake cha al-Kashf wal Bayaan kuwa Imam Ja'ffar as-Swadiq (as) alisema kuhusiana na Aya hii: 'Sisi ndio hiyo Kamba ya Mwenyezi Mungu ambayo amesema kuhusiana nayo: Na shikamaneni na Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane.' Naye al-Hafidh al-Hasakani wa madhehebu ya Hanafi ananukuu maneno yanayofanana na haya katika Tafsiri yake ya Shawahid at-Tanzil Liqawaid at-Tafdhil kutoka kwa Imam Swadiq (as) anayesema: 'Sisi ndio hiyo Kamba ya Mwenyezi Mungu…..Anayeshikamana na Wilaya (uongozi) ya Ali bin Abi Talib huwa ameshikamana na wema. Hivyo anayeshikamana naye huwa ni muumini na anayemwacha huwa ametoka kwenye dini.'
Nam wapenzi wasikilizaji, ni wazi kuwa alama ya kuwa na imani ni kumtii Mwenyezi Mungu na kusalimu amri kwa moyo na kimatendo mbele ya maamrisho na makatazo yote ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, ikiwa ni pamoja na kushikamana vilivyo na Kamba yake, ambao ni Ahlu Bait wa Mtume wake (saw). Hili linathibiti vipi?
Al-Hakim al-Hasakani amenukuu Hadithi kutoka kwa Hussein bin Khalid, kutoka kwa Ali bin Musa ar-Ridha, kutoka kwa baba zake kutoka kwa Imam Ali bin Abi Talib (as) kwamba alisema: 'Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alisema: 'Anayetaka kupanda safina ya wokovu na kushikamana na kishiko madhubuti, na Kamba imara ya Mwenyezi Mung basi na amfanye Ali kuwa kiongozi wake na kuwafuata viongozi waongofu kutoka kizazi chake.'
Nam, katika kizazi chake ni Maimamu watoharifu wa kwanza wao akiwa ni Imam Hassan al-Mujtaba na wa pili ni Hussein, wajukuu na maua mawili ya Mtume (saw). Kisha baada yao ni Maimamu wengine tisa waongofu na wabarikiwa wanaotokana na kizazi cha Hussein, Bwana wa Vijana wa Peponi (as).
**********
Ndugu wasikilizaji, si Mashia pekee ndio waliofahamu na kutafsiri neno 'Kamba ya Mwenyezi Mungu' kuwa ni Maimamu wa haki na watoharifu kutoka katika Nyumba ya Mtume Mtukufu (saw) kutokana na Hadithi ya Mtume tuliyotangulia kuisoma kwenye kipindi hiki, bali maulama na wanazuoni wengi wa Kisuni wanakubaliana nao katika tafsiri na ufafanuzi wa Aya hii inayozungumzia Kamba ya Mwenyezi Mungu. Hii ni kwa sababu wametegemea Hadithi sahihi kuhusiana na suala hili, kadiri kwamba hakuna njia wala chaguo jingine ghairi ya kukubaliana na Hadithi hizi na kuzitegemea katika tafsiri na vitabu vya vyao vingine wanavyoviamini.
Kuhusu hili, ath-Tha'labi amethibitisha kwamba Ahlulu Bait wa Mtume Mtukufu (saw) ndio 'Kamba ya Mwenyezi Mungu' waliokusudiwa katika Aya tukufu ya 'Kamba ya Mwenyezi Mungu.' Ukweli huo umethibitishwa pia na Ibn as-Swibyaan al-Misri as-Shafii' katika kitabu chake cha Is'haaf ar-Raghibeen na as-Shablakhi as-Shafii' katika kitabu cha Nur al-Abswaar, al-Qunduzi al-Hanafi katika kitabu cha Yanabiul Mawadda na al-Hadhrami as-Shafii katika kitabu cha Rashfat as-Swadi min Bahri Fadhail Bani an-Nabii al-Hadi. Naye az-Zamakhshari as-Shafii' ananukuu katika Tafsiri yake ya al-Kashhaf Hadithi ambayo imepokelewa kutoka kwa Mtume Mtukufu (saw) kwamba alisema: 'Fatwimah ni damu ya moyo wangu (kitu bora na safi zaidi), wanawe ni matunda ya moyo wangu, mumewe nuru ya macho yangu na Maimamu wanaotokana na kizazi chake ni walinda amana (waaminifu) wa Mwenyezi Mungu, ni Kamba iliyoteremshwa kutoka Kwake kwenda kwa viumbe wake. Mtu anayeshikamana nao huokoka na anayewaacha huangamia.'
Kwa maelezo hayo, Qur'ani peke yake haimuokoi mwandamu bila ya kuunganishwa na kushikamanishwa na Mtume Mtukufu (saw) pamoja na Ahli zake watoharifu (as). Kwa msingi huo ni wazi kuwa ibada peke yake haitoshi kama haijashikamanishwa na Thaqalain, yaani Vitu Viwili Vizito (vyenye thamani kubwa) ambavyo ni Kirabu cha Mwenyezi Mungu, Qur'ani Tukufu na Aali za Mtume (saw). Aali hawa ndio aliousia wafuatwe kwa amri ya Mwenyezi Mungu, ni watukufu, makhalifa, wapendwa na mawalii wake, nao ni Ali Ameer al-Mu'minee, Bwana wa Maimamu Wabarikiwa, al-Hassan na al-Hussein na Maimamu wengine tisa maasumeena wanaotokana na kizazi cha Hussein (as). Tunatakiwa kushikamana, kufungamana, kuwapenda, kuwanusuru na kuwasaidia watukufu hawa barabara katika pande zote za kiimani, kimaadili na kielimu kama tunavyoamriwa kufanya na Mwenyezi Mungu mwenyewe na Mtume wake (saw) kama tulivyoona katika vipindi vilivyopita.
Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambacho kimekujieni kama kawaida kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ikikutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapojaliwa kuwa pamoja nanyi tena juma lijalo, tunakuageni kwa kusema Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.