Sibtain katika Qur'ani na Hadithi 15
Assalaam Alaikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Hii ni sehemu ya 15 ya kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambacho tunatumai mmejiweka tayari kukisikiliza.
Ndugu wasikilizaji, katika kipindi cha leo tunakusudia kujadili maana ya baadhi ya Aya zinazozungumzia udharura wa kushimakamana na Mwenyezi Mungu kama ilivyokuja katika moja ya Aya hizo ambayo ni Aya ya 101 ya Surat al-Imran inayosema: Na mwenye kushikamana na Mwenyezi Mungu basi huyo ameongozwa kwenye Njia Iliyo Nyooka.
Kama tunavyojua sote, Aya nyingi za Qur'ani huzungumzia mambo kwa ujumla tu na ni Hadithi ndizo huja na kuwabainisha Waislamu kwa undani mambo yanayokusudiwa na Aya hizo. Kuhusu hilo Hakim al-Askalani al-Hanafi anamnukuu sahaba mwema na mashuhuri wa Mtume (saw) Jabir bin Abdallah al-Answari akisema kuwa Mtume Mtukufu (saw) alisema: 'Hakika Mwenyezi Mungu alimjaalia Ali, mke wake na wanawe kuwa hoja yake kwa viumbe wake, nao ni milango ya elimu katika Umma wangu. Mtu anayewafuata, huongozwa kwenye njia iliyonyooka.'
Hivyo watukufu hao (as) ni sababu ya uongofu, na kushikamana na Mwenyezi Mungu kunalazimu kufuatwa watukufu hao.
Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 175 ya Surat an-Nisaa: Ama wale waliomwamini Mwenyezi Mungu, na wakashikamana naye, basi atawaingiza katika rehema yake na fadhila, na atawaongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka. Aya hii ni kati ya Aya zinazoaashiria mfungamano uliopo kati ya kufungamana na Mwenyezi Mungu na uongofu katika njia iliyo nyooka ambayo ni mashuhuri kuwa ni ufuataji wa miongozo na uongozi wa Muhammad na Aali zake (as). Miongozi mwa Aali hao ni Hasanaani, yaani Imam Hassan na Hussein (as) ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu ameamuru wafuatwe pamoja na kizazi chao (as) kwa kusema katika Aya ya 103 ya Surat al-Imran: Na shikamaneni na Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Je, kuna hoja na dalili gani juu ya suala hili?
***********
Sayyid Hasim al-Bahrani anamnukuu mwandishi wa kitabu cha al-Manaqib al-Fakhirati fi al-Itrati at-Twahira ambaye ni Abu Abdurahman Abdallah bin Ahmad bin Hambal, ambaye ananukuu Hadithi kutoka kwa Ibn Mubarak bin Masrur kutoka kwa Said bin Jubair kutoka kwa Abdallah bin Abbas akisema: Tulikuwa kwa Mtume (saw) alipofika hapo bedui mmoja na kusema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Nilikusikia ukisema: Na shikamaneni na Kamba ya Mwenyezi Mungu. Je, hii Kamba ya Mwenyezi Mungu tunayopasa kushikamana nayo ni ipi? Hapo Mtume (saw) akaupiga mkono wake kwenye mkono wa Ali na kusema: Shikamaneni na huyo kwani ndiye Kamba madhubuti.'
Kuna hadithi nyingine ndefu ambayo imepokelewa kutoka kwa swahaba mwema wa Mtume Jabir al-Answari (MA) ambaye anasema kwamba watu wa Yemen walifunga safari kwenda kuonana na Mtume (saw) kwani walikuwa na jambo walilotaka kumuuliza. Katika mazungumzo yao walimuuliza: 'Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ni nani wasii (atakayechukua uongozi wa Waislamu baada yako) wako? Mtume (saw) akajibu kwa kusema: Ni yule ambaye Mwenyezi Mungu ameamrisha watu wafungamane naye kwa kusema: Na shikamaneni na Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Wakasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Tubainishie Kamba hii ya Mwenyezi Mungu ni nini? Mtume (saw) akasema: Ni kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema: Isipokuwa wakishika kamba ya Mwenyezi Mungu na kamba ya watu (Aal Imran 112). Kisha alifafanua zaidi kwa kusema: Kamba ya Mwenyezi Mungu ni Kitabu chake na kamba ya watu ni Wasii wangu.'
Nam ndugu wasikilizaji, Aya na Hadithi tulizotangulia kuzisoma zimefafanua na kubainisha wazi Jadithi ya Thaqalain inayosema: 'Hakika nimekuachieni Vizito viwili ambavyo iwapo mtashikamana navyo barabara, hamtapotea kamwe baada yangu; Kitabu cha Mwenyezi Mungu ambayo ni Kamba iliyoteremshwa kutoka mbinguni hadi ardhini na kizazi changu, Ahlul Bait wangu….' Na Aya aliyoitolea dalili Mtume (saw) kuhusiana na suala hilo ni hii inayosema: Wamepigwa na udhalili popote wanapokutikana, isipokuwa wakishika kamba ya Mwenyezi Mungu na kamba ya watu.
Na jambo hili linatuthibitishia wazi wapenzi wasikilizaji kwamba, Mawasii wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), ndiyo hiyo Kamba ya Mwenyezi Mungu ambao tumeamrishwa kushikamana nao na kuwafuata, la sivyo, tutapigwa na udhalili popote pale tunapokutikana, na kustahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, na kupigwa na unyonge na udhalili, kama ilivyokuja mwishoni mwa Aya hiyo ya kushikamana na Kamba ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Ndugu wasikilizaji, kadhalika inathibiti kama tulivyosema mwanzoni kuwa Mawasii wa Mtume (saw), wakiwemo Hassan na Hussein (as), ndio Kizoto cha pili ambacho watu wanapasa kushikamana nacho pamoja na Kizito cha kwanza ambacho ni Kitabu kitakatifu cha Mwenyezi Mungu, la sivyo wanadamu watakumbwa na upotovu na hatimaye kutumbukia kwenye shimo refu la adhabu kali ya Mwenyezi Mungu.
**********
Na Ahlul Bait (as), ndugu wasikilizaji, wamesisitiza sehemu nyingi kuwa wao ndio ambao Mwenyezi Mungu aliwaamrisha waja wake wawafuate na kushikamana nao ili mtu asije akadai baadaye kwamba hakuna na habari ya hilo. Kuhusu hilo Imam Baqir (as) amenukuliwa katika Tafsiri ya al-Ayyashi akisema: 'Aali za Muhammad (as) ndio ile Kamba ambayo Mwenyezi Mungu aliwaamuru watu washikamane nayo.' Imam Swadiq (as) pia anasema: 'Sisi ndio Kamba ya Mwenyezi Mungu', akitolea hoja kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema: Na shikamaneni na Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane.
'Wala msifarikiane'……. Kwa nini Mwenyezi Mungu akatoa katazo hilo mpenzi msikilizaji? Imam Baqir (as) anatujibu kwa kusema: 'Hakika Mwenyezi Mungu alifahamu kuwa wangefarikiana baada ya kuondoka Mtume wao na kuhitilafiana. Hivyo aliwakataza kufarikiana kama alivyowakataza waliowatangulia na kuwaamrisha wakusanyike na kuwa kitu kimoja kwenye Wilaya ya Aali za Muhammad (saw) wala wasifarikiane.'
Nam, Wapenzi wasikilizaji, tunaona jinsi watu walivyopotea njia baada ya kukataa kushimkama na Imam Hassan al-Mujtaba (as) hadi kufikia kiwango cha kuwafuata watawala taghuti wa Bani Umayyia na vilevile walivyopotea njia na kupotoka baada ya kukataa kushikamana na Imam Hussein (as) kiasi cha kufikia hatua ya kumuua kinyama Imam wa zama zao na mjukuu huyo wa Mtume Mtukufu (saw), na badala yake kumkubali fasiki na ghasibu Yazid kuwa kiongozi wao. Hivyo Mwenyezi Mungu alighadhibishwa nao, akawapiga unyonge na udhalili na kuwaacha wapotee!
Nam wapenzi wasikilizaji, suala hili ni muhimu sana ambapo Mwenyezi Mungu anawataka waja wake washikamane kimamilifu na watu ambao watawaokoa baada ya kuwaongoza kwenye njia nyoofu. Ni wazi kuwa kushikamana huku kwanza kunahitajia kujitenga na maadui wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake (saw) na pili ni kuwafuata viongozi ambao waliteuliwa na Mwenyezi Mungu Mwenyewe ambao ni Mtume Muhammad (saw), pamoja na kizazi chake kitoharifu (as). Hoja yetu kuhusiana na suala hili ni Aya za Mwenyezi Mungu na Hadithi sahihi zilizopokelewa kutoka kwa viongozi hao wema na wateule wa Mwenyezi Mungu. Ama moja ya Aya hizo ni hii ya 256 ya Surat al-Baqarah inayosema: Basi anayemkataa Shet'ani na akamuamini Mwenyezi Mungu bila ya shaka amekamata kishikio madhubuti, kisichovunjika.
Ama kuhusu Hadithi ni ile iliyopokelewa kutoka kwa Mtume Mtukufu (saw) inayosema: 'Mtu anayetaka kukamata kishiko madhubuti cha Mwenyezi Mungu ambacho amekizungumzia katika Kitabu chake, basi na amfuate Ali bin Abi Talib na al-Hassan na al-Hussein kwa sababu hakika Mwenyezi Mungu anawapenda kutoka kwenye Arshi yake.'
Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji wa idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikikutangazieni kutoka hapa mjini Tehran. Basi hadi tutakapokutana tena Juma lijalo panapo majaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh.