Sibtain katika Qur'ani na Hadithi
Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Karibuni kusikiliza sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambacho bila shaka kitatunufaisha sote kwa njia moja au nyingine. Allahumma Swali Ala Muhammadin wa Aali Muhammad.
Moja ya sifa na fadhila kuu za Mtume Muhammad (saw) na Aali zake watoharifu (as) ni kuwa Mwenyezi Mungu mwenyewe na Malaika wake wote wanawaswalia watukufu hawa na kuwaamrisha waumini pia wawaswalie. Anasema katika Aya ya 56 ya Surat al-Ahzab ya kitabu chake kitakatifu cha Qur'ani: Hakika Mwenyezi Mungu na Malaika wake wanamswalia Nabii. Enyi mlioamini! Mswalieni na mumsalimu kwa salamu….. Allahumma Swali Ala Muhammadin wa Aali Muhammad. Hizo ni swala tatu wapenzi wasikilizaji. Swala ya kwanza ni ya Mwenyezi Mungu ambayo ni rehema na baraka kutoka kwake, ya pili ni ya Malaika, nayo ni ya utokaso unaotoka kwa MwenyezI Mungu Mtukufu kwenda kwa Mtume wake (saw) na swala ya tatu ni ya waumini ambao wameamrishwa na Mwenyezi Mungu kumswalia Mtume wao, kwa sababu wanaitikia wito wake (Mungu) na kutekeleza amri zake. Swala ya waumini ni dua yao kwa Mtume (saw). Maana ya swala yao hiyo ni kwamba wanathibitisha kwamba wangali wanalinda na kuheshimu mapatano na amana ambayo waliikubali walipopatiwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu: (Je, si mimi ni Mola wenu? Wakasema ndio). Hivyo kwa swala yao hiyo kwa Mtume na Aali zake, huwa wamesadikisha, kukiri, kuthibitisha na kusalimu amri kikweli mbele ya Mwenyezi Mungu juu ya yale aliyoyateremsha katika kitabu chake na kuyaweka kwenye sheria zake ambazo alimteremshia Mtume wake kupitia Wahyi. Baada ya kuaga na kuondoka duniani Mtume (saw), sheria hizo zilidumishwa na kuendelezwa na watukufu na warithi wake wa haki ambao waliusiwa kuchukua nafasi hiyo kwa amri ya Mwenyezi Mingu, wa kwanza wao akiwa ni Imam Ali bin Abi Talib, kisha al-Hassan na al-Hussein, na baadaye Maimamu wengine tisa maasumina waliotokana na kizazi cha Imam Hussein (as).
*********
Ni adhama na utukufu mkubwa ulioje huu, wapenzi wasikilizaji, kwa Mtume wetu Muhammad (saw), ambapo hata Mwenyezi Mungu mwenyewe pamoja na utukufu wote alionao, na Malaika wake, lakini wamemswalia na wangali wanamswali mtukufu huyo (saw). Mbali na hayo, waumini pia wameamrishwa wamswalie mtukufu huyo pamoja na Aali zake (as) kupitia kauli ya Mswalieni na mumsalimu kwa salamu….. Allahumma Swali Ala Muhammadin wa Aali Muhammad.
Kumsalimu kwa salamu hapa ni kwa moja kwa moja kwa maana kwamba siku aliyosema Mtume Mtukufu (saw): 'Yule ambaye mimi ni msimamizi wa mambo yake basi na Ali ni msimamizi wa mambo yake', ilikuwa ni amri ya Mwenyezi Mungu na hivyo Waislamu wote walipaswa kusalimu amri na kumfuata Imam Ali Amir al-Mu'mineen (as). Na siku ile Mtume (saw) alipowaainisha wajukuu wake al-Hassan na al-Hussein kuwa Maimu, Waislamu na waumini wote waliwajibika kutii amri hiyo na kusalimu amri. Kwa msingi huo, Imam Hassan al-Mujtaba (as) aliposimama kupambana na taghuti wa Sham Waislamu waliwajibika kusimama na kusaidiana naye dhidi ya taghuti huyo. Vilevile alipoamua kufanya suluhu na kulinda nafsi na damu ya Waislamu isimwagike bure walipasa pia kuheshimu uamuzi wake na kukubaliana naye katika hilo. Walipasa kufanya hivyo hivyo pia wakati Imam Hussein (as) ambaye ni Bwana wa Vijana wa Peponi, aliposimama kupambana na fasiki wa Sham, mkiukaji mkubwa wa sheria za Mwenyezi Mungu na ghasibu wa ukhalifa wa Mtume Muhammad (saw). Umma wa Kiislamu ulipaswa kusimama wote kusaidiana na Imam huyo dhidi ya fasiki huyo kwa sababu ndiye Imamu ambaye aliainishwa na kuteuliwa na Mtume kwa amri wa Mwenyezi Mungu na kuwataka Waislamu wote wamnusuru katika kila hali. Ni wazi kuwa kusalimu amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake kunalazimu kumnusuru mtu wanayependa na waliyemchagua kuongoza Umma wa Kiislamu. Bila shaka Mtume na Ahlu Bait wake (as) ndio nia ya saada na wongofu na ndio ile Kamba aliyoizungumzia Mwenyezi Mungu katika Aya ya 35 ya Surat al-Maida kwa kusema: Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na tafuteni njia ya kumfikia. Na tunawahutubu katika ziara ya Jamiatul al-Kabira kwa kusema: 'Nyinyi ndio njia kuu iliyonyooka, mashahidi wa dunia hii iliyo na mwisho na ponyo (waponyaji) la dunia ya kudumu milele, rehema inayofikisha kwenye kusudio, Aya iliyohifadhiwa, amana iliyolindwa na mlango uliofanywa kuwa mtihani kwa wanadamu. Kila anayekujieni huongoka na asiyekujieni huhiliki na kuangamia.'
***********
Na kuna Aya hii nyingine ya 28 katika Surat al-Hadid inayosema: Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na muaminini Mtume wake, atakupeni sehemu mbili katika rehema yake, na atakujaalieni muwe na nuru ya kwenda nayo. Baada ya kuamini na kuitakidi Umola wa Mwenyezi Mungu na utume wa Mtume wake, Muumini huwa amepata baraka kubwa kwa kuamini na kuwafuata Maimamu wa Nyumba ya Mtume (as). Ni kwa nini isiwe hivyo, hali ya kuwa kuna Aya nyingi zinazoashiria Uimamu huo na Hadithi nyingi za Mtume (saw) zinashiria na kusisitiza juu ya jambo hilo? Hivyo muumini anayeamini na kuitakidi maneno na ujumbe wa Mtume (saw) kuhusiana na ukhalifa wa Maimamu kumi na wawali, bila shaka huwa ni katika wale watu walioongoka na kufuata kikamilifu njia inayomridhisha Mwenyezi Mungu. Imam Baqir (as) anasema kuhusiana na maana ya ibara ya: Na atakujaalieni muwe na nuru ya kwenda nayo katika Aya tuliyotangulia kusoma kuwa ni: Imamu mnayemfuata.
Na katika Maimamu wa haki, wapenzi wasikilizaji, ni Maimamu al-Hassan na al-Hussein (as) ambao ni wajukuu, maua na makhalifa wawili wa Mtume (saw). Al-Hamawaini as-Shafi' anamnukuu Ibn Abbas katika kitabu chake cha Faraid as-Simtain kwamba Myahudi mmoja kwa jina la Na'thal alimuuliza Mtume (saw) kwa kusema: Hakuna Mtume ambaye hakuwa na mtu wa kumrithi, na Mtume wetu Musa bin Imran alirithiwa na Yushua bin Nun. Hivyo twambie mrithi wako unayemuusia akurithi ni nani? Mtume (saw) akamjibu kwa kumwambia: Hakika wasii (mrithi) wangu ni Ali bin Abi Talib, kisha baada yake ni wajukuu wangu al-Hassan na al-Hussein, ambapo watafuatwa na Maimamu tisa kutoka katika kizazi cha Hussein.'
Kuna Aya nyingine wapenzi wasikilizaji nayo ni Aya ya 32 ya Surat al-Fatir inayosema: Kisha tumewarithisha Kitabu hao ambao tuliwateuwa miongoni mwa waja wetu. Kati yao yupo aliyejidhulumu nafsi yake, na yupo wa katikati, na yupo aliyetangulia katika mambo ya kheri, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo fadhila kuu.
Allama Tabatabai anasema katika Tafsiri yake ya al-Mizan kwamba maana ya Aya; Kisha tumewarithisha Kitabu hao ambao tuliwateuwa miongoni mwa waja wetu, ni baadhi ya watu wateule tu katika waja wake na sio waja wote kwa sababu, Kati yao yupo aliyejidhulumu nafsi yake, na yupo wa katikati, na yupo aliyetangulia katika mambo ya kheri…… Ama waja wateule walioteuliwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe kama inavyosema Aya hiyo tukufu ni wale walioarifishwa na Imam Swadiq (as) kwa kusema: 'Wao ni Aali za Muhammad (saw)…..' Vilevile wateule hao wamearifishwa na Mtume Mtukufu (saw) alipoulizwa na Yahudi Jandal bin Janada kwa kusema: Naomba unijulishe mawasii watakaokuja baada yako. Mtume akamjibu kama anavyonukuu al-Kanji as-Shafi' katika kitabu chake cha Kifayat at-Talib: Mawasii wangu ni kumi na wawili….. wa kwanza wao ni Bwana wa Mawasii na Baba wa Maimamu Ali, wanawe al-Hassan na al-Hussein.' Na kisha akawahesabu hadi kumfikia Imam Msubiriwa, al-Imam al-Mahdi (af).
Hao ndio mabwana wa viumbe walioteuliwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu baada ya kuwafadhilisha na kuwatakasa kati ya waja wake wote ili wapate kuwaongoza wanadamu katika yale yanayomridhisha Mweyezi Mungu na wapate kumtii na vilevile wawe ni viongozi wananaowaongoza waja wake katika yale anayoyataka Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji muda uliotengewa kipindi hiki ndio unafikia ukingoni. Ni matumaini yetu kwamba mmepata kunufaika vya kutosha na yale tuliokuandalieni katika kipindi cha leo kilichokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikikutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapokutana tena katika kipindi kingine, panapo majaaliwa yake Mola, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Alaykum Warahmatullahi wa Barakatuh.