Sibtain katika Qur'ani na Hadithi
Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Tunakukaribisheni katika kipindi kingine cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambapo bado tunaendelea kuzungumzia sifa na fadhila za Maimamu Hassan na Hussein (as), wajukuu na maua mawili ya Mtume Mtukufu (saw) kwa mujibu wa Aya za Qur'ani za na Hadithi.
Tukianza, tunasema kuwa kuna Aya nyingi sana, wapenzi wasikilizaji, yaani kwa makumi, zinazowazungumzia wajukuu wawili hawa wa Mtume Mtukufu (saw) kama inavyonukuliwa kutoka kwa Ibn Abbas. Tungependa kuashiria hapa Aya ifuatayo kuhusiana na suala hili. Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 34 ya Suratul Baqarah: Na vivyo hivyo tumekufanyeni muwe Umma wa wastani, ili muwe mashahidi juu ya watu wote, na Mtume awe ni shahidi juu yenu.
Kuhusiana na Aya hii tunatafuta maana yake kwa Aya hiyo hiyo yenyewe na pia kwa kutegemea Hadithi zinazoifafanua.
Salim bin Qais al-Hilali anamnukuu Imam Ali Amir al-Mu'mineen Ali (as) akisema: 'Mwenyezi Mungu alitukusudia sisi kwa kauli yake inayosema: ili muwe mashahidi juu ya watu wote. Hii ni kwa sababu Mtume wa MwenyezI Mungu (saw) ni shahidi kwetu sisi, na sisi ni mashahidi wa Mwenyezi Mungu juu ya viumbe wake na hoja Yake kwenye ardhi Yake. Na sisi ndio wale ambao Mwenyezi Mungu amesema juu yao: Na vivyo hivyo tumekufanyeni muwe Umma wa wastani.' Hadithi hii pia imenukuliwa na mwanazuoni wa Kihanafi, al-Hakim al-Hasakani katika kitabu chake cha Shawahid at-Tanzil Liqawaid at-Tafdhil
Miongoni mwa mambo aliyoyajadili Furat al-Kufi katika Tafsiri yake kuhusiana na maana ya Aya ni kauli ya Imam Ja'far as-Swadiq (as) akisema: 'Sisi ndio Umma wa wastani na mashahidi wa Mwenyezi Mungu Mtukufu juu ya viumbe wake na hoja katika ardhi yake.' Imam huyo huyo pia amenukuliwa sehemu nyingine akisema: 'Miongoni mwetu yupo shahidi katika kila zama: Ali bin Abi Talib katika zama zake, al-Hassan katika zama zake, al-Hussein katika zama zake na kila mmoja wetu anayeita katika njia ya Mwenyezi Mungu.'
Ushihidi mwingine ni ule uliotolewa na as-Swaffar al-Qumi katika kitabu chake cha Baswair ad-Darajaat kutoka kwa Imam Swadiq (as) akisema katika kufasiri Aya hiyo hiyo tukufu: 'Sisi ndio mashahidi juu ya watu wote katika kile walichonacho katika halali na haramu na kile walichopoteza (walichopuuza) katika hayo. Al-Kulaini pia amemnukuu Imam Swadiq (as) katika kitabu chake cha al-Kafi akisema: 'Sisi ndio Umma wa wastani na mashahidi wa Mwenyezi Mungu juu ya viumbe wake na hoja yake katika ardhi yake.
Na katika kupinga na kuwalalamikia wale waliojaribu kupotosha maana halisi ya Aya hii kwa wale waliokusudiwa na Mwenyezi Mungu, Al-Ayyashi anamnukuu Imam Swadiq (as) katika Tafsiri yake ya Al-Ayyashi akisema kuhusiana na maana ya 'Umma wa wastani' kuwa: 'Yaani Umma ambao uliwajibishiwa wito wa Ibrahim, 'Mmekuwa ni umma bora mliotolewa kwa watu,' nao ni umma wa wastani uliotolewa kwa watu. Imam huyo huyo (as) pia amenukuliwa katika kitabu cha al-Manaqib cha Ibn Shahr Ashub akifafanua maana inayofanana na hii tuliyoiashiria kuhusiana na Aya hii ya: Na vivyo hivyo tumekufanyeni muwe Umma wa wastani, ili muwe mashahidi juu ya watu wote, na Mtume awe ni shahidi juu yenu.
**********
Wapenzi wasikiliza, tunapata maana na maelekezo katika Ayah na Hadithi za Ahlul Bait wa Mtume Mtukufu (saw) ambayo yanaoana na kufungama moja kwa moja na mantiki na sheria za Mwenyezi Mungu, maelekezo ambayo yanasisitiza kwamba ni lazima kuwepo na mashahidi wake katika jamii ya mwanadamu, kama ambavyo mashahidi hao wanapasa kuwa watu wachache tu walioteuliwa na Mwenyezi Mungu juu ya viumbe wake, baada ya kuwapa wanadamu hao neema zote za humu duniani. Mungu amewateua mashahidi hao ili wapate kusimamia na kuwaongoza wanadamu kuelekea kwenye njia nyoofu ya Muumba wao. Miongoni mwa mashaidi hao watakatifu na wasiotenda dhambi ni Imam Hassan na Hussein (as) pamoja na vizazi vyao vitukufu (as).
Na hatimaye wapendwa wasikilizaji tunapasa kuzingatia hapa nuktaa hii muhimu kwamba istilahi ya Ahlul Bait wa Mtume (saw) inakusudiwa tu Mtume Muhammad, Ali, Fatwimah, Hassan na Huseini na baada yao Maimamu wengine tisa kutokana na kizazi chao kitoharifu kinachotokana na Imam Hussein (as). Lakini iwapo istilahi hiyo itatumika kuwahusu watu wanaofungamana moja kwa moja na Mtume (saw) na katika hali maalumu kama vile ya Hadithi Kisaa au Mubahala, basi watakaokuwa wanakusudiwa katika hali hiyo ni Amir Mu'mineena Ali (as), Fatwimat az-Zahraa (as) pamoja na wanao wao wawili al-Hassan na al-Hussein (as).
Jambo hili pia limeashiriwa na kusisitizwa na vyanzo vya wanazuoni wa Kisuni kabla ya kuzungumzia vyanzo vya Kishia katika vitabu vya Tafsiri, Hadithi, Sira na Historia.
Nukta nyingine muhimu na ya dharura ambayo tunapasa kuiashiria hapa ni kwamba Aya zote ambazo tumekusomeeni katika kipindi hiki na vipindi vingine vilivyopita zote zinasisitiza kwa uwazi mkubwa kwamba Ahlul Bait wa Mtume (as), wakiwemo Imam Hassan na Imam Hussein (as) wote ni maasumu kwa maana kuwa wamekingwa na kutenda dhambi na kwamba wao ni muendelezo wa Mtume Mtukufu (saw). Kwa maelezo hayo ni wazi kuwa kuwapenda na kuwatii ni jambo la lazima kwa Waislamu kwa kuwa wao ndio Kamba ya Mwenyezi Mungu ambayo Waislamu wanawajibika kushikamana nayo. Watukufu hao wameongozwa na kupata maelekezo ya mbinguni ili nao wapate kuwaongoza na kuwaelekeza wanadamu kwenye njia nyoofu.
Hivyo hongera na pongezi kwa wale wanaowafuata kiimani na kiitikadi, na heri kwa wale wanaowapenda, kuwatii na kushikamana nao na Mwenyezi Mungu kuwafisha wakiwa kwenye njia hiyo hiyo.
Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi chetu hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Bsi hadi tutakapojaaliwa kukutana tena katika kipindi kingine kama hiki siku na wakati kama huu wa leo, tunakuageni nyote tukitumai kuwa mmenufaika vya kutosha na yale yote mliyoyasikia katika kipindi hiki. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo, panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.