Sibtain katika Qur'ani na Hadithi
Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Hii ni sehemu ya 26 katika mfululizo wa vipindi hivi vya Sibtain ambavyo vinazungumzia fadhila na utukufu wa Maimamu wawili watukufu Hassan na Hussein (as) ambao ni wajukuu watoharifu wa Mtume Mtukufu (saw).
Katika Hadithi ambazo tumepata kuzizungumzia katika vipindi vilivyopita tumeaona kwamba wajukuu wawili hawa wa Mtume wametajwa moja kwa moja kuwa ni watoto wake ambapo Mwenyezi Mungu anathibitisha jambo hilo katika Aya tukufu ya Mubahala ambayo ni Aya ya 61 katika Surat Aal Imran ambayo inasema: Watakaokuhoji katika haya baada ya kukufikia elimu hii waambie: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wake zetu na wake zenu, na sisi wenyewe na nyinyi wenyewe, kisha tuombe kwa unyenyekevu tutake laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie waongo.
Hadithi na riwaya zote za historia ya Uislamu zinasema kwa sauti moja kwamba Mtume Mtukufu (saw) hakutoka kwenda kwenye tukio la Mubahala ambalo lilikuwa ni la kujadiliana kiitikadi na Wakristo wa Najran ila akiwa na mtoto wa ami yake na wasii wake Ali (as), Binti yake Fatwimatu az-Zahra (as), wajukuu wake Hassan na Hussein ambao ni watoto wa binti yake Fatwimah na mtoto wa Ami yake Ali (as).
Fakhr ar-Razi anasema katika Tafsiri ya Kabir chini ya Anwani 'Suala la Nne' kwamba: Hakika Aya hii inathibitisha kwamba Hassan na Hussein (as) walikuwa watoto wa Mtume (saw). Alipotaka aitiwe watoto wake, ni Hassan na Hussein ndio waliitwa na hivyo wawili hao wakachukuliwa kuwa watoto wake na jambo linalosisitiza ukweli huo ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Aya za 84 hadi n86 za Surat al-An'aam inayosema: Na hizo ndizo hoja zetu tulizompa Ibrahim kuhojiana na watu wake. Tunamnyanyua kwa vyeo tumtakaye. Hakika Mola wako ni Mwenye hikima na Mwenye ujuzi. Na tukamtunukia (Ibrahim) Is-haq na Yaakub. Kila mmoja wao tulimwongoa. Na Nuhu tulimwongoa kabla. Na katika kizazi chake tulimwongoa Daud na Suleiman na Ayyub na Yusuf na Musa na Harun. Na hivi ndivyo tunavyowalipa wanaofanya wema. Na Zakaria na Yahya na Isa na Ilyas. Wote walikuwa miongoni mwa watu wema. Na Ismail, na Al Yasaa, na Yunus, na Lut'. Na wote tuliwafadhilisha juu ya walimwengu wote.
Kwa dalili hiyo Fakhr Razi anasema: Ni wazi kuwa Isa (as) alinasibishwa kwa Ibrahim (as) kupitia mama yake na si kupitia baba, na hivyo kuthibiti ukweli kuwa mtoto wa binti anaweza kuitwa kuwa mtoto wa baba ya binti huyo.' Naye Ibn Hajar al-Makki as-Shafi' anasema katika kitabu cha as-Swawaiq al-Muhriqa kwamba: 'Fahamu kuwa, watoto wa Fatwimah na kizazi chao wanaitwa watoto (yaani watoto wa Mtume (saw)) nao wananasibishwa kwake kwa nasaba iliyo sahihi na yenye manufaa duniani na Akhera. Na anasema katika sehemu nyingine: Na wilaya ni dalili, nayo inathibitisha kwamba watoto wa mabinti huitwa kuwa ni watoto.'
Baada ya dalili hii thabiti unabainika wazi uongo na batili ya Bani Abbas waliopokonya na kughusubu haki ya ukhalifa kutoka kwa watu waliofaa na wastahiki wa ukhalifa huo, kudai kwamba watoto wa Fatwimah sio watoto wa Mtume (saw) bali ni watoto wa Ali (as) tu. Maneno haya ya batili yalikaririwa na kundi jingine lililowafuata ni kana kwamba lilikuwa limepofuka na kutojua yaliyoandikwa katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu na vile vile mambo yaliyokubaliwa na Waislamu wengine wote bila kujali Ushia wala Usuni wao.
Kuhusu hilo, Tabari as-Shafi' anaandika katika kitabu chake cha Dhakhairul Uqba fii Manaqib Dhawil Qurba kwamba: Mwenyezi Mungu aliposema: Watakaokuhoji katika haya baada ya kukufikia elimu hii waambie: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu….., Mtume (saw) aliwaita wanne hao yaani Ali, Fatwimah, Hassan na Hussein.' Naye Abu Said al-Khidri amenukuliwa akisema: Aya hii ilipoteremka, Mtume (saw) aliwaita Ali, Fatwimah, Hassan na Hussein na kisha akasema: 'Allahumma! Hawa ndio Ahlu Bait wangu.' Hadithi hii imenukuliwa na Muslim na pia Tirmidhi.
Al-khawarazmi ambaye ni Msuni wa madhehebu ya Hanafi ananukuu katika kitabu chake cha 'Maqtal Hussein' (as) Hadithi ambayo imepokelewa na Usama bin Zaid bin Haritha kwamba alisema: 'Nilienda kwa Mtume (saw) usiku mmoja kwa ajili ya kutekelezewa haja fulani. Mtume (saw) alitoka nyumbani kwake huku akiwa amebeba vitu fulani ambavyo sikuvijua mara moja. Nilipotimiziwa haja yangu, nilimuuliza Mtume: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Nini vitu hivi ulivyobeba? Baadaye ikafahamika kuwa vitu hivyo alivyokuwa amevibeba Mtume (saw) kwenye makwapa yake, walikuwa Imam Hassan na Hussein (as). Kisha akasema Mtume (saw): Wawili hawa ni wanangu na wana wa binti yangu. Akasema: Eeh Mwenyezi Mungu! Unafahamu kwamba ninawapenda watoto wawili hawa, hivyo naomba uwapende', au kama ilivyo katika riwaya nyingine: Basi mpende kila anayewapenda.'
Wapenzi wasikiliza, hali kadhalika al-Hafidh ad-Dimishki ibn Asakir ambaye ni mfuasi wa madhehebu ya Shafi' anasema kumuhusu Imam Hussein (as) katika kitabu chake cha Tarikh Madinat ad-Dimishk Kwamba Abdallah bin Omar bin al-Khattab alisema kuhusu Hassan na Hussein (as) kwamba walikuwa wakilishwa elimu kulishwa. Ibn Asakir ananukuu riwaya nyingine ambayo inaishia kwa mapokezi ya Mudrik bin Ammara kwamba alisema: 'Nilimwona Ibn Abbas akiwa amewashikia Hassan na Hussein kifaa cha kupandia ngamia (kipandio), watu wakamwambia: Je, unawashikia kifaa cha kupandia ngamia ilihali wewe ni mkubwa wao kiumri?! Akawajibu: Hawa ni watoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, je, si ni fahari kubwa kwangu mimi kuwashikia kifaa hicho?!
*******
Miongoni mwa fadhila na sifa za Maimamu Hassan na Hussein (as) ni kwamba walishabihiana na kufafa sana na babu yao Mtume Mtukufu (saw) ambaye ni kiumbe bora zaidi ulimwenguni. Jambo hilo liliwafanya wengi kuamini kwa dhati kuwa wawili hao walikuwa wana, wajukuu na warithi halisi wa Mtume (saw) kidini na kiitikadi.
Siku moja Abu Hanifa aliulizwa iwapo aliwahi kumwona Mtume akasema: Ndio, alikuwa akifanana sana na Hassan bin Ali. Naye Abdallah bin Zubair anasema: Mtu aliyefanana na kupendwa sana na Mtume kati ya Watu wa Nyumba yake ni Hassan bin Ali (sa).
Ndugu wasikilizaji, al-Mutaqqi al-Hindi anasema katika kitabu cha Kanz al-Ummal akimnukuu Imam Ali (as) kwamba Imam alisema: 'Anayetaka kumwona mtu anayeshabihiana zaidi na Mtume (saw) tokea shingoni hadi kwenye uso wake basi na amtazame Hassan bin Ali na anayetaka kuomwona anayeshabihiana zaidi na Mtume tokea shingoni hadi kwenye miguu yake kwa maumbile na rangi na amtazame Hussein bin Ali.'
Hiyo ndiyo hekima na busara ya Mwenyezi Mungu ambaye alifananisha na kushabihisha wajukuu wawili hao wa Mtume Mtukufu (saw) na babu yao huyo ili wapate kuwa tulizo, ukumbusho na ruwaza njema kwa Wasislamu na walimwengu kwa ujumla na vile vile kuwa sababu ya wao kumpenda (Mtume) kupitia watukufu hao (as).