Alkhamisi, 01 Septemba, 2022
Leo ni Alkhamisi Mwezi Nne Mfunguo Tano, Safar 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe Mosi Septemba 2022 Miladia.
Miaka 848 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe Mosi Septemba mwaka 1174, kazi ya ujenzi wa mnara maarufu wa Pisa uliopo katika mji wa Pisa nchini Italia ilianza. Lengo la kujengwa mnara huo lilikuwa ni kupachikwa saa kubwa juu yake. Lakini baada ya muda kupita tangu ulipoanza ujenzi wa mnara huo wenye urefu wa mita 57 kwenda juu, jengo hilo liliegama na kuinama kwa takriban mita tano kutoka mstari wa usawa na kwa sababu hiyo mnara wa Pisa umekuwa maarufu kwa jina la Mnara wa Pisa Ulioinama. Pamoja na hayo, kutokana na juhudi za wahandisi na wataalamu wa nchi mbalimbali, muegamo huo umerekebishwa kwa kiwango fulani.
Tarehe mosi Septemba 1923, tetemeko kubwa sana la ardhi la Kantō ambalo lilisababisha uharibifu mkubwa lilitokea nchini Japan katika kisiwa kikuu cha nchi hiyo cha Honshū. Watu zaidi ya 140,000 waliuawa kutokana na zilzala hiyo iliyokuwa na ukubwa wa 8.2 kwa kipimo cha rishta. Mtetemeko huo ulikuwa mkubwa kiasi kwamba mtikisiko wake ulihisika katika maeneo kadhaa ya miji ya Tokyo na Yokohama. Mbali na maafa makubwa yaliyosababishwa na tetemeko hilo, watu wengi sana nchini Japan walibaki bila makazi kutokana na nyumba nyingi kubomolewa na kuteketea kwa moto.
Siku kama ya leo miaka 85 iliyopita, yaani tarehe Mosi Septemba 1939 Vita Vikuu vya Pili vya Dunia vilianza kwa shambulio la jeshi la Ujerumani ya Manazi dhidi ya Poland. Adolf Hitler alitumia fikra na mitazamo yake ya ubaguzi wa rangi kuhalalisha sera zake za kujipanua; na kwa muda mfupi akaweza kuvamia na kulikalia eneo kubwa la ardhi ya Ulaya na sehemu mojawapo ya kaskazini mwa Afrika. Wakati huohuo, Italia na Japan, ambazo zilikuwa waitifaki wa Ujerumani katika vita hivyo nazo pia zilianzisha uvamizi na ukaliaji wa maeneo mengine ya Afrika na Asia. Lakini ulipofika mwaka 1943, wakati jeshi la Ujerumani lilipokabiliwa na upinzani mkali wa wananchi wa Urusi na kusambaratishwa, mlolongo wa kushindwa na kurudi nyuma Wajerumani Manazi ulianza na hatimaye mnamo mwezi Mei 1945, Ujerumani ilisalimu amri bila masharti yoyote. Lakini kwa upande wa mashariki ya Asia, Japan iliendelea kupigana mpaka miji yake ya Hiroshima na Nagasaki iliposhambuliwa na Marekani kwa mabomu ya atomiki mnamo Agosti 1945. Watu kati ya milioni 40 hadi 50 waliuawa katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia vilivyosababisha pia hasara ya mabilioni ya dola kwa nchi mbalimbali.
Miaka 57 iliyopita katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria Shamsia, yaani tarehe 10 Shahrivar 1344 Hijria Shamsia, ilianzishwa kamati ya utumiaji wa nishati ya atomiki nchini Iran. Mwaka 1335, bunge la taifa la zama hizo lilipitisha mpango wa kuasisi "Kituo cha Atomiki cha Chuo Kikuu cha Tehran" na mnamo mwezi Azar 1344, mtambo wa megawati tano wa atomiki wa mafunzo na utafiti wa Iran ambao ulinunuliwa Marekani ulikuwa tayari kuanza kazi. Mwaka 1345 mtambo huo ulianza kutumika katika kituo cha utafiti cha Amir Abad Tehran na ungali unaendelea kufanya kazi hadi leo huku ukifanyiwa ukaguzi na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA. Mwaka 1352, Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran AEOI na bila kupoteza muda likafanya mazungumzo na nchi za Ulaya kwa ajili ya uJenzi wa vinu vya nyuklia nchini. Kufuatia mazungumzo hayo, mashirika mawili ya Ujerumani na Ufaransa yalikubali kujenga mitambo miwili ya nyuklia ya megawati elfu moja katika mji wa Bushehr kusini mwa Iran na kudhamini utoaji wa fueli kwa ajili ya mitambo hiyo. Lakini baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, na kinyume na ahadi yaliyozotoa, mashirika hayo yalisitisha ujenzi wa vinu hivyo na kuondoka nchini. Hata hivyo wanasayansi vijana wa Kiirani, kwa kushirikiana na shirika la nishati ya atomiki la Russia walikamilisha ujenzi wa kiwanda cha nyuklia cha Bushehr ambacho ni cha kwanza Mashariki ya Kati kinachozalisha nishati bila kutumika kwa malengo ya kijeshi; na hadi sasa kiwanda hicho kinaendelea na uzalishaji wa nishati hapa nchini.
Na miaka 53 iliyopita, yaani tarehe Mosi Septemba 1969, Kanali Muammar Gaddafi aliingia madarakani nchini Libya kupitia mapinduzi ya kijeshi. Kabla ya mapinduzi hayo Libya ilikuwa chini ya utawala wa kifalme; na Mfalme Idris I alikuwa ndiye mtawala wa nchi hiyo. Wakati Idris alipokuwa nchini Uturuki kwa matibabu, kundi la maafisa wa jeshi wakiongozwa na Kanali Gaddafi walifanya mapinduzi na kumwondoa madarakani mfalme huyo na kuasisi Jamhuri ya Kisoshalisti nchini Libya. Kuanzia hapo Libya ikajifungamanisha na Urusi na muda si mrefu baadaye sekta za mafuta na benki za nchi hiyo zikataifishwa. Baada ya kusambaratika Shirikisho la Kisovieti la Urusi, Gaddafi alianza kuelekea kambi ya Magharibi na kuyasabilia makampuni ya Kimagharibi maliasili ya mafuta ya nchi hiyo. Utawala wa kiimla wa Kanali Muammar Gaddafi uliangushwa na wanamapinduzi Agosti 21, 2011 na yeye mwenyewe akauawa baada ya miezi sita ya vuguvugu la Mwamko wa Kiislamu lililoikumba nchi hiyo na nyingine kadhaa za kaskazini mwa Afrika.