Jumanne tarehe 06 Septemba 2022
Leo ni Jumanne tarehe 9 Safar 1444 Hijria sawa na Septemba 6 mwaka 2022.
Katika siku kama ya leo miaka 1407 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, aliuawa shahidi Ammar bin Yassir, sahaba mkubwa wa Mtume Muhammad (saw) na msaidizi wa karibu wa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Ammar bin Yasir aliuawa katika vita vya Siffin vilivyojiri kati ya majeshi ya Imam Ali (as) na Muawiya bin Abi Sufian. Ammar alizaliwa miaka 57 kabla ya Hijra ya Mtukufu Mtume na wazazi wake wawili, yaani Yassir na Sumayyah, ndio waliokuwa mashahidi wa kwanza katika Uislamu. Sahaba huyu mtukufu alisimama imara dhidi ya maudhi ya makafiri na alishiriki katika vita mbalimbali pamoja na Bwana Mtume (SAW). Wakati mmoja Mtume alimwambia: "Ewe Ammar! Baada yangu kutatokea fitina, na katika hali hiyo mfuate Ali bin Abi Twalib na kundi lake, kwani Ali yuko pamoja na haki na haki iko pamoja na Ali.

Siku kama ya leo miaka 1023 iliyopita, alifariki dunia Abu Ali Maskawayh, mtaalamu, mwanahistoria na mwanafikra mkubwa wa Kiislamu. Miskawayh alizaliwa mwaka 320 katika mji wa Rei ulio karibu na mji mkuu wa Iran ya sasa. Miskawayh alikuwa mwalimu katika elimu za zama zake sambamba na kufanya utafiti katika elimu ya tiba, kemia, historia na falsala. Miongoni mwa athari zilizobakia za Abu Ali Miskawayh ni pamoja na kitabu kiitwacho "Tahdhibul-Akhlaq", "Tajaaribul-Umam" na "Jaavidaane Kherad."

Tarehe 9 Safar miaka 849 iliyopita yaani tarehe tisa Safar mwaka 595 Hijria, alifariki dunia Ibn Rushd Andalusi, msomi mkubwa wa falsafa wa Kiislamu. Abul-Walid Muhammad Bin Ahmad Bin Rushd, ambaye alikuwa miongoni mwa wasomi wakubwa wa elimu ya falsafa wa Kiislamu katika karne ya 6 Hijiria, alikuwa pia mtaalamu katika elimu za fiqhi, hadithi, fasihi, mantiki na elimu nyingine za wakati huo. Ibn Rushd aliyekuwa akiishi Andalusia (Uhispania ya leo) alikuwa mtu wa karibu kwa mfalme na miongoni mwa makadhi wa eneo moja la utawala wa kifalme. mwanafalsafa huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi kikiwemo cha 'Bidaayatul-Mujtahid' 'Falsafatu Ibn Rushdi' na 'al-Kulliyaat'.
Siku kama ya leo miaka 256 iliyopita, alizaliwa John Dalton, msomi na mtaalamu wa fizikia wa Kingereza katika familia ya watu wa kijijini. Kutokana na Dalton kupendelea sana elimu na licha ya kukabiliwa na matatizo mengi, alifanikiwa kwenda shuleni na kujifunza mambo mbalimbali. Ni wakati huo ndipo alipoanza kufanya uchunguzi na utafiti katika masuala mbalimbali ya kielimu. Dalton alibuni na kuvumbua mambo mengi katika uwanja wa fizikia, kemia na sayansi asilia baada ya utafiti mkubwa. Msomi huyo hakuchoka na badala yake aliendeleza utafiti mkubwa katika uga atomu. John Dalton alifariki dunia mwaka 1944.
Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita, jeshi la India lilianzisha mashambulizi makubwa dhidi ya Pakistan kufuatia machafuko ya zaidi ya mwezi mmoja katika mipaka ya nchi mbili hizo. Hivyo vilikuwa vita vya pili vikubwa kuwahi kutokea kati ya nchi mbili hizo jirani kuhusiana na eneo la Kashmir. Vita hivyo vilidumu kwa takribani wiki tatu. Pakistan na India zilikubaliana kusimamisha mapigano kufuatia upatanishi wa Urusi ya zamani. Viongozi wa nchi mbili hizo hatimaye waliafikiana kuanza mazungumzo tarehe 10 mwezi Juni mwaka 1966 huko Tashkent mji mkuu wa Uzbekistan nchini ya upatanishi wa Waziri Mkuu wa Urusi ya zamani. Japokuwa azimio la Tashkent lilibainisha njia za kumaliza mgogoro wa eneo la Kashmir na namna ya kuboresha uhusiano kati ya New Delhi na Islamabad na pia kukaribishwa na nchi mbalimbali duniani, lakini lilishindwa kumaliza hitilafu kati ya India na Pakistan kuhusu umiliki wa eneo la Kashmir.
Katika siku kama ya leo miaka 54 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Swaziland ilipata uhuru kutoka kwa Uingereza na kila inapowadia siku kama ya leo husherekewa nchini humo kwa anwani ya siku ya taifa. Kuimarika ukoloni wa Ulaya huko kusini mwa Afrika kulisababisha pia Swaziland kukaliwa kwa mabavu na wakoloni wa Ulaya. Hatimaye katika siku kama ya leo nchi hiyo ndogo ya kusini mwa Afrika ilipata uhuru. Swaziland ina ukubwa wa kilomita mraba 17364 na kijiografia iko kusini mwa bara la Afrika ikiwa inapakana na nchi za Msumbiji na Afrika Kusini.

Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, baada ya kupamba moto harakati za mapambano ya wananchi Waislamu wa Iran dhidi ya utawala wa kidikteta wa Shah, kulifanyika maandamano makubwa katika maeneo mbalimbali kote nchini. Kwa sababu hiyo utawala wa Shah uliokuwa umepatwa na wasiwasi mkubwa kutokana na harakati hizo za mapinduzi, uliamua kupiga marufuku maandamano ya aina yoyote ile. Wakati huo huo huo Imam Ruhullah Khomeini MA aliyekuwa uhamishoni huko Najaf nchini Iraq alitoa taarifa akiwataka wananchi wa Iran kudumisha harakati za mapambano. Katika sehemu moja ya taarifa yake kwa wananchi, Imam Khomeini aliyataja maandamano yanayofanywa kwa ajili ya kufikia malengo ya Kiislamu kuwa ni ibada.
