Jumamosi, 10 Septemba, 2022
Leo ni Jumamosi tarehe 13 Mfunguo Tano Safar 1444 Hijria sawa na tarehe 10 Septemba 2022 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1141 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alifariki dunia mtaalamu wa hadithi wa Kiislamu Abu Abdulrahman Ahmad bin Shuaib Nasai, maarufu kwa jina la Sheikhul Islam. Nasai alizaliwa mwaka 220 Hijria katika mojawapo ya vijiji vya Khorasan kaskazini mwa Iran na akaelea nchini Misri akiwa kijana. Akiwa huko alipata elimu ya fiqhi na hadithi na akaanza kufunza taaluma hizo. Baadaye Sheikhul Islam Nasai aliekele Damascus, Syria ambako alibainisha sifa na maadili ya watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Aali zake) na kupigwa mara kadhaa na wapinzani wa Ahlul Bait. Hatimaye alielekea Hijaz na kuishi mjini Makka. Nasai ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha "Khasaisu Amirul Muuminina Ali" na kile cha "Sunanun Nasai" ambacho ni miongoni mwa vitabu mashuhuri vya hadithi vya Kiislamu. ***
Katika siku kama ya leo miaka 1074 iliyopita alifariki dunia mtaalamu wa fasihi, fiqhi na tafsiri ya Qurani Muhammad Azhari Harawi. Alizaliwa mwaka 282 Hijria katika eneo la Harat nchini Afghanistan.Harawi alitekwa nyara na Waarabu wa jangwani akiwa safarini kuelekea Makka kwa ajili ya ibada ya hija na huko alijifunza lahaja asilia ya lugha ya Kiarabu ambayo aliitumia katika vitabu vyake. Mtaalamu huyo wa lugha ameandika vitabu vingi vya tafsiri na hadithi. Kitabu chake muhimu zaidi ni kile cha "Tahdhibul Lugha." ***
Miaka 108 iliyopita yaani tarehe 10 Septemba mwaka 1914 kulitokea vita baina ya majeshi ya Ujerumani na Russia kando kando ya maziwa ya Masurian. Vita hivyo vilianza kufuatia kuzuka Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia na kujiunga Russia na kambi ya nchi waitifaki. Katika vita hivyo vya Masurian, Wajerumani wakiongozwa na kamanda Paul Von Hindenburg walifanikiwa kupata ushindi na kuwauwa takribani wanajeshi 20,000 wa Russia na kuwateka nyara wengine 45,000. Hatimaye mwaka 1917 baada ya kutokea mapinduzi nchini Russia, nchi hiyo ilijiondoa katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia. ***
Siku kama ya leo miaka 68 iliyopita, mtetemeko mkubwa wa ardhi ulitokea katika eneo la Orleansville kusini magharibi mwa Algeria. Janga hilo la mtetemeko wa ardhi lilisababisha mji mmoja uliokuwa na wakazi 30,000 kuangamia na watu 10,000 kupoteza maisha yao. Fauka ya hayo, makumi ya maelfu ya wananchi wa kusini magharibi mwa Algeria walibaki bila ya makazi. Mtetemeko huo vilevile ulitoa pigo kubwa kwa miundo mbinu ya uchumi wa nchi hiyo. ***
Katika siku kama ya leo miaka 43 iliyopita yaani tarehe 19 Shahrivar aliaga dunia Sayyid Mahmoud Taleghani kiongozi wa kidini, mwanaharakati, mwanamapambano na mfasiri wa Qur'ani Tukufu wa Iran. Ayatullah Taleghani alikuwa akifuatilia kwa karibu matukio ya kisiasa ya Iran tangu akiwa kijana. Kipindi fulani alitiwa nguvuni na kufungwa jela miaka miwili na utawala wa Kitaghuti wa Shah uliokuwa ukitawala hapa nchini kwa kosa la kushiriki katika harakati ya wananchi ya tarehe 15 Khordad. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliteuliwa na Imam Khomeini kuwa Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Imam wa Swala ya Ijumaa ya Tehran. ***
Na tarehe 10 Septemba mwaka 1990 yaani miaka 32 iliyopita, Samuel Kanyon Doe aliyekuwa rais wa Jamhuri ya Liberia aliuawa na kundi la waasi. Samuel Doe alishika madaraka ya nchi mwaka 1980 akiwa sajenti mwenye umri wa miaka 29 tu baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji damu akitumia umaskini, kupanda kwa gharama za maisha na hali mbaya ya wananchi. Hata hivyo utawala wa kidikteta wa Samuel Doe haukufanikiwa kupunguza machungu na mashaka ya Waliberia bali kinyume chake alipanua zaidi hitilafu za kikabila na kuzidisha matatizo ya kiuchumi na kijamii. Vilevile alitayarisha uwanja wa kuporwa zaidi utajiri wa madili ya almasi ya nchi hiyo kupitia njia ya kupanua zaidi uhusiano wa Liberia na Marekani na utawala haramu wa Israel. Mauaji ya Samuel Doe yalifuatiwa na vita vya ndani nchini Liberia ambavyo viliendelea kwa kipindi cha miaka 15 na kusababisha vifo vya watu karibu laki mbili na nusu. ***