Sep 11, 2022 01:20 UTC
  • Jumapili, Septemba 11, 2022

Leo ni Jumapili, mwezi 14 Mfunguo Tano Safar 1444 Hijria, sawa na tarehe 11 Septemba, 2022 Milaadia

Katika siku kama ya leo miaka 812 iliyopita sawa na tarehe 14 Safar mwaka 632 Hijria alifariki dunia Abul Mahasin Bahauddin mashuhuri kwa jina la Ibn Shidad, fakihi, kadhi na mwanahistoria wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 539 huko Mosul, moja ya miji ya Iraq na alihifadhi Qur'ani akiwa bado mtoto na baadaye akajifunza hadithi, tafsiri na kusoma Qur'ani na kupata umahiri mkubwa katika taaluma hizo. Ibn Shidad alifanya safari katika nchi mbalimbali za Kiislamu kwa ajili ya kutafuta elimu. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni an Nawadir al Sultwaniya, Dalailul Ah-kam na al Aswaa kinachozungumzia maisha ya Nabii Musa A.S. na mapambano yake dhidi ya Firauni.

Ibn Shidad

 

Miaka 437 iliyopita katika siku kama hii ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alizaliwa Mulla Muhsin Faidh Kashani, aliyekuwa faqihi, mpokezi wa hadithi, mwanafalsafa na arifu mkubwa wa Kiislamu nchini Iran. Faidh Kashani alipata elimu za fiqhi, hadithi, tafsiri na falsafa kwa wanazuoni wakubwa wa zama zake kama Muhammad Taqi Majlisi, Sheikh Bahai na Mulla Sadra. Msomi huyo mkubwa ameandika vitabu vingi, mashuhuri zaidi vikiwa ni tafsiri ya Qur'ani ya al Swafi, Mafatiihu Sharaai', al Wafi na al Mahajjatul Baidhaa.

Kaburi la Mulla Muhsin Faidh Kashani

 

Siku kama ya leo miaka 224 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Milaadia, kisiwa cha Sri Lanka kilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na wakoloni wa Kiingereza. Kisiwa hicho ambacho kijiografia kipo kusini mwa Bara Hindi, kuanzia karne ya 3 Miladia kilikuwa kikihesabiwa kuwa moja ya vituo muhimu vya kiutamaduni vya Mabudha.

Sri Lanka

 

Miaka 74 iliyopita katika siku kama hii ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Milaadia, aliaga dunia Muhammad Ali Jinnah, mwasisi wa Pakistan. Jinnah alizaliwa mwaka 1876 katika mji wa Karachi kusini mwa Pakistan. Muhammad Ali Jinnah alikuwa miongoni mwa shakhsiya walioasisi chama cha Muslim League mnamo mwaka 1906. Chama cha Muslim League awali kilikuwa kikijishughulisha na masuala ya kiutamaduni na kidini, lakini baadaye kikaingia katika uwanja wa siasa na kutaka kuundwa nchi huru kwa ajili ya Waislamu.

Muhammad Ali Jinnah

 

Siku kama ya leo miaka 49 iliyopita, Jenerali Agustino Pinoche kamanda wa wakati huo wa vikosi vya majini vya Chile aliipindua serikali halali ya Salvador Alande katika mapinduzi yaliyoungwa mkono na Marekani. Alande ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kisoshalisti cha Chile, alichaguliwa kuwa Rais wa nchi hiyo mwaka 1970.

Jenerali Agustino Pinoche

 

Na miaka 21 iliyopita katika siku kama ya leo yaaani tarehe 11 Septemba mwaka 2001, ndege mbili kati ya nne za abiria za Marekani zilizotekwa nyara ziligonga minara miwili pacha ya jengo la Biashara la Kimataifa la mjini New York huku ndege moja ikigonga jengo la Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) huko Washington. Ndege ya nne ililengwa ikiwa katika anga ya Pensylvania na kuangushwa. Baadhi ya ghorofa za jengo la Biashara ya Kimataifa ziliporomoka na sehemu ya jengo la Pentagon pia ikaharibiwa katika mashambulizi hayo ya kigaidi. Karibu watu 3200 waliuawa katika mashambulizi hayo. Marekani ilitangaza kuwa mtandao wa al Qaida uliokuwa ukiongozwa na Usama bin Laden raia wa Saudi Arabia, ndio uliohusika na mashambulizi hayo. Baada ya matukio ya Septemba 11 nchini Marekani, kulianza wimbi la ubaguzi na mashambulizi dhidi ya Waislamu na matukufu ya dini yao katika nchi za Magharibi.

Shambulio la Septemba 11