Sep 13, 2022 21:41 UTC
  • Jumatano tarehe 14 Septemba 2022

Leo ni Jumatano tarehe 17 Safar 1444 Hijria inayosadifiana na Septemba 14 mwaka 2022.

Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita yaani tarehe 23 Shahrivar mwaka 1357 Hijria Shamsia kulifanyika maandamano makubwa hapa nchini kuwaenzi mashahidi waliokuwa wameuawa na vibaraka wa Shah siku kadhaa kabla yake. Siku hiyo umati mkubwa wa watu ulimiminika katika makaburi ya Behest Zahraa mjini Tehran kuwaenzi mashahidi hao. Askari wa utawala wa Shah walikuwa na nia ya kuzuia maandamano hayo lakini umati mkubwa wa wananchi walioshiriki maandamano ulidumisha malalamiko yao dhidi ya utawala wa kidikteta wa Shah huko wakipiga nara za: “Iran ni nchi yetu na Khomeini na kiongozi wetu.”

Maandamano ya wananchi dhidi ya Shah

Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, hati ya Jumuiya ya Nchi Zinazozalisha Mafuta kwa Wingi Duniani (OPEC) ilitiwa saini na nchi za Iran, Saudia, Iraq, Kuwait na Venezuela. Jumuiya hiyo ilianzishwa kwa lengo la kukabiliana na makampuni makubwa ya mafuta ya Magharibi ambayo yalikuwa yakisimamia uvumbuzi, uchimbaji na uuzaji wa bidhaa hiyo kimataifa na kuainisha bei ya bidhaa hiyo muhimu kwa maslahi yao binafsi na kwa madhara ya nchi zalishaji. Licha ya kwamba awali jumuiya hiyo haikuwa na nguvu wala ushawishi wowote, lakini ilikuja kupata nguvu zaidi baada ya nchi kadhaa zikiwemo, Algeria, Libya, Nigeria, Qatar, Imarat, Gabon, Indonesia na Ecuador ambazo ni wazalisha wa mafuta kujiunga nayo.

Katika siku kama ya leo miaka 210 iliyopita, moja kati ya ajali kubwa za moto ulimwenguni ilitokea katika mji mkuu wa Russia Moscow. Moto huo uliwashwa kwa makusudi. Ilikuwa imepita siku moja tu, tangu mji huo uvamiwe na kukaliwa kwa mabavu na majeshi ya Napoleone Bonaparte, wakati mji huo ulipochomwa moto kwa amri ya mtawala wa wakati huo wa mji huo. Lengo la mtawala huyo lilikuwa ni kuyafanya majeshi ya Bonaparte yashindwe kustafidi na suhula za mjini humo katika kuendelea kubaki katika mji huo. Moto huo mkubwa uliteketeza na kuharibu kabisa robo tatu ya mji wa Moscow.

Katika siku kama ya leo miaka 189 iliyopita, alizaliwa Sheikh Abdul Rahim Sultanul-Qurrai Tabrizi, qaari mkubwa wa Qur’ani Tukufu na mmoja wa walimu mashuhuri wa taaluma ya qiraa, huko mjini Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran. Baada ya kujifunza taaluma hiyo kutoka kwa baba yake, Sultanul-Qurrai Tabrizi alifahamiana na Sheikh Shamil Daghestani na kushirikiana naye. Wakati Sheikh Shamil Daghestani alipoandaa jeshi kwa ajili ya kupambana na Warusi, Sultanul-Qurrai alifanya safari kuelekea Daghestani ili kushiriki katika harakati hiyo. Baadaye alirejea Tabriz na kuanzisha chuo cha kisomo cha Qur’ani na ni wakati huo ndipo alipopewa lakabu ya Sultanul-Qurrai. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na ‘Risala katika Elimu ya Tajwidi’. Sultanul-Qurrai alifariki dunia mwaka 1336 Hijiria mjini Tabriz.

Siku kama ya leo miaka 548 iliyopita, alizaliwa Muhammad Mustafa Imad, maarufu kwa jina la  Abus-Su’ud, faqihi na mfasiri wa Kiislamu katika kijiji cha Mudares, karibu na mji wa Istanbul, Uturuki. Baada ya kukamilisha masomo yake Abus-Suud  alianza kufundisha sambamba na kujishughulisha na kazi ya ukadhhi mjini Istanbul. Aliendelea na kazi hiyo hadi mwishoni mwa uhai wake. Msomi huyo alifanya jitihada kubwa za kuhakikisha kwamba sheria za utawala wa Kiothmani (Ottoman Empire) zinaoana na sheria za Kiislamu. Mbali na kujua lugha ya Kituruki, msomi huyo pia alikuwa hodari katika lugha za Kifarsi na Kiarabu na aliandika mashairi kwa kutumia lugha hizo. Miongoni mwa vitabu vya Abus-Suud ni pamoja na 'Tafsiru Abis-Suud' 'Dua Nameh' 'Qanun Nameh' na 'Mafrudhaat.'

Siku kama ya leo miaka 633 iliyopita, utawala wa Othmania uliidhibiti na kuikalia kwa mabavu ardhi ya Serbia. Tukio hilo lilijiri wakati wa operesheni za utawala huo za kuzitia katika miliki yake ardhi za Ulaya. Ushindi huo ulipatikana katika kipindi cha ufalme wa Sultan Murad wa Kwanza Mfalme III wa utawala huo. Licha ya kuweko uasi wa wananchi wa Serbia, lakini ardhi yao iliendelea kuwa chini ya udhibiti wa Ufalme huo kwa karibu karne tano. 

Sultan Murad wa Kwanza