Sep 23, 2022 23:01 UTC
  • Jumamosi, 24 Septemba, 2022

Leo ni Jumamosi tarehe 27 Mfunguo Tano Safar 1444 Hijria mwafaka na tarehe 24 Septemba 2022 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 83 iliyopita, ndege za kijeshi za Ujerumani zilianza kufanya mashambulio makubwa dhidi ya mji mkuu wa Poland, Warsaw. Mashambulio hayo yalifanyika sambamba na kuanza Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na yaliendelea kwa muda wa siku tatu. Hatimaye wananchi wa mji huo walisalimu amri mbele ya majeshi ya Ujerumani baada ya mapambano ya siku kumi na moja. Mashambulio hayo ya kinyama yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 15,000. ***

Muonekano wa Warsaw mji mkuu wa Poland

 

 

Katika siku kama ya leo miaka 48 iliyopita, Guinea Bissau ilitangaza uhuru wake kutoka kwa mkoloni Mreno. Guinea Bissau iligunduliwa mwaka 1446 na Mwana Mfalme Henry aliyekuwa akitawala Ureno pamoja na wenzake na kuwa koloni la nchi hiyo. Guinea Bissau ambayo ilikuwa ikijulikana kwa jina la Guinea Ureno, ilikuwa miongoni mwa vituo vya biashara ya utumwa ya wazungu katika karne za 17 na 18. Na hatimaye ilipofika mwaka 1974, Ureno ikakubali kuwa huru nchi ya Guinea Bissau. Guinea Bissau iko kaskazini magharibi mwa Afrika na katika pwani ya Bahari ya Atlantic. ***

Bendera ya Guinea Bissau

 

Miaka 44 iliyopita katika siku kama hii ya leo, vikosi vya usalama vya utawala wa Baath nchini Iraq vikishirikiana na utawala wa Shah viliizingira nyumba ya Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu huko Najaf. Kwa kuzingatia uhusiano wake mzuri na utawala wa Shah, utawala wa zamani wa Iraq ulimtaka Imam Khomeini asifanye mahojiano na waandishi wa habari, kutoa taarifa, kuhutubia wala kuzungumzia hali ya mambo ya Iran dhidi ya utawala wa Shah. Imam Khomeini aliwajibu kwa kusema kuwa: "Nitatekeleza wajibu wangu wa kisheria popote pale nitakapokuwa." Baada ya hapo, serikali ya wakati huo ya Iraq, ilimlazimisha Imam Khomeini kuondoka Iraq na hatua hiyo ikaandaa uwanja wa hijra ya kihistoria ya Imam Khomeini ya kuelekea Paris, Ufaransa na kupamba moto harakati za Mapinduzi ya Kiislamu. ***

Imam Khomeini akiondoka Iraq na kuelekea Ufaransa

 

Na siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Abdul-A'alaa Mussawi Sabzawari mwanachuoni mashuhuri wa Iran. Ayatullah Sabzawari alizaliwa mwaka 1290 Hijiria Shamsia, katika mji wa Sabzawar uliopo kaskazini mashariki mwa Iran. Mwanachuoni huyo alipata elimu ya msingi katika miji ya Sabzawar na Mash’had, na baadaye alielekea Najaf nchin Iraq na kupata elimu ya juu ya maarifa ya Kiislamu. Ayatullah Sayyid Abdul-A'alaa Mussawi Sabzawari ameandika vitabu vingi na maarufu zaidi ni tafsiri ya Qur'ani ya ‘Mawaahibul-Rahman fii Tafsiril-Qur’an’ chenye juzuu 20, ‘Muhadh-Dhibul-Ahkaam fii Bayaanil-Halali wal-Haraam’ chenye juzuu 30 na ‘Tahdhibul-Usuul’ chenye juzuu mbili. ***

yatullah Sayyid Abdul-A'alaa Mussawi Sabzawari