Akhlaqi Katika Uislamu (31)
Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 31 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki ambacho kwa leo kitazungumzia miongozo mingine ya kiakhlaqi ya dini tukufu ya Uislamu. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.
Mpendwa msikilizaji, katika vipindi kadhaa vilivyopita tumebainisha nukta kadhaa kuhusu mambo yanayoweza kuwa na taathira kubwa katika kuimarisha mihimili ya ndoa na familia. Miongoni mwa mambo muhimu zaidi kati ya hayo ni kuifanya familia mahali salama na pa amani kimaadili; kwani kama ambavyo huwezi kutarajia matunda mazuri na mazao bora katika ardhi kavu, yabisi na isiyo na rutuba, ndivyo vivyo hivyo tusiwe na mategemeo ya kupata watoto wema walioeleleka na kufunzika, katika familia ambayo haina uzima wa kinafsi wala usafi wa kimaadili. Ili kuifanya familia iwe na mazingira safi na salama, hatua kuu na ya msingi ni kuimarisha ndani yake maadili na itikadi sahihi za dini.
Imam Jaafar Sadiq (AS) amesema: "kabla fikra za upotoshaji hazijaziteka nyoyo zao na mbegu potofu hazijapandwa kwenye ardhi ya nafsi zao, yatangulieni hayo kwa kuwajuza watoto wenu mafundisho ya Uislamu halisi." Al Kafi 1/43.
Kwa mujibu wa maneno haya matukufu, jukumu la pamoja la akina baba na akina mama ni kuhakikisha kwa upande mmoja, wao wenyewe wanakuwa na uelewa wa mafundisho ya kujenga nafsi, ya Uislamu; na kwa upande mwingine kuzifahamu barabara fikra na mitazamo potofu ili kuweza kuhifadhi fitra ya kitauhidi na kuyalinda maumbile safi ya watoto wao na mitazamo na mielekeo yenye sumu ya shirki na ukafiri.
Hatua nyingine ya msingi ya kuifanya familia iwe na mazingira salama, inapasa ichukuliwe na wazazi hasa mama, ambao ndio wenye nafasi muhimu zaidi katika malezi ya watoto wao; nayo ni kuzipalilia mbegu za thamani za kiakhlaqi na heshima za kiutu ndani ya nafsi zao.
Imam Ali (AS) ametubainishia utukufu wa kujipamba na akhlaqi njema aliposema: "Hata kama tungekuwa hatuna matumaini na imani ya kupata Pepo wala hofu ya kuchelea moto, na malipo ya athawabu na adhabu (kutokana na amali zetu), basi bado ingepasa na ingestahiki kujipamba kwa akhlaqi njema, kwa sababu ndizo zinazotuonyesha njia ya mafanikio." (Mustadrakul-Wasaail 11/193)
Moja ya vielelezo vya wazi vya kiakhlaqi ni adabu katika kauli na tabia ndani ya taasisi ya ndoa na familia. Inapasa kauli nzuri na za murua na maneno ya heshima, upendo na ukweli yatawale ndani ya familia; na watu wake wajitahidi kujiweka mbali kabisa na utumiaji wa maneno makali, yasiyo na nadhari na mantiki na yanayoweza kutibua na kuvuruga hisia za mtu. Lakini mbali na hayo, tabia na mienendo ya watu inapasa iwe ya namna ambayo, heshima na staha ya kila mmoja ndani ya familia, hususan baba na mama, ambao wana hadhi na daraja maalumu katika utamaduni wa Kiislamu, ichungwe na kuzingatiwa.
Moja ya madhihirisho makubwa yanayoakisi mwenendo wa watu ni aina ya mavazi wanayovaa watu wa familia. Hata kama familia inafahamika kuwa ni sehemu ya maisha ya faragha ya watu, lakini watoto wanapofikia umri wa baleghe au uwezo wa kiakili wa kufahamu mambo, haipasi mtu yeyote wa familia kuvaa mavazi yasiyo ya staha na yanayochochea ghariza za kijinsia, kwa sababu yanaweza kuwasukuma jamaa wa familia kwenye ufisadi. Hakuna shaka kuwa kuwepo kwa utamaduni wa watu kuwa na haya na soni kutaifanya familia iwe na watu wanaojiheshimu na kustahiana; hali ambayo inapatikana kwa kuchunga mipaka ya mahusiano yakiwemo ya aina ya mavazi wanayovaa jamaa wa familia hiyo.
Moja ya sera na mipango michafu ya Uistikbari wa dunia ni kueneza utamaduni wa kutembea uchi na kushamirisha maingiliano ya kimwili yasiyo na mipaka, unayoyachochea kupitia usambazaji wa filamu za ngono katika ulimwengu wa sinema, televisheni na intaneti, lengo kuu likiwa ni kukitumbukiza kizazi cha vijana kwenye lindi la ufuska na kuwafanya wakatae kufuata taratibu za ufungaji ndoa rasmi, kwa kuishia kuanzisha mahusiano haramu ya kingono huku wakijiridhisha na hoja kwamba: "kuna haja gani ya kununua ng'ombe, wakati inawezekana kupata maziwa freshi kila siku!"
Ni wazi mpendwa msikilizaji, kwamba kama kizazi cha vijana kitaporomoka kimaadili hadi kufikia kiwango hiki hakitachunga tena mpaka wowote ule. Kitakachofutia ni kupoteza hadhi na heshima yake ya kiutu na kuwa duni zaidi kuliko chochote kile kilicho duni. Hapo huishia kughariki kwenye dimbwi la pumbao, kutojielewa na kutangatanga; na kama isemavyo Qur’ani, kuwa mithili ya wanyama, bali duni zaidi ya wanyama, kutokana na kupitisha maisha yao bila madhumuni wala lengo lolote la kimantiki.
Msingi mwingine muhimu sana wa kuihifadhi na kuienzi familia, ni desturi na utaratibu wa kuamiliana, kulahikiana na kutembeleana mtu na jamaa zake; suala ambalo Uislamu umelitilia mkazo sana, mpaka ikaelezwa kwamba kukata mahusiano na jamaa ni moja ya madhambi makuu. Mahusiano ya kiudugu yanapokuwa ya kuheshimiana na kustahiana huimarisha misingi na thamani za kidini na kiutu; na pale watu wanapokuwa na mazoea ya kutembeleana, fikra na nyoyo zao huwa na ukuruba zaidi, na mapenzi na masikilizano baina yao huzidi kuongezeka. Lakini pale watu wanapokata udugu au hata kama ukiwepo, ukawa si wa uhusiano mzuri, moyo wa upendo na urafiki baina ya jamaa wa koo na familia hudhoofika, hasahasa kwa watoto, ambao ndio wanaotarajiwa kuja kujenga vizazi vijavyo. Mahusiano dhaifu ya kiujamaa huwaweka mbali watoto hao na thamani za kidini na kiakhlaqi. Ifikiapo hatua hiyo, si tu hatutaweza kuzirekebisha fikra na tabia zao, bali si hasha kukata udugu au kuwa na mahusiano ya kiudugu yasiyo na upendo na maelewano, kukayumbisha pia misingi yetu sisi wenyewe ya imani na itikadi za dini. Kwa hiyo ili kuepukana na madhara hayo, inatupasa tuyaangalie upya na kuyarekebisha pale yanapoharibika, mahusiano yetu ya kiudugu na kifamilia. Na kwa maelezo hayo mpendwa msikilizaji niseme pia kuwa, sehemu ya 31 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 32 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/