Nov 10, 2022 17:32 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (42)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 42 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki ambacho maudhui yake ya leo ni kuhusu umuhimu na udharura wa watawala wa Kiislamu kuchunga na kuzingatia akhlaqi za kiuchumi. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Katika mfululizo wa 41 wa kipindi hiki tulieleza kwamba, katika mfumo wa kiuchumi wa Uislamu "uadilifu" una nafasi na hadhi maalumu. Lakini kama tulivyoashiria pia, viongozi wa jamii, mtindo wao wa maisha na mfumo wa uongozaji na uendeshaji vinaweza kutoa mchango athirifu katika kusimamisha "uadilifu wa kiuchumi".

Moja ya vigezo na ruwaza bora za uadilifu ni Mtume SAW ambaye Mwenyezi Mungu Mtukufu amemuelezea katika aya ya 21 ya Suratul-Ahzab kwamba sira na mwenendo wake ni mfano wa kuigwa na mwongozo wa kufuatwa na watu wanaomwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Kiyama na wanaotaraji malipo mema ya Mola katika siku hiyo.

Imam Ali AS, ambaye alilelewa na kukulia kwenye chuo cha Utume, ameifafanua nukta hiyo ya mwenendo ulio ruwaza na mfano wa kuigwa wa Mtume SAW katika hotuba ya 60 ya Nahjul-Balagha aliposema: "mja anayependeza zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule anayemfanya Mtume wake kuwa ndiye kigezo chake". Kisha mtukufu huyo akaanza kufafanua sira na mwenendo wa maisha wa Mtume wa Allah, ambaye alikuwa dhihirisho la sifa zote za uadilifu katika umma wa Kiislamu kwa kusema: "Mtume SAW alikuwa akikaa kitako chini (bila kuweka jamvi) kula chakula, akikaa na kuchanganyika na watumwa, akishona mwenyewe viatu vyake na akitia kiraka mwenyewe nguo yake, akipanda punda asiye na soji na hata akimpakia mtu nyuma yake. Siku alipoona pazia lenye anuai za picha kwenye mlango wa nyumba yake, alimwita mke wake na kumwambia: liondoe, kwani kila ninapolitupia jicho huikumbuka dunia na mapambo yake. Mtume SAW

aliipa mgongo dunia kwa moyo wake, akaing'oa kumbukumbu yake ndani ya nafsi yake, na akipenda mapambo yake yafichike mbele ya macho yake ili asiifanye ikawa vazi lake wala kuichukulia kuwa makao yake na kujenga tumaini la kubaki ndani yake. Kwa hiyo akaitoa ndani ya nafsi yake, akaivua ndani ya moyo wake na akaiondoa mbele ya macho yake. Aliondoka duniani tumbo tupu kwa njaa na akaingia akhera roho yake ikiwa safi iliyotakasika; na akaitika wito wa Mola wake kwa imani kamili; na kwa muda wote alioishi duniani hakuweka jiwe juu ya jiwe jengine kujijengea kasri lolote".

Kisha Imam Ali AS akasema: "Ni ihsani kubwa iliyoje aliyotufanyia Mwenyezi Mungu kwa kutuletea kiongozi kama yeye ili awe ruwaza na kigezo chetu cha kufuata".

Baada ya hayo tuliyoeleza mpendwa msikilizaji, inafaa sasa tujiulize suali la msingi, nalo ni kwamba, watawala waliojidai kuwa makhalifa wa Bwana Mtume SAW, hasa wa tawala za kiimla za Bani Umayya na Bani Abbas, ni kweli walifuata njia ileile aliyopita Mtume huyo wa Allah kwa ajili ya kusimamisha uadilifu na kuondoa ubaguzi, upendeleo na ufa wa kimatabaka? Kujibu suali hili tunaweza kusema kwamba, japokuwa fat-hu na ushindi kadhaa wa kadha uliopatikana baada ya kutawafu na kuaga dunia Bwana Mtume SAW zilipanua maeneo yaliyokuwa chini ya mamlaka ya Waislamu, lakini upataji ngawira nyingi vitani uliwafanya watawala wa Kiislamu wawe na utashi na mapenzi makubwa ya vitu vya kimaada, mpaka ukaifanya jamii ya Kiislamu ianze kusahau kidogo kidogo utamaduni wa kutetea na kusimamia haki na uadilifu; na badala yake kuvutiwa na kutekwa na utamaduni wa kibwanyenye, kupenda anasa, kujilimbikizia mali, kupenda ulaji rushwa, unyonyaji na uonevu. Tutadondoa hapa mifano michache tu ya takwimu za kutisha, za matukio hayo kama yalivyosimuliwa kwenye vyanzo vya kuaminika vya vitabu vya historia:

Khalifa wa Tatu Othman Ibn Affan, alikuwa mtu wa mwanzo, kinyume na ilivyokuwa sira ya Bwana Mtume SAW, kukengeuka mkondo wa uadilifu wa Kiislamu. Aligawa utajiri wa Baitul-Mal kwa kuwatunukia jamaa na watu wake wa karibu bila hesabu wala makadirio, ilhali ufukara na umasikini ulikuwa umekithiri ndani ya jamii ya Waislamu. Alimpatia Talha, sahaba maarufu wa Bwana Mtume SAW, shehena ya dhahabu ya ngamia mia tatu na dinari laki mbili.

Zubair, sahaba mwingine mashuhuri wa Bwana Mtume SAW, ambaye naye pia alitajirika kupitia njia hiyo, alikuwa na nyumba kumi na moja Madina, nyumba mbili Basra, nyumba moja katika mji wa Kufa na nyumba nyingine moja Misri; na kwa mujibu wa baadhi ya simulizi, jumla ya mali alizoacha zilifika dinari za dhahabu milioni hamsini na tisa na laki nane. Katika zizi la sahaba Abdulrahman Ibn Auf, kulikuwa na farasi elfu moja, ngamia elfu moja na kondoo elfu kumi. Wakati sahaba Zaid Ibn Thabit alipofariki dunia, aliacha rundo la dhahabu na fedha, kiasi kwamba warithi wake walilazimika kulivunjavunja kwa shoka ili waweze kugawana. Milki zake na mashamba aliyoacha yalikuwa na thamani ya dinari laki moja. Khalifa Othman alimpatia Marwan ngawira zilizopatikana katika ardhi za Afrika zilizokombolewa, mbali na dirhamu laki moja na nusu pamoja na eneo la Fadak. Alimpa pia ndugu wa Marwan aitwaye Harith dirhamu laki tatu.

Suali la kujiuliza hapa ni je, ni wao waliofuata sira na mwenendo wa Mtume SAW, au Imam Ali AS, ambaye katika Ukhalifa wake, wakati ndugu yake aitwaye Aqil alipomtaka amgaie kitu katika Baitul-Mal, alichukua chuma na kukiweka motoni kisha akakiweka karibu na mikono yake. Wakati Aqil alipolalama kwa muunguzo wa joto lake, Imam Ali alimwambia: "Wewe unalalama na kuungulika kwa moto mdogo na wa kupita wa duniani, unataka ukaniingize mimi kwenye moto wa milele?" Katika kisa kingine, wakati binti wa Imam Ali AS alipoazima kidani kwenye Baitul-Mal kwa kuchukuliwa dhamana na mtu, pale mtukufu huyo alipokiona kidani hicho shingoni mwa binti yake huyo aliamuru kirejeshwe haraka kwenye hazina ya Waislamu na akamwambia: "kama usingekuwa umekichukua kuwa ni amana, basi ungekuwa mwanamke wa mwanzo katika Bani Hashim ambaye ningemkata mkono wake kwa kosa la wizi…"

Kwa masikitiko ni kuwa, uporaji katika hazina ya Waislamu haukuishia katika utawala wa Khalifa Othman Ibn Affan, kwani msingi huo mbaya uliojengwa katika utawala wake ulifikia kilele katika zama za Muawiya, ambaye aliugeuza ukhalifa kuwa ufalme, pale nyumba na maskani zilipogeuzwa kuwa makasri; na hali ya udugu na usawa ilipogeuzwa kuwa ya ubaguzi, upendeleo na ufa mkubwa wa kimatabaka baina ya watu. Abu Dhar al Ghifari, sahaba mwaminifu wa Bwana Mtume SAW, alibaidishwa na kupelekwa uhamishoni katika eneo la Ar-Rabadha akaaga dunia hukohuko akiwa peke yake kwenye hali ya upweke na ukiwa. Kosa lake lilikuwa ni kulalamikia ulimbikizaji mali uliofanywa na Othman Ibn Affan na Muawiya bin Abi Sufiyan. Baada ya kuhitimishwa utawala wa Bani Umayya, sera hizo mbovu na chafu zilirithiwa na Bani Abbas; ambao nao pia walichota kwenye mfuko wa hazina ya Waislamu kadiri walivyoweza kwa ajili ya kujineemesha na kujistarehesha. Waliitumia hazina hiyo kujengea makasri ya kifahari, mbali na kuwatunukia na kuwazawadia jamaa zao na wale waliokuwa wanyenyekevu na watiifu kwa makhalifa; na hivyo ndivyo ulivyozikwa rasmi uadilifu wa kiuchumi. Na kwa maelezo hayo basi mpendwa msikilizaji niseme pia kuwa sehemu ya 42 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 43 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/